Marko
9 Zaidi ya hilo, akaendelea kuwaambia: “Kwa kweli nawaambia nyinyi, Kuna baadhi ya wale ambao wamesimama hapa ambao hawataonja kifo hata kidogo mpaka kwanza wauone ufalme wa Mungu ukiwa tayari umekuja katika nguvu.” 2 Basi siku sita baadaye Yesu alichukua pamoja naye Petro na Yakobo na Yohana, akawaleta juu katika mlima ulioinuka sana wakiwa peke yao. Naye akageuzwa umbo mbele yao, 3 na mavazi yake ya nje yakawa yenye kumetameta, yakiwa meupe zaidi kuliko vile msafisha-nguo yeyote duniani angeweza kuyafanya meupe. 4 Pia, Eliya pamoja na Musa wakaonekana kwao, nao walikuwa wakiongea na Yesu. 5 Na kwa kujibu Petro akamwambia Yesu: “Rabi, ni vizuri kwetu kuwa hapa, kwa hiyo na tusimamishe mahema matatu, moja lako na moja la Musa na moja la Eliya.” 6 Kwa kweli, yeye hakujua ni nini alilopaswa kujibu, kwa maana walipata kuwa wenye hofu sana. 7 Na wingu likafanyika, likiwafunika kivuli, na sauti ikaja kutoka katika lile wingu: “Huyu ni Mwana wangu, mpendwa; msikilizeni yeye.” 8 Hata hivyo, kwa ghafula wakatazama huku na huku na hawakuona yeyote pamoja nao tena kamwe, ila Yesu peke yake.
9 Walipokuwa wakiteremka kutoka kwenye ule mlima, yeye aliwaagiza waziwazi kutosimulia yeyote kile walichoona, mpaka baada ya Mwana wa binadamu awe amefufuliwa kutoka kwa wafu. 10 Nao wakashika lile neno moyoni, lakini wakazungumza miongoni mwao wenyewe kile ambacho huku kufufuliwa kutoka katika wafu kulimaanisha. 11 Nao wakaanza kumuuliza, wakisema: “Kwa nini waandishi husema kwamba kwanza ni lazima Eliya aje?” 12 Akawaambia: “Eliya aja kwanza na kurudisha mambo yote; lakini ni jinsi gani kwamba imeandikwa kwa habari ya Mwana wa binadamu kwamba lazima apatwe na mateso mengi na kutendwa kama asiye wa maana? 13 Lakini mimi nawaambia nyinyi, kwa kweli Eliya amekuja, nao walimfanya mambo mengi kama walivyotaka, kama vile imeandikwa kwa habari yake.”
14 Sasa, walipokuja kuelekea wale wanafunzi wengine, wakaona umati mkubwa umewazunguka huku na huku na waandishi wakibishana nao. 15 Lakini mara tu umati wote ulipomwona ukafadhaika, na, ukimkimbilia, ukaanza kumsalimu. 16 Naye akawauliza: “Mnabishania nini nao?” 17 Na mmoja wa ule umati akamjibu: “Mwalimu, nilileta mwana wangu kwako kwa sababu ana roho asiyesema; 18 na popote pale amkamatapo humbwaga kwenye ardhi, naye hutoa povu na kusaga meno yake na kupoteza nguvu zake. Nami niliwaambia wanafunzi wako wamfukuze, lakini hawakuweza.” 19 Kwa kujibu, akawaambia: “Ewe kizazi kisicho na imani, ni kwa muda gani lazima niendelee kuwa pamoja nanyi? Ni kwa muda gani lazima nichukuliane nanyi? Mleteni kwangu.” 20 Kwa hiyo wakamleta kwake. Lakini kwa kumwona tu, mara moja yule roho akamtia yule mtoto katika mifurukuto, na baada ya kuanguka juu ya ardhi akafuliza kugaagaa huku na huku, akitoa povu. 21 Naye akauliza baba yake: “Ni kwa muda gani hilo limekuwa likitukia kwake?” Akasema: “Tangu utoto na kuendelea; 22 na mara nyingi akawa akimtupa-tupa ndani ya moto na ndani ya maji ili kumwangamiza. Lakini ikiwa waweza kufanya jambo lolote, utusikitikie na kutusaidia.” 23 Yesu akamwambia: “Usemi huo, ‘Ikiwa waweza’! Ah, mambo yote yaweza kuwa kwa mtu ikiwa ana imani.” 24 Mara akipaaza kilio, baba ya yule mtoto mchanga akawa akisema: “Nina imani! Unisaidie ambapo nahitaji imani!”
25 Yesu, sasa akiona kwamba umati ulikuwa ukikimbia pamoja kuwasogelea, akakemea yule roho asiye safi, akimwambia: “Wewe roho usiyesema na uliye kiziwi, nakuagiza, toka ndani yake wala usimwingie tena.” 26 Na baada ya kupaaza kilio na kupatwa na mifurukuto mingi akatoka; naye mtoto akawa ni kama amekufa, hivi kwamba idadi kubwa zaidi kati yao walikuwa wakisema: “Amekufa!” 27 Lakini Yesu akamshika mkono na kumwinua, naye akainuka. 28 Kwa hiyo baada ya kuingia katika nyumba wanafunzi wake wakaanza kumuuliza kwa faragha: “Kwa nini sisi hatukuweza kumfukuza?” 29 Naye akawaambia: “Aina hii haiwezi kutoka kwa chochote ila kwa sala.”
30 Kutoka huko wakaondoka na kushika njia yao kwenda kupitia Galilaya, lakini hakutaka yeyote apate kujua hilo. 31 Kwa maana alikuwa akifundisha wanafunzi wake na kuwaambia: “Mwana wa binadamu atapaswa kukabidhiwa mikononi mwa watu, nao watamuua, lakini, ijapokuwa atauawa, yeye atafufuliwa siku tatu baadaye.” 32 Hata hivyo, walikuwa hawaelewi huo usemi, nao waliogopa kumuuliza swali.
33 Nao wakaja kuingia Kapernaumu. Sasa alipokuwa ndani ya nyumba akawatokezea swali: “Mlikuwa mkibishania nini barabarani?” 34 Wakafuliza kukaa kimya, kwa maana barabarani walikuwa wamebishania miongoni mwao wenyewe nani aliye mkubwa zaidi. 35 Kwa hiyo akaketi na kuwaita wale kumi na wawili na kuwaambia: “Ikiwa yeyote ataka kuwa wa kwanza, lazima awe wa mwisho kati ya wote na mhudumu wa wote.” 36 Naye akachukua mtoto mchanga, akamsimamisha katikati yao akamkumbatia na kuwaambia: 37 “Yeyote yule apokeaye mmoja wa watoto wachanga wa namna hii juu ya msingi wa jina langu, anipokea mimi; na yeyote yule anipokeaye mimi, apokea, si mimi tu, bali pia yeye aliyenituma mimi.”
38 Yohana akamwambia: “Mwalimu, tuliona mtu fulani akitoa roho waovu kwa utumizi wa jina lako nasi tukajaribu kumzuia, kwa sababu yeye hakuwa akiandamana nasi.” 39 Lakini Yesu akasema: “Msijaribu kumzuia, kwa maana hakuna yeyote atakayefanya kazi zenye nguvu juu ya msingi wa jina langu atakayeweza kwa upesi kunitukana mimi; 40 kwa maana yeye asiye dhidi yetu yuko upande wetu. 41 Kwa maana yeyote yule awapaye nyinyi kikombe cha maji ya kunywa kwa sababu ya kwamba nyinyi ni wa Kristo, kwa kweli nawaambia nyinyi, hatapoteza kwa vyovyote thawabu yake. 42 Lakini yeyote yule akwazaye mmoja wa wadogo hawa waaminio, ingekuwa bora zaidi kwake ikiwa jiwe la kusagia kama lile lizungushwalo na punda lingewekwa kuzunguka shingo yake naye kwa kweli atupwe ndani ya bahari.
43 “Na ikitukia wakati wowote mkono wako wakufanya ukwazike, ukatilie mbali; ni bora zaidi kwako kuingia katika uhai ukiwa umeharibika viungo kuliko kwenda zako ukiwa na mikono miwili kuingia katika Gehena, katika moto usioweza kuzimwa. 44 —— 45 Na ikiwa mguu wako wakufanya ukwazike, ukatilie mbali; ni bora zaidi kwako kuingia katika uhai ukiwa kilema kuliko kutupwa ukiwa na miguu miwili kuingia katika Gehena. 46 —— 47 Na ikiwa jicho lako lakufanya ukwazike, litupilie mbali; ni bora zaidi kwako kuingia katika ufalme wa Mungu ukiwa na jicho moja kuliko kutupwa ndani ya Gehena ukiwa na macho mawili, 48 mahali ambapo funza wao hafi na ule moto hauzimwi.
49 “Kwa maana kila mtu lazima atiwe chumvi kwa moto. 50 Chumvi ni bora; lakini ikitukia wakati wowote kwamba chumvi yapoteza nguvu yayo, nyinyi mtakoleza hiyo yenyewe na nini? Iweni na chumvi ndani yenu wenyewe, na dumisheni amani nyinyi kwa nyinyi.”