Marko
11 Sasa walipokuwa wakikaribia kufika Yerusalemu, Bethfage na Bethania kwenye Mlima wa Mizeituni, akatuma wawili wa wanafunzi wake 2 na kuwaambia: “Nendeni mwingie katika kijiji kilicho karibu yenu, na mara tu mpitapo ndani yacho mtakuta mwana-punda amefungwa, ambaye hakuna yeyote wa wanadamu ameketi juu yake; mfungueni mmlete. 3 Na ikiwa yeyote awaambia nyinyi, ‘Kwa nini mnafanya hili?’ semeni, ‘Bwana amhitaji, na atamrudisha hapa mara moja.’” 4 Kwa hiyo wakaenda zao na kukuta mwana-punda amefungwa kwenye mlango, nje kwenye barabara ya kandokando, nao wakamfungua. 5 Lakini baadhi ya wale wenye kusimama hapo wakaanza kuwaambia: “Mnafanya nini kufungua huyo mwana-punda?” 6 Wakawaambia hao kama vile Yesu alivyokuwa amesema; nao wakawaacha waende.
7 Nao wakamletea Yesu huyo mwana-punda, nao wakaweka mavazi yao ya nje juu yake, naye akaketi juu yake. 8 Pia, wengi wakatandaza mavazi yao ya nje barabarani, lakini wengine wakakata matawi yenye majani kutoka mashambani. 9 Na wale waliokuwa wakienda mbele na wale waliokuwa wakifuata nyuma wakafuliza kupaaza kilio: “Okoa, twasihi! Mbarikiwa ni yeye ajaye katika jina la Yehova! 10 Wenye kubarikiwa ni ufalme unaokuja wa baba yetu Daudi! Okoa, twasihi, katika mahali palipo juu!” 11 Naye akaingia Yerusalemu, katika hekalu; naye akatazama huku na huku juu ya vitu vyote, na, kwa kuwa saa ilikuwa tayari imesonga, akatoka kwenda Bethania pamoja na wale kumi na wawili.
12 Siku iliyofuata, walipokuwa wamekuja kutoka Bethania, akawa mwenye njaa. 13 Na kwa umbali akaona mara hiyo mtini uliokuwa na majani, naye akaenda kuona kama labda angeweza kupata kitu fulani juu ya huo. Lakini, alipoujia, hakupata kitu ila majani, kwa maana hayakuwa majira ya tini. 14 Kwa hiyo, kwa kujibu, akauambia: “Acha mtu asile matunda kutoka kwako tena kamwe milele.” Na wanafunzi wake walikuwa wakisikiliza.
15 Sasa wakaja Yerusalemu. Huko akaingia katika hekalu akaanza kufukuza nje wale waliokuwa wakiuza na kununua katika hekalu, naye akazipindua meza za wabadili-fedha na mabenchi ya hao waliokuwa wakiuza njiwa; 16 naye alikuwa haachi yeyote kuchukua chombo kupitia hekalu, 17 lakini akafuliza kufundisha na kusema: “Je, haikuandikwa, ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa ajili ya mataifa yote’? Lakini nyinyi mmeifanya pango la wapokonyaji.” 18 Na makuhani wakuu na waandishi wakasikia hilo, nao wakaanza kutafuta sana jinsi ya kumwangamiza; kwa maana walikuwa wakimhofu, kwa maana umati wote kwa kuendelea ulikuwa ukistaajabishwa na fundisho lake.
19 Na ilipokuwa jioni-jioni, walikuwa wakienda kutoka jijini. 20 Lakini walipokuwa wakipita hapo mapema asubuhi, wakaona ule mtini tayari umenyauka kabisa toka mizizi. 21 Kwa hiyo Petro, akiukumbuka, akamwambia: “Rabi, ona! ule mtini uliolaani umenyauka kabisa.” 22 Na kwa kujibu Yesu akawaambia: “Iweni na imani katika Mungu. 23 Kwa kweli nawaambia nyinyi kwamba yeyote yule aambiaye mlima huu, ‘Inuliwa na utupwe ndani ya bahari,’ na hatii shaka moyoni mwake lakini ana imani kwamba yale asemayo yatatukia, itakuwa hivyo kwake. 24 Hii ndiyo sababu nawaambia nyinyi, Mambo yote msaliyo na kuomba iweni na imani kwamba ni kama tayari mmeyapokea, nanyi mtakuwa nayo. 25 Na msimamapo mkisali, sameheni chochote kile mlicho nacho dhidi ya yeyote; ili Baba yenu aliye katika mbingu apate kuwasamehe makosa yenu nyinyi pia.” 26 ——
27 Nao wakaja tena Yerusalemu. Na alipokuwa akitembea katika hekalu, makuhani wakuu na waandishi na wanaume wazee wakamjia 28 na kuanza kumwambia: “Ni kwa mamlaka gani wewe wafanya mambo haya? au ni nani aliyekupa wewe mamlaka hii kufanya mambo haya?” 29 Yesu akawaambia: “Hakika nitawauliza nyinyi swali moja. Nyinyi nijibuni mimi, nami pia hakika nitawaambia nyinyi ni kwa mamlaka gani nafanya mambo haya. 30 Je, ubatizo wa Yohana ulikuwa wa kutoka mbinguni au wa kutoka kwa wanadamu? Nijibuni.” 31 Kwa hiyo wakaanza kujadiliana kwa kutoa sababu miongoni mwao wenyewe, wakisema: “Tukisema, ‘Kutoka mbinguni,’ atasema, ‘Basi, kwa nini hamkumwamini?’ 32 Lakini tukithubutu kusema, ‘Kutoka kwa wanadamu’?”—Walikuwa wakihofu umati, kwa maana huo wote ulichukua kwamba Yohana alikuwa kwa kweli amekuwa ni nabii. 33 Basi, kwa kumjibu Yesu wakasema: “Hatujui.” Naye Yesu akawaambia: “Wala mimi siwaambii nyinyi ni kwa mamlaka gani nafanya mambo haya.”