Marko
8 Siku hizo, kulipokuwa tena na umati mkubwa nao haukuwa na kitu cha kula, yeye akawaita wanafunzi na kuwaambia: 2 “Nahisi sikitiko kwa ajili ya umati, kwa sababu tayari ni siku tatu ambazo umekaa karibu nami nao hauna kitu cha kula; 3 nami nikiuagiza uende zao nyumbani kwao ukiwa umefunga, utazimia barabarani. Kwa kweli, baadhi yao ni wa kutoka mbali sana.” 4 Lakini wanafunzi wake wakamjibu: “Ni kutoka wapi yeyote hapa katika mahali pa upweke ataweza kushibisha watu hawa kwa mikate?” 5 Na bado akaendelea kuwauliza: “Ni mikate mingapi mliyo nayo?” Wakasema: “Saba.” 6 Naye akauagiza umati uegame juu ya ardhi, naye akachukua ile mikate saba, akashukuru, akaimega, na kuanza kuwapa wanafunzi wake waandae, nao wakaiandaa kwa umati. 7 Walikuwa pia na samaki wadogo wachache; na, akiisha kubariki hao, akawaambia waandae hao pia. 8 Basi wakala na kushiba, nao wakaokota ziada ya vipande vidogo, makapu saba ya chakula yaliyojaa. 9 Na bado kulikuwa na karibu wanaume elfu nne. Mwishowe akawaacha waende zao.
10 Na mara akaipanda mashua pamoja na wanafunzi wake akaja kuingia katika zile sehemu za Dalmanutha. 11 Hapa Mafarisayo wakatokea na kuanza kubishana naye, wakitafuta sana kutoka kwake ishara kutoka mbinguni, ili kumtia kwenye jaribu. 12 Kwa hiyo akapiga kite sana rohoni mwake, na kusema: “Kwa nini kizazi hiki chatafuta sana ishara? Kwa kweli mimi nasema, hakuna ishara itakayopewa kwa kizazi hiki.” 13 Ndipo akawaacha, akapanda ndani tena, na kwenda zake hadi ukingo wa pili.
14 Ikawa kwamba walisahau kuichukua mikate, na hawakuwa na kitu katika mashua ila mkate mmoja. 15 Naye akaanza kuwaagiza waziwazi na kusema: “Fulizeni kufungua macho yenu, jihadharini na chachu ya Mafarisayo na chachu ya Herode.” 16 Kwa hiyo wakaanza kujadiliana juu ya jambo la kwamba hawakuwa na mikate yoyote. 17 Akijua hilo, akawaambia: “Kwa nini mwajadiliana kwa sababu hamna mikate? Je, hamjafahamu bado na kupata maana? Je, mnakuwa na mioyo yenu ikiwa mizito isiweze kuelewa? 18 ‘Ijapokuwa mna macho, hamwoni; na ijapokuwa mna masikio, hamsikii?’ Na hamkumbuki, 19 wakati nilipoimega ile mikate mitano kwa ajili ya wale wanaume elfu tano, ni vikapu vingapi vyenye kujaa vipande vidogo mlivyookota?” Wakamwambia: “Kumi na viwili.” 20 “Nilipoimega ile saba kwa ajili ya wale wanaume elfu nne, ni makapu mangapi ya chakula yenye kujaa vipande vidogo mliyookota?” Nao wakamwambia: “Saba.” 21 Ndipo akawaambia: “Je, bado hamjapata maana?”
22 Sasa wakafika Bethsaida. Hapa watu wakamletea mtu aliye kipofu, nao wakamsihi sana amguse huyo. 23 Naye akimshika mkono yule mtu aliye kipofu, akamleta nje ya kijiji, na, akiisha kutema mate juu ya macho yake, Yesu akaweka mikono juu yake na kuanza kumuuliza: “Je, unaona kitu chochote?” 24 Na yule mtu akatazama juu na kuanza kusema: “Naona watu, kwa sababu naangalia ionekanayo kama miti, lakini inatembea huku na huku.” 25 Kisha akaweka mikono yake tena juu ya macho ya huyo mtu, na huyo mtu akaona waziwazi, naye akarudishiwa kuona, naye alikuwa akiona kila kitu dhahiri. 26 Kwa hiyo akamwagiza aende zake nyumbani, akisema: “Lakini usiingie katika kijiji.”
27 Yesu na wanafunzi wake sasa wakaondoka kwenda vijiji vya Kaisaria Filipi, na njiani akaanza kuuliza wanafunzi wake, akisema: “Watu wanasema kwamba mimi ni nani?” 28 Wakamwambia: “Yohana Mbatizaji, na wengine, Eliya, bado wengine, Mmoja wa manabii.” 29 Naye akawatokezea swali: “Ingawa hivyo, nyinyi mwasema mimi ni nani?” Kwa kujibu Petro akamwambia: “Wewe ndiwe Kristo.” 30 Ndipo akawaagiza kwa mkazo wasimwambie yeyote juu yake. 31 Pia, akaanza kuwafundisha kwamba Mwana wa binadamu lazima apatwe na mateso mengi na kukataliwa na wanaume wazee na makuhani wakuu na waandishi na kuuawa, na kufufuliwa siku tatu baadaye. 32 Kwa kweli, kwa usemi wa waziwazi alikuwa akitoa taarifa hiyo. Lakini Petro akamchukua kando na kuanza kumkemea. 33 Akageuka, akatazama wanafunzi wake akamkemea Petro, na kusema: “Nenda nyuma yangu, Shetani, kwa sababu wewe wafikiri, si fikira za Mungu, bali yale ya wanadamu.”
34 Basi akaita umati kwake pamoja na wanafunzi wake na kuwaambia: “Ikiwa yeyote ataka kunifuata, na ajikane mwenyewe na kuchukua mti wake wa mateso na kunifuata kwa kuendelea. 35 Kwa maana yeyote yule atakaye kuokoa nafsi yake ataipoteza; lakini yeyote yule aipotezaye nafsi yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya habari njema ataiokoa. 36 Kwa kweli, ina manufaa gani kwa mtu kupata faida ya kuwa na ulimwengu wote na kupoteza nafsi yake? 37 Kwa kweli, ni nini ambacho mtu angetoa katika kubadilishana kwa ajili ya nafsi yake? 38 Kwa maana awaye yote yule mwenye kuaibika juu yangu na maneno yangu katika kizazi hiki chenye uzinzi na chenye dhambi, Mwana wa binadamu ataaibika juu yake pia awasilipo katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu.”