Marko
5 Basi, wakafika upande ule mwingine wa bahari kuingia katika wilaya ya Wagerasene. 2 Na mara baada ya yeye kutoka katika mashua mtu mmoja aliye chini ya nguvu ya roho asiye safi akakutana naye kutoka kati ya makaburi ya ukumbusho. 3 Yeye alikuwa na kikao chake miongoni mwa makaburi; na kufikia wakati huo hakuna kabisa mtu aliyeweza kumfunga hata kwa mnyororo, 4 kwa sababu nyakati nyingi alikuwa amefungwa kwa pingu na minyororo, lakini ile minyororo ilikatwa-katwa naye na zile pingu zilivunjwa-vunjwa kabisa; na hakuna mtu aliyekuwa na nguvu ya kumtiisha. 5 Na kwa kuendelea, usiku na mchana alikuwa akipaaza kilio makaburini na milimani na kujikatakata kwa mawe. 6 Lakini alipoona Yesu mara hiyo kutoka mbali akakimbia akamsujudia, 7 na, alipokuwa amepaaza kilio kwa sauti kubwa, akasema: “Mimi nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu Aliye Juu Zaidi Sana? Nakuweka chini ya kiapo kwa Mungu usinitese-tese.” 8 Kwa maana alikuwa amekuwa akimwambia: “Mtoke mtu huyo, wewe roho asiye safi.” 9 Lakini Yesu akaanza kumuuliza: “Jina lako nani?” Naye akamwambia: “Jina langu ni Lejioni, kwa sababu tuko wengi.” 10 Naye akamsihi sana mara nyingi asiwatoe hao roho nje ya ile nchi.
11 Basi kundi kubwa la nguruwe lilikuwapo penye mlima likilisha. 12 Kwa hiyo wakamsihi sana, wakisema: “Ututume tuingie katika wale nguruwe, ili tupate kuingia ndani yao.” 13 Naye akawaruhusu. Ndipo wale roho wasio safi wakatoka na kuingia katika wale nguruwe; na lile kundi likatimua mbio kali juu ya genge kuingia katika bahari, wakiwa karibu elfu mbili, nao wakafa maji mmoja baada ya mwingine katika bahari. 14 Lakini wachungaji wa hao nguruwe wakakimbia wakaripoti hilo katika jiji na mashambani; na watu wakaja kuona ni nini kilichokuwa kimetukia. 15 Kwa hiyo wakamjia Yesu, nao wakamwona yule mtu aliyepagawa na roho waovu akiwa ameketi amevishwa na akiwa na akili yake timamu, mtu yule aliyekuwa amekuwa na lile lejioni; nao wakawa wenye hofu. 16 Pia, wale waliokuwa wameona hilo wakawasimulia wao jinsi hilo lilivyokuwa limetukia kwa huyo mtu aliyepagawa na roho waovu na juu ya wale nguruwe. 17 Na kwa hiyo wakaanza kumsihi sana aende zake kutoka wilaya zao.
18 Basi alipokuwa akipanda mashua, yule mtu aliyekuwa amepagawa na roho waovu akaanza kumsihi sana ili apate kuendelea kuwa pamoja naye. 19 Hata hivyo, hakumwacha afanye hivyo, bali alimwambia: “Nenda nyumbani kwa jamaa zako, ukaripoti kwao mambo yote ambayo Yehova amekufanyia na rehema aliyokuwa nayo juu yako.” 20 Naye akaenda zake akaanza kupiga mbiu katika Dekapolisi kuhusu mambo yote ambayo Yesu alimfanyia, na watu wote wakaanza kustaajabu.
21 Baada ya Yesu kuvuka tena katika mashua na kurudi hadi ule ukingo wa upande wa pili umati mkubwa ukakusanyika pamoja kwake; naye alikuwa kando ya bahari. 22 Sasa mmoja wa maofisa-wasimamizi wa sinagogi, Yairo kwa jina, akaja na, alipomwona mara hiyo, akaanguka miguuni pake 23 akamsihi sana mara nyingi, akisema: “Binti yangu mdogo yuko katika hali mahututi. Uje tafadhali uweke mikono yako juu yake ili apate kupona na kuishi.” 24 Ndipo akaenda zake pamoja naye. Na umati mkubwa ulikuwa ukimfuata na kumsonga.
25 Basi kulikuwa na mwanamke aliyeshikwa na mtiririko wa damu miaka kumi na miwili, 26 naye alikuwa ameteswa sana na matabibu wengi na alikuwa ametumia mali zake zote na hakuwa amenufaishwa bali, badala ya hivyo, akawa na hali mbaya zaidi. 27 Aliposikia mambo juu ya Yesu, akaja nyuma katika ule umati akagusa vazi lake la nje; 28 kwa maana alifuliza kusema: “Nikigusa tu mavazi yake ya nje nitapona.” 29 Na mara chemchemi yake ya damu ikakauka kabisa, naye akahisi mwilini mwake kwamba alikuwa ameponywa ule ugonjwa wenye kutia kihoro.
30 Mara, pia, Yesu akatambua ndani yake mwenyewe kwamba nguvu ilikuwa imemtoka, naye akageuka huku na huku katika ule umati na kuanza kusema: ‘Ni nani aliyegusa mavazi yangu ya nje?’ 31 Lakini wanafunzi wake wakaanza kumwambia: “Waona umati unavyokusonga, nawe wasema, ‘Ni nani aliyenigusa mimi?’” 32 Hata hivyo, alikuwa akitazama huku na huku ili amwone mwanamke aliyekuwa amefanya hilo. 33 Lakini huyo mwanamke, akiwa mwenye kuogopa na akitetemeka, akijua lililokuwa limetukia kwake, akaja akaanguka chini mbele yake akamwambia kweli yote. 34 Yesu akamwambia: “Binti, imani yako imekufanya upone. Nenda kwa amani, na uwe katika afya njema kutokana na ugonjwa wako wa kutia kihoro.”
35 Alipokuwa bado akisema, watu fulani kutoka nyumbani mwa ofisa-msimamizi wa sinagogi wakaja na kusema: “Binti yako alikufa! Kwa nini kumsumbua mwalimu tena?” 36 Lakini Yesu, akitukia kusikia neno lililokuwa likisemwa, akamwambia ofisa-msimamizi wa sinagogi: “Usiwe na hofu, dhihirisha tu imani.” 37 Basi hakuacha yeyote afuatane naye ila Petro na Yakobo na Yohana ndugu ya Yakobo.
38 Kwa hiyo wakaja kwenye nyumba ya ofisa-msimamizi wa sinagogi, naye akaona ule mvurugo wenye makelele na wale wenye kutoa machozi na kutokeza sauti nyingi za kuomboleza, 39 na, baada ya kuingia, akawaambia: “Kwa nini mnasababisha mvurugo wenye makelele na kutoa machozi? Mtoto mchanga hakufa, bali analala usingizi.” 40 Ndipo wakaanza kumcheka kwa dharau. Lakini, akiisha kuwatoa nje wote, akachukua baba na mama ya huyo mtoto mchanga na walio pamoja naye, naye akaingia mahali alimokuwa huyo mtoto mchanga. 41 Na, akishika mkono wa huyo mtoto mchanga, akamwambia:“Talitha kumi,” ambalo, litafsiriwapo, humaanisha: “Mwanamwali, nakuambia, Inuka!” 42 Na mara yule mwanamwali akainuka akaanza kutembea, kwa maana alikuwa mwenye umri wa miaka kumi na miwili. Na mara moja wakapigwa na bumbuazi ya upeo wa shangwe kubwa. 43 Lakini yeye akawaagiza tena na tena wasiache yeyote ajue juu ya hilo, naye akasema kwamba mtoto apewe kitu ale.