Marko
4 Naye akaanza tena kufundisha kando ya bahari. Na umati mkubwa sana ukakusanyika karibu naye, hivi kwamba akapanda ndani ya mashua akaketi baharini, lakini umati wote kando ya bahari ulikuwa juu ya ukingo. 2 Kwa hiyo akaanza kuwafundisha mambo mengi kwa vielezi na kuwaambia katika kufundisha kwake: 3 “Sikilizeni. Tazameni! Mpanzi alitoka kwenda kupanda. 4 Naye alipokuwa akipanda, baadhi ya mbegu ikaanguka kando ya barabara, na ndege wakaja wakaila kabisa. 5 Na mbegu nyingine ikaanguka juu ya mahali penye miamba-miamba ambapo, bila shaka, haikuwa na udongo mwingi, nayo ikachipuka mara hiyo kwa sababu ya kutokuwa na kina cha udongo. 6 Lakini jua lilipochomoza, ikaunguzwa, na kwa sababu ya kutokuwa na mzizi ikanyauka. 7 Na mbegu nyingine ikaanguka katikati ya miiba, na ile miiba ikamea na kuisonga, na haikutoa tunda lolote. 8 Lakini nyingine ikaanguka juu ya udongo ulio bora, nayo, ikamea na kuongezeka, ikaanza kutoa matunda, nayo ilikuwa ikizaa mara thelathini, na sitini na mia.” 9 Kwa hiyo akaongeza neno hili: “Acheni yeye aliye na masikio ya kusikiliza asikilize.”
10 Basi alipopata kuwa peke yake, wale waliomzunguka pamoja na wale kumi na wawili wakaanza kumuuliza juu ya vile vielezi. 11 Naye akaanza kuwaambia: “Kwenu ile siri takatifu ya ufalme wa Mungu imepewa, lakini kwa wale walio nje mambo yote yatukia kwa vielezi, 12 ili, ingawa wanatazama, wapate kutazama na bado wasione, na, ingawa wanasikia, wapate kusikia na bado wasipate maana yake, wala wasirudi kamwe na kupewa msamaha.” 13 Zaidi, akawaambia: “Hamjui kielezi hicho, na kwa hiyo mtaelewaje vielezi vingine vyote?
14 “Mpanzi hupanda lile neno. 15 Basi, hawa, ndio wale walio kando ya barabara ambapo lile neno limepandwa, lakini mara tu wakiisha kuwa wamesikia hilo Shetani huja na kuliondoa neno lililopandwa ndani yao. 16 Na hivyohivyo hawa ndio wale waliopandwa juu ya mahali penye miamba-miamba: mara tu wakiisha kuwa wamelisikia neno, walipokea kwa shangwe. 17 Lakini hawana mzizi ndani yao wenyewe, bali wao huendelea kuwako kwa wakati fulani; kisha mara tu dhiki au mnyanyaso utokeapo kwa sababu ya lile neno, wao hukwazika. 18 Na bado kuna wengine wanaopandwa katikati ya miiba; hawa ndio ambao wamelisikia neno, 19 lakini mahangaiko ya mfumo huu wa mambo na nguvu ya udanganyifu ya mali na tamaa za mambo yale mengine hufanya mipenyezo na kulisonga neno, nalo huwa lisilozaa matunda. 20 Mwishowe, wale waliopandwa juu ya udongo ulio bora ndio wale wasikilizao lile neno na kulipokea kwa mwelekeo mzuri na kuzaa matunda mara thelathini na sitini na mia.”
21 Naye akaendelea kuwaambia: “Taa hailetwi ili kuwekwa chini ya kikapu cha kupimia au chini ya kitanda, ndivyo? Huletwa ili kuwekwa juu ya kinara cha taa, sivyo? 22 Kwa maana hakuna jambo lililofichwa ila kwa kusudi la kufichuliwa; hakuna lililositiriwa kwa uangalifu ila kwa kusudi la kuja kwenye uwazi. 23 Yeyote aliye na masikio ya kusikiliza, acheni asikilize.”
24 Zaidi akawaambia: “Kazieni uangalifu yale ambayo mnasikia. Kwa kipimo kile mnachopimia, nyinyi mtapimiwa hicho, ndiyo, mtaongezewa zaidi. 25 Kwa maana yeye aliye na kitu atapewa zaidi; lakini yeye asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitaondolewa mbali kutoka kwake.”
26 Kwa hiyo akaendelea kusema: “Katika njia hii ufalme wa Mungu ni kama vile wakati mtu atupapo mbegu juu ya ardhi, 27 naye hulala usingizi wakati wa usiku na huamka wakati wa mchana, na ile mbegu huota na hukua kuwa ndefu, asijue ni jinsi gani hasa. 28 Ardhi hujizalia yenyewe matunda hatua kwa hatua, kwanza jani la nyasi, kisha suke la bua, mwishowe punje iliyo kamili katika suke. 29 Lakini mara tu matunda yaruhusupo, yeye hutia kwa nguvu mundu, kwa sababu wakati wa mavuno umekuja.”
30 Naye akaendelea kusema: “Tutaufananisha ufalme wa Mungu na nini, au tutauweka katika kielezi gani? 31 Kama punje ya haradali, ambayo ilipopandwa katika ardhi ilikuwa ndiyo mbegu ndogo zaidi sana kati ya zote ambazo zipo juu ya dunia— 32 lakini wakati ambapo imepandwa, humea na kuwa kubwa zaidi kuliko mboga nyingine zote na hutokeza matawi makubwa, hivi kwamba ndege wa mbinguni waweza kupata makao chini ya kivuli chayo.”
33 Kwa hiyo kwa vielezi vingi vya namna hiyo alikuwa akisema nao lile neno, kwa kadiri walivyoweza kusikiliza. 34 Kwa kweli, bila kielezi hakuwa akisema nao, lakini kwa faragha alikuwa akieleza mambo yote kwa wanafunzi wake.
35 Na siku hiyo, ilipokuwa jioni, akawaambia: “Acheni tuvuke hadi ukingo ule mwingine.” 36 Kwa hiyo, walipokuwa wamekwisha kuuruhusu umati kwenda, wakamchukua katika mashua, kama vile alivyokuwa, na kulikuwa na mashua nyinginezo pamoja naye. 37 Sasa kukatokea dhoruba kubwa ya upepo wenye nguvu nyingi, na mawimbi ukafuliza kupiga kwa nguvu ndani ya mashua, hivi kwamba mashua ikawa karibu kujawa na maji. 38 Lakini yeye alikuwa katika tezi, akiwa amelala usingizi juu ya mto. Kwa hiyo wakamwamsha na kumwambia: “Mwalimu, je, wewe hujali kwamba tuko karibu kuharibiwa?” 39 Ndipo akajiamsha mwenyewe akakemea upepo na kuiambia bahari: “Usu! Nyamaa!” Na upepo ukapunguka, kukawa shwari kubwa. 40 Kwa hiyo akawaambia: “Kwa nini mna moyo wa woga? Je, bado hamjawa na imani yoyote?” 41 Lakini wakahisi hofu isiyo ya kawaida, nao wakawa wakiambiana: “Kwa kweli huyu ni nani, kwa sababu hata upepo na bahari humtii?”