Marko
12 Pia, akaanza kusema nao kwa vielezi: “Mtu alipanda shamba la mizabibu, akaweka ua kulizunguka, akachimba pipa la sindikio la divai na kusimamisha mnara, akalikodisha kwa walimaji, akasafiri nchi ya nje. 2 Sasa katika majira yapasayo akatuma mtumwa kwa walimaji, ili aweze kupata baadhi ya matunda ya shamba la mizabibu kutoka kwa walimaji. 3 Lakini wakamchukua, wakampiga sana na kumwacha aende bila kitu. 4 Na tena akatuma mtumwa mwingine kwao; na huyo wakampiga kichwani na kumvunjia heshima. 5 Naye akatuma mwingine, na huyo wakamuua; na wengine wengi, baadhi yao waliwapiga sana na baadhi yao waliwaua. 6 Alikuwa na mmoja zaidi, mwana mpendwa. Akamtuma mwisho kwao, akisema, ‘Watamstahi mwana wangu.’ 7 Lakini walimaji hao wakasema miongoni mwao wenyewe, ‘Huyu ndiye mrithi. Njoni, acheni tumuue, na urithi utakuwa wetu.’ 8 Kwa hiyo wakamchukua wakamuua, na kumtupa nje ya shamba la mizabibu. 9 Mwenye kumiliki shamba la mizabibu atafanya nini? Atakuja na kuwaangamiza walimaji, na atawapa wengine shamba la mizabibu. 10 Je, hamkusoma kamwe andiko hili, ‘Jiwe walilolikataa wajenzi, limekuwa jiwe la pembeni lililo kuu. 11 Kutoka kwa Yehova hilo limekuja kuwa, na ni la kustaajabisha machoni petu’?”
12 Ndipo wakaanza kutafuta sana jinsi ya kumkamata, lakini walihofu umati, kwa maana walijua kwamba alisema kile kielezi akiwafikiria wao. Kwa hiyo wakamwacha wakaenda zao.
13 Halafu wakatuma kwake baadhi ya Mafarisayo na wafuasi wa chama cha Herode, kumnasa katika usemi wake. 14 Hao walipowasili wakamwambia: “Mwalimu, twajua wewe ni mwenye ukweli na hujali yeyote, kwa maana hutazami kuonekana kwa nje kwa watu, bali wafundisha njia ya Mungu kupatana na kweli: Je, yaruhusika kisheria kumlipa Kaisari kodi ya kichwa au la? 15 Je, tutalipa, au hatutalipa?” Akigundua unafiki wao, akawaambia: “Kwa nini mwanitia kwenye jaribu? Nileteeni dinari niitazame.” 16 Wakaleta moja. Naye akawaambia: “Sanamu na mwandiko huu ni wa nani?” Wakamwambia: “Wa Kaisari.” 17 Ndipo Yesu akasema: “Mlipeni Kaisari vitu vya Kaisari, lakini mlipeni Mungu vitu vya Mungu.” Nao wakaanza kumstaajabia.
18 Sasa Masadukayo wakamjia, wasemao hakuna ufufuo, nao wakamtokezea swali hili: 19 “Mwalimu, Musa alituandikia kwamba ikiwa ndugu ya mtu fulani afa na aacha mke nyuma lakini haachi mtoto, ndugu yake apaswa kumchukua huyo mke na kuinua uzao kutoka kwake kwa ajili ya ndugu yake. 20 Kulikuwa na ndugu saba; na wa kwanza akamchukua mke, lakini alipokufa hakuacha uzao wowote. 21 Na yule wa pili akamchukua, lakini akafa bila kuacha uzao; na yule wa tatu njia ileile. 22 Na wale saba hawakuacha uzao wowote. Mwisho wa wote yule mwanamke akafa pia. 23 Katika ufufuo yeye atakuwa mke wa yupi kati ya hao? Kwa maana wale saba walimpata kuwa mke wao.” 24 Yesu akawaambia: “Je, si hiyo ndiyo sababu mmekosea, kutojua kwenu ama Maandiko ama nguvu ya Mungu? 25 Kwa maana wafufuliwapo kutoka kwa wafu, wanaume hawaoi wala wanawake hawaozwi, bali wao ni kama malaika katika mbingu. 26 Lakini kuhusu wafu, kwamba wafufuliwa, je, hamkusoma katika kitabu cha Musa, katika simulizi juu ya kijiti cha miiba, jinsi Mungu alivyomwambia, ‘Mimi ni Mungu wa Abrahamu na Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo’? 27 Yeye ni Mungu, si wa wafu, bali wa walio hai. Mmekosea sana.”
28 Sasa mmoja wa waandishi aliyekuwa amekuja na kuwasikia wakibishana, akijua kwamba alikuwa amewajibu kwa njia bora, akamuuliza: “Ni amri ipi iliyo ya kwanza kati ya zote?” 29 Yesu akajibu: “Ya kwanza ni hii, ‘Sikia, Ewe Israeli, Yehova Mungu wetu ni Yehova mmoja, 30 nawe lazima umpende Yehova Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa nafsi yako yote na kwa akili yako yote na kwa nguvu zako zote.’ 31 Ya pili ni hii, ‘Lazima umpende jirani yako kama wewe mwenyewe.’ Hakuna amri nyingine yoyote iliyo kubwa zaidi kuliko hizi.” 32 Yule mwandishi akamwambia: “Mwalimu, ulisema vema kupatana na kweli, ‘Yeye ni Mmoja, na hakuna mwingine ila Yeye’; 33 na huku kumpenda kwa moyo wote wa mtu na kwa uelewevu wote wa mtu na kwa nguvu zote za mtu na huku kumpenda jirani ya mtu kama yeye mwenyewe ni bora zaidi sana kuliko matoleo yote mazima ya kuchomwa na dhabihu zote.” 34 Ndipo Yesu, akifahamu kwamba alikuwa amejibu kwa kutumia akili, akamwambia: “Wewe hauko mbali na ufalme wa Mungu.” Lakini hakuna mtu aliyekuwa tena kamwe na moyo wa kumuuliza swali.
35 Hata hivyo, alipokuwa akitoa jibu, Yesu akaanza kusema akifundisha katika hekalu: “Ni jinsi gani waandishi husema kwamba Kristo ni mwana wa Daudi? 36 Kwa roho takatifu Daudi mwenyewe alisema, ‘Yehova alimwambia Bwana wangu: “Keti kwenye mkono wangu wa kuume mpaka niweke maadui wako chini ya miguu yako.”’ 37 Daudi mwenyewe humwita yeye ‘Bwana,’ lakini yawaje kwamba yeye ni mwana wake?”
Na umati mkubwa ulikuwa ukimsikiliza kwa upendezi. 38 Na katika fundisho lake akaendelea kusema: “Jihadharini na waandishi ambao hutaka kutembea wakizunguka wakiwa wamevaa makanzu na hutaka salamu katika mahali pa masoko 39 na viti vya mbele katika masinagogi na mahali pa kutokeza zaidi sana kwenye milo ya jioni. 40 Wao ndio wanaozinyafua nyumba za wajane na kwa kisingizio wanafanya sala zilizo ndefu; hawa watapokea hukumu nzito zaidi.”
41 Naye akaketi akitazama masanduku ya hazina na kuanza kuangalia jinsi umati ulivyokuwa ukitumbukiza fedha ndani ya masanduku ya hazina; na matajiri wengi walikuwa wakitumbukiza ndani sarafu nyingi. 42 Sasa mjane fulani maskini akaja akatumbukiza ndani sarafu ndogo mbili, ambazo zina thamani ndogo sana. 43 Kwa hiyo akawaita wanafunzi wake na kuwaambia: “Kwa kweli nawaambia nyinyi kwamba mjane maskini huyu alitumbukiza ndani zaidi ya wote wale waliokuwa wakitumbukiza fedha ndani ya masanduku ya hazina; 44 kwa maana wote walitumbukiza ndani kutokana na ziada yao, lakini yeye, kutokana na uhitaji wake, alitumbukiza ndani vyote alivyokuwa navyo, riziki yake yote.”