Marko
13 Alipokuwa akienda kutoka hekaluni mmoja wa wanafunzi wake alimwambia: “Mwalimu, ona! namna ya mawe na namna ya majengo!” 2 Hata hivyo, Yesu akamwambia: “Waona majengo makubwa haya? Kwa vyovyote jiwe halitaachwa hapa juu ya jiwe lisitupwe chini.”
3 Na alipokuwa ameketi juu ya Mlima wa Mizeituni hekalu likiwa laonekana, Petro na Yakobo na Yohana na Andrea wakaanza kumuuliza kwa faragha: 4 “Tuambie, mambo haya yatakuwa wakati gani, na ishara itakuwa nini wakati mambo yote haya yakusudiwapo kufikia umalizio?” 5 Kwa hiyo Yesu akaanza kuwaambia: “Jihadharini kwamba mtu yeyote asiwaongoze nyinyi vibaya. 6 Wengi watakuja juu ya msingi wa jina langu, wakisema, ‘Mimi ndiye,’ na wataongoza wengi vibaya. 7 Zaidi ya hayo, msikiapo juu ya vita na ripoti za vita, msiogofishwe; mambo hayo lazima yatukie, lakini mwisho bado.
8 “Kwa maana taifa litainuka dhidi ya taifa na ufalme dhidi ya ufalme, kutakuwa na matetemeko ya dunia mahali pamoja baada ya pengine, kutakuwa na upungufu wa chakula. Hayo ni mwanzo wa maumivu makali ya ghafula ya taabu.
9 “Kwa habari yenu, jihadharini nyinyi wenyewe; watu watawakabidhi nyinyi kwenye mahakama za mahali, nanyi mtapigwa katika masinagogi na kufanywa msimame mbele ya magavana na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushahidi kwao. 10 Pia, katika mataifa yote lazima habari njema ihubiriwe kwanza. 11 Lakini wanapowaongoza nyinyi ili kuwakabidhi, msihangaike kimbele juu ya ni jambo gani mtasema; bali lolote lile mpewalo katika saa hiyo, semeni hilo, kwa maana si nyinyi mnaosema, bali ni roho takatifu. 12 Zaidi ya hilo, ndugu atakabidhi ndugu kwenye kifo, na baba atakabidhi mtoto, na watoto watainuka dhidi ya wazazi na kufanya wauawe; 13 nanyi mtakuwa vitu vya kuchukiwa na watu wote kwa sababu ya jina langu. Lakini yeye ambaye amevumilia hadi mwisho ndiye atakayeokolewa.
14 “Hata hivyo, mwonapo mara hiyo kile kitu chenye kuchukiza sana ambacho husababisha ukiwa kikiwa kimesimama ambapo hakipaswi (mwacheni msomaji atumie ufahamu), ndipo waacheni wale walio katika Yudea waanze kukimbilia milimani. 15 Mwacheni mtu aliye juu ya paa ya nyumba asiteremke, wala asiingie ndani kuchukua kitu chochote kutoka nyumbani mwake; 16 na mwacheni mtu aliye katika shamba asirudi kwa mambo yaliyo nyuma kuchukua vazi lake la nje. 17 Ole wao wanawake wenye mimba na wale wanaonyonyesha kitoto kichanga katika siku hizo! 18 Fulizeni kusali kwamba isipate kutukia wakati wa majira ya baridi kali; 19 kwa maana siku hizo zitakuwa siku za dhiki ya namna ambayo haijatukia tangu mwanzo wa viumbe ambavyo Mungu aliumba hadi wakati huo, na haitatukia tena. 20 Kwa kweli, kama Yehova hangekuwa amezikata siku hizo ziwe fupi, hakuna mwili ambao ungeokolewa. Lakini yeye amezikata siku hizo ziwe fupi kwa sababu ya wachaguliwa ambao amechagua.
21 “Ndipo, pia, yeyote akiwaambia, ‘Oneni! Kristo ni huyu hapa,’ ‘Oneni! yule pale,’ msiamini hilo. 22 Kwa maana Makristo wasio wa kweli na manabii wasio wa kweli watainuka na kuzitoa ishara na maajabu ili kuongoza wapotee njia, ikiwezekana, wachaguliwa. 23 Basi, nyinyi jihadharini; nimewaambia mambo yote kimbele.
24 “Lakini katika siku hizo, baada ya dhiki hiyo, jua litatiwa giza, na mwezi hautatoa nuru yao, 25 nazo nyota zitakuwa zikianguka kutoka mbinguni na nguvu zilizo katika mbingu zitatikiswa. 26 Na ndipo watakapomwona Mwana wa binadamu akija katika mawingu pamoja na nguvu kubwa na utukufu. 27 Na ndipo atakapowatuma malaika na kuwakusanya wachaguliwa wake pamoja kutoka zile pepo nne, kutoka ncha ya dunia hadi ncha ya mbingu.
28 “Basi kutokana na mtini jifunzeni hiki kielezi: Mara tu tawi lao changa likuapo kuwa jororo na kutoa majani yalo, mwajua kwamba kiangazi kiko karibu. 29 Hivyohivyo pia nyinyi, mwonapo mambo hayo yakitukia, jueni kwamba yuko karibu, kwenye milango. 30 Kwa kweli nawaambia nyinyi kwamba kizazi hiki hakitapitilia mbali kwa vyovyote mpaka mambo yote hayo yatukie. 31 Mbingu na dunia zitapitilia mbali, bali maneno yangu hayatapitilia mbali.
32 “Kuhusu siku hiyo au saa hakuna mtu ajuaye, wala malaika mbinguni wala Mwana, ila Baba. 33 Fulizeni kutazama, fulizeni kuwa macho, kwa maana hamjui ni lini ulio wakati uliowekwa rasmi. 34 Ni kama mtu asafiriye kwenda nchi ya nje aliyeacha nyumba yake akawapa mamlaka watumwa wake, kila mmoja kazi yake, na kumwamuru mtunza-mlango kufuliza kulinda. 35 Kwa hiyo fulizeni kulinda, kwa maana nyinyi hamjui ni wakati gani bwana-mkubwa wa nyumba anakuja, kama ni wakati wa jioni-jioni au katikati ya usiku au awikapo jogoo au mapema asubuhi; 36 ili awasilipo kwa ghafula, asiwakute nyinyi mkiwa mmelala usingizi. 37 Lakini lile niwaambialo nyinyi nawaambia wote, Fulizeni kulinda.”