Marko
10 Kutoka hapo akainuka na kuja kwenye mipaka ya Yudea na ng’ambo ya Yordani, na tena umati ukaja pamoja kwake, na kama alivyokuwa na desturi ya kufanya akaanza tena kuufundisha. 2 Mafarisayo sasa wakamkaribia na, ili kumtia kwenye jaribu, wakaanza kumuuliza kama iliruhusika kisheria mwanamume kumtaliki mke. 3 Kwa kujibu akawaambia: “Musa aliwaamuru nyinyi nini?” 4 Wakasema: “Musa aliruhusu kuandika cheti cha kufukuza na kutaliki mke.” 5 Lakini Yesu akawaambia: “Kwa kufikiria ugumu wenu wa moyo aliwaandikia nyinyi amri hiyo. 6 Hata hivyo, tangu mwanzo wa kuumba ‘Yeye aliwafanya wa kiume na wa kike. 7 Kwa sababu hiyo mtu ataacha baba yake na mama yake, 8 na hao wawili watakuwa mwili mmoja’; hivi kwamba wao si wawili tena, bali mwili mmoja. 9 Kwa hiyo kile ambacho Mungu alifunga nira pamoja mtu yeyote na asikitenganishe.” 10 Alipokuwa tena katika nyumba wanafunzi wakaanza kumuuliza kuhusu hilo. 11 Naye akawaambia: “Yeyote yule atalikiye mke wake na kuoa mwingine afanya uzinzi dhidi ya mke, 12 na ikitukia wakati wowote mwanamke, baada ya kutaliki mume wake, aolewa na mwingine, yeye afanya uzinzi.”
13 Sasa watu wakaanza kumletea watoto wachanga ili awaguse; lakini wanafunzi wakawakemea. 14 Kwa kuona hili Yesu akaghadhibika na kuwaambia: “Waacheni watoto wachanga waje kwangu; msijaribu kuwakomesha, kwa maana ufalme wa Mungu ni wa walio kama hao. 15 Kwa kweli nawaambia nyinyi, Yeyote yule asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mchanga hataingia kwa vyovyote ndani ya huo.” 16 Naye akachukua watoto akawakumbatia na kuanza kuwabariki, akiweka mikono yake juu yao.
17 Naye alipokuwa akitoka ashike njia yake aende, mtu fulani akamkimbilia na kuanguka akipiga magoti mbele yake na kumtokezea swali: “Mwalimu Mwema, lazima nifanye nini ili kurithi uhai udumuo milele?” 18 Yesu akamwambia: “Kwa nini waniita mwema? Hakuna mtu aliye mwema, ila mmoja, Mungu. 19 Wewe wazijua amri, ‘Usiue kimakusudi, Usifanye uzinzi, Usiibe, Usitoe ushahidi usio wa kweli, Usipunje, Heshimu baba yako na mama yako.’” 20 Mtu huyo akamwambia: “Mwalimu, mambo yote hayo nimeyashika tangu ujana wangu na kuendelea.” 21 Yesu akamtazama akahisi upendo kwa ajili yake na kumwambia: “Jambo moja limekosekana kwako: Nenda, uuze vitu ulivyo navyo uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni, na uje uwe mfuasi wangu.” 22 Lakini yeye akahuzunika kwa usemi huo na kwenda zake akiwa ametiwa kihoro, kwa maana alikuwa na miliki nyingi.
23 Baada ya kutazama huku na huku Yesu akawaambia wanafunzi wake: “Jinsi litakavyokuwa jambo gumu kwa wale wenye fedha kuingia katika ufalme wa Mungu!” 24 Lakini wanafunzi wakashangaa kwa sababu ya maneno yake. Kwa kujibu Yesu akawaambia tena: “Watoto, jinsi lilivyo jambo gumu kuingia katika ufalme wa Mungu! 25 Ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko kwa mtu tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.” 26 Wakawa wenye kustaajabu bado zaidi na kumwambia: “Ni nani ambaye, kwa kweli, aweza kuokolewa?” 27 Akiwatazama moja kwa moja Yesu akasema: “Kwa wanadamu haiwezekani, bali kwa Mungu sivyo, kwa maana mambo yote yawezekana kwa Mungu.” 28 Petro akaanza kumwambia: “Tazama! Sisi tuliacha vitu vyote na tumekuwa tukikufuata wewe.” 29 Yesu akasema: “Kwa kweli nawaambia nyinyi watu, Hakuna ambaye ameacha nyumba au akina ndugu au akina dada au mama au baba au watoto au mashamba kwa ajili yangu na kwa ajili ya habari njema 30 ambaye hatapata mara mia sasa katika kipindi hiki cha wakati, nyumba na akina ndugu na akina dada na akina mama na watoto na mashamba, pamoja na minyanyaso, na katika mfumo wa mambo unaokuja uhai udumuo milele. 31 Hata hivyo, wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na wa mwisho wawe wa kwanza.”
32 Sasa walikuwa wakisonga mbele barabarani kupanda kwenda Yerusalemu, na Yesu alikuwa akienda mbele yao, nao wakaona mshangao; lakini wale waliofuata wakaanza kuhofu. Mara nyingine tena akachukua wale kumi na wawili kando na kuanza kuwaambia mambo haya yaliyokusudiwa kumpata: 33 “Sisi hapa, tunasonga mbele kupanda kwenda Yerusalemu, na Mwana wa binadamu atakabidhiwa kwa makuhani wakuu, na waandishi, nao watamhukumu adhabu ya kifo na watamkabidhi kwa watu wa mataifa, 34 nao watamfanyia ucheshi na watamtemea mate na kumpiga mijeledi na kumuua, lakini siku tatu baadaye atafufuliwa.”
35 Na Yakobo na Yohana, wana wawili wa Zebedayo, wakachukua hatua kumwendea na kumwambia: “Mwalimu, twataka wewe utufanyie chochote kile tukuombacho.” 36 Yeye akawaambia: “Mwataka niwafanyie nini?” 37 Wakamwambia: “Uturuhusu kuketi, mmoja kwenye mkono wako wa kuume na mmoja kwenye mkono wako wa kushoto, katika utukufu wako.” 38 Lakini Yesu akawaambia: “Hamjui ni nini mnachoomba. Je, mwaweza kunywa kikombe ambacho ninakunywa, au kubatizwa kwa ubatizo ninaobatizwa?” 39 Wakamwambia: “Twaweza.” Ndipo Yesu akawaambia: “Kikombe ninachokunywa mtakunywa, na ubatizo ambao kwa huo ninabatizwa mtabatizwa. 40 Hata hivyo, huku kuketi kwenye mkono wangu wa kuume au kwenye mkono wangu wa kushoto si kwangu kutoa, bali ni kwa wale ambao kwa ajili yao kumetayarishiwa.”
41 Basi, wale wengine kumi waliposikia juu ya hilo, wakaanza kughadhibikia Yakobo na Yohana. 42 Lakini Yesu, baada ya kuwaita kwake, akawaambia: “Mwajua kwamba wale ambao huonekana kuwa wanatawala mataifa hupiga ubwana juu yao na watu wakubwa wao hutumia mamlaka juu yao. 43 Hivyo sivyo ilivyo miongoni mwenu; bali yeyote yule atakaye kuwa mkubwa miongoni mwenu lazima awe mhudumu wenu, 44 na yeyote yule atakaye kuwa wa kwanza miongoni mwenu lazima awe mtumwa wa wote. 45 Kwa maana hata Mwana wa binadamu alikuja, si kuhudumiwa, bali kuhudumu na kutoa nafsi yake kuwa fidia katika kubadilishana kwa ajili ya wengi.”
46 Nao wakaja kuingia Yeriko. Lakini yeye na wanafunzi wake na umati mkubwa walikuwa wakienda kutoka Yeriko, Bartimayo (mwana wa Timayo), kipofu aliye mwombaji, alikuwa ameketi kando ya barabara. 47 Aliposikia kwamba alikuwa ni Yesu Mnazareti, akaanza kupaaza sauti na kusema: “Mwana wa Daudi, Yesu, uwe na rehema juu yangu!” 48 Ndipo wengi wakaanza kumwambia kwa kusisitiza awe kimya; lakini ndivyo naye alivyofuliza kupaaza sana sauti zaidi na zaidi: “Mwana wa Daudi, uwe na rehema juu yangu!” 49 Kwa hiyo Yesu akasimama na kusema: “Mwiteni.” Nao wakamwita yule mtu aliye kipofu, wakimwambia: “Jipe moyo, inuka, anakuita.” 50 Akitupa vazi lake la nje, akaruka kusimama kwa miguu yake na kumwendea Yesu. 51 Na kwa kumjibu yeye Yesu akasema: “Wataka nikufanyie nini?” Yule mtu aliye kipofu akamwambia: “Raboni, acha nipate tena kuona.” 52 Na Yesu akamwambia: “Nenda, imani yako imekufanya upone.” Na mara akapata tena kuona, naye akaanza kumfuata barabarani.