Marko
7 Sasa Mafarisayo na baadhi ya waandishi waliokuwa wamekuja kutoka Yerusalemu wakakusanyika kumzunguka. 2 Nao walipoona baadhi ya wanafunzi wake wakila mlo wao kwa mikono iliyotiwa unajisi, yaani, bila kuoshwa— 3 kwa maana Mafarisayo na Wayahudi wote hawali isipokuwa waoshe mikono yao hadi kwenye kiko, wakishika sana mapokeo ya watu wa nyakati za hapo zamani, 4 na, warudipo kutoka sokoni, hawali isipokuwa wajisafishe wenyewe kwa kunyunyiza; na kuna mapokeo mengine mengi ambayo wamepokea ili kushika sana, mabatizo ya vikombe na mitungi na vyombo vya shaba;— 5 Kwa hiyo Mafarisayo na waandishi hawa wakamuuliza: “Kwa nini wanafunzi wako hawajiendeshi wenyewe kulingana na mapokeo ya watu wa nyakati za hapo zamani, bali hula mlo wao kwa mikono iliyotiwa unajisi?” 6 Yeye akawaambia: “Isaya kwa kufaa alitoa unabii juu yenu wanafiki, kama vile imeandikwa, ‘Watu hawa huniheshimu mimi kwa midomo yao, bali mioyo yao imeondolewa mbali nami. 7 Ni bure kwamba wao hufuliza kuniabudu, kwa sababu wao hufundisha amri za watu kuwa mafundisho.’ 8 Mkiwa mnaiacha amri ya Mungu, mwashika sana mapokeo ya wanadamu.”
9 Zaidi, yeye akaendelea kuwaambia: “Kwa ustadi mwaweka kando amri ya Mungu kusudi mhifadhi mapokeo yenu. 10 Kwa kielelezo, Musa alisema, ‘Heshimu baba yako na mama yako,’ na, ‘Acheni yeye ambaye hutukana baba au mama na afikie mwisho katika kifo.’ 11 Lakini nyinyi watu mwasema, ‘Ikiwa mtu amwambia baba yake au mama yake: “Chochote kile nilicho nacho ambacho kwacho waweza kupata manufaa kutoka kwangu ni korbani, (yaani, zawadi iliyowekwa wakfu kwa Mungu,)”’— 12 Nyinyi watu hammwachi yeye tena afanye hata jambo moja kwa ajili ya baba yake au mama yake, 13 na hivyo mwalibatilisha neno la Mungu kwa mapokeo yenu ambayo nyinyi mlikabidhiwa. Na mambo mengi yafananayo na hilo nyinyi huyafanya.” 14 Kwa hiyo, akiuita tena umati kwake, akaendelea kuuambia: “Nisikilizeni, nyinyi nyote, na ipateni maana. 15 Hakuna chochote kutoka nje ya mtu kipitacho ndani yake kiwezacho kumtia unajisi; bali mambo yatokayo katika mtu ndiyo mambo yamtiayo mtu unajisi.” 16 ——
17 Basi alipokuwa ameingia katika nyumba akiwa mbali na umati, wanafunzi wake wakaanza kumuuliza habari ya kile kielezi. 18 Kwa hiyo yeye akawaambia: “Nyinyi pia hamna ufahamivu kama wao? Je, hamjui kwamba hakuna chochote kutoka nje kipitacho ndani ya mtu kiwezacho kumtia unajisi, 19 kwa kuwa hicho hupita, si ndani ya moyo wake, bali kuingia katika matumbo yake, nacho hupita nje kuingia katika mtaro wa takataka?” Kwa njia hiyo akatangaza vyakula vyote kuwa safi. 20 Zaidi, akasema: “Kile ambacho hutoka ndani ya mtu ndicho humtia mtu unajisi; 21 kwa maana kutoka ndani, kutoka katika moyo wa watu, hutoka mawazowazo mabaya: uasherati, wizi, mauaji-kimakusudi, 22 uzinzi, kutamani, matendo ya uovu, udanganyi, mwenendo mlegevu, jicho lenye husuda, kufuru, kiburi, ukosefu wa akili. 23 Mambo maovu yote hayo hutoka ndani na humtia mtu unajisi.”
24 Kutoka huko akainuka akaenda kuingia katika mikoa ya Tiro na Sidoni. Naye akaingia katika nyumba na hakutaka yeyote apate kujua hilo. Na bado hangeweza kuponyoka utambuzi; 25 lakini mara hiyo mwanamke ambaye binti yake mdogo alikuwa na roho asiye safi alisikia habari zake akaja na kujiangusha mwenyewe chini miguuni pake. 26 Yule mwanamke alikuwa mtoka-Ugiriki, Msiria-Mfoinike kwa taifa; naye alifuliza kumwomba afukuze roho mwovu kutoka katika binti yake. 27 Lakini Yesu akaanza kumwambia: “Kwanza acha watoto washibe, kwa maana si sawa kuuchukua mkate wa watoto na kuutupa kwa mbwa wadogo.” 28 Hata hivyo, kwa kujibu, huyo mwanamke akamwambia: “Ndiyo, bwana, na bado hao mbwa wadogo chini ya meza hula baadhi ya makombo ya watoto wadogo.” 29 Ndipo Yesu akamwambia: “Kwa sababu ya kusema hayo, nenda; yule roho mwovu amemtoka binti yako.” 30 Kwa hiyo akatoka kwenda zake hadi nyumbani kwake na kukuta huyo mtoto mchanga amelazwa juu ya kitanda na roho mwovu amemtoka.
31 Basi alipokuwa akirudi kutoka katika mikoa ya Tiro akaenda kupitia Sidoni hadi bahari ya Galilaya akipanda kupita katikati ya mikoa ya Dekapolisi. 32 Hapo wakamletea mtu kiziwi na aliye na kizuizi cha usemi, nao wakamsihi kwa bidii aweke mkono wake juu yake. 33 Naye akamchukua kutoka katika umati kwa faragha akaweka vidole vyake ndani ya masikio ya yule mtu na, baada ya kutema mate, akamgusa ulimi wake. 34 Na akitazama juu mbinguni akatweta kwa nguvu na kumwambia: “Efatha,” yaani, “Funguka.” 35 Basi, nguvu zake za kusikia zikafunguliwa, na kile kizuizi cha ulimi wake kikalegezwa, naye akaanza kusema kama kawaida. 36 Ndipo akawaamuru wasimwambie yeyote; lakini kwa kadiri alivyozidi kuwa akiwaamuru, kwa kadiri hiyo ndivyo walivyozidi kuwa wakipiga mbiu juu ya hilo. 37 Kwa kweli, walikuwa wakistaajabishwa kwa njia izidiyo zaidi sana iliyo ya kawaida nao wakasema: “Amefanya mambo yote vema. Afanya hata viziwi wasikie na wasiosema waseme.”