Matendo
22 “Wanaume, akina ndugu na akina baba, sikieni kujitetea kwangu kwenu sasa.” 2 (Basi, waliposikia alikuwa akisema nao katika lugha ya Kiebrania, wakafuliza kukaa kimya hata zaidi, naye akasema:) 3 “Mimi ni Myahudi, aliyezaliwa katika Tarso ya Kilikia, lakini aliyeelimishwa katika jiji hili penye miguu ya Gamalieli, nikiwa nimefunzwa kwa usahihi kabisa Sheria ya akina baba wa kale, nikiwa mwenye bidii kuhusu Mungu kama vile nyinyi nyote mlivyo siku hii. 4 Nami nilinyanyasa Njia hii hadi kifo, nikifunga na kukabidhi kwenye magereza wanaume na wanawake pia, 5 kama ambavyo kuhani wa cheo cha juu na pia kusanyiko lote la wanaume wazee wawezavyo kunitolea ushahidi. Kutoka kwao nilipata pia barua nizipeleke kwa akina ndugu katika Damasko, nami nilikuwa nimeshika njia yangu kwenda kuwaleta wale waliokuwa huko pia hadi Yerusalemu wakiwa wamefungwa ili waadhibiwe.
6 “Lakini nilipokuwa nikisafiri na kukaribia Damasko, karibu katikati ya mchana, kwa ghafula kutoka mbinguni nuru kubwa ikamweka kunizunguka, 7 nami nikaanguka kwenye ardhi na kusikia sauti ikiniambia, ‘Sauli, Sauli, kwa nini unaninyanyasa?’ 8 Mimi nikajibu, ‘Wewe ni nani, Bwana?’ Naye akaniambia, ‘Mimi ni Yesu Mnazareti, ambaye wewe unanyanyasa.’ 9 Basi watu waliokuwa pamoja nami wakaona, kwa kweli, hiyo nuru lakini hawakuisikia sauti ya mwenye kusema nami. 10 Ndipo nikasema, ‘Nitafanya nini, Bwana?’ Bwana akaniambia, ‘Inuka, shika njia yako uende kuingia katika Damasko, na huko utaambiwa juu ya kila kitu ambacho umewekewa kufanya.’ 11 Lakini kwa kuwa singeweza kuona kitu chochote kwa sababu ya utukufu wa nuru hiyo, nikawasili Damasko, nikiwa naongozwa kwa mkono wa wale waliokuwa pamoja nami.
12 “Basi Anania, mwanamume fulani mwenye kumhofu Mungu kulingana na Sheria, mwenye kuripotiwa vema na Wayahudi wote wenye kukaa huko, 13 akanijia na, akisimama kando yangu, akaniambia, ‘Sauli, ndugu, pata kuona tena!’ Nami nikatazama juu kumwelekea saa ileile. 14 Yeye akasema, ‘Mungu wa baba zetu wa zamani amekuchagua uje kujua mapenzi yake na kuona yule Aliye mwadilifu na kuisikia sauti ya kinywa chake, 15 kwa sababu wewe wapaswa kuwa shahidi kwa ajili yake kwa watu wote juu ya mambo ambayo umeona na kusikia. 16 Na sasa kwa nini unakawia? Inuka, ubatizwe na uoshe dhambi zako kwa kuitia jina lake.’
17 “Lakini nilipokuwa nimerudi Yerusalemu na nikiwa nasali hekaluni, nikaingia katika njozi 18 na kumwona akiniambia, ‘Fanya upesi uondoke Yerusalemu haraka, kwa sababu hawatakubali ushahidi wako kunihusu.’ 19 Nami nikasema, ‘Bwana, wao wenyewe wajua vema kwamba nilikuwa na kawaida ya kuwatia gerezani na kuwapiga viboko katika sinagogi moja baada ya jingine wale wenye kuamini juu yako; 20 na wakati damu ya Stefano shahidi wako ilipokuwa ikimwagwa, mimi mwenyewe nilikuwa pia nimesimama kando nikikubaliana na kulinda mavazi ya nje ya hao waliokuwa wakimmaliza.’ 21 Na bado akaniambia, ‘Shika njia yako uende, kwa sababu mimi nitakutuma nje mbali sana kwa mataifa.’”
22 Basi wakafuliza kumsikiliza mpaka kwenye neno hili, nao wakainua sauti zao, wakisema: “Mwondolee mbali mtu wa namna hiyo duniani, kwa maana yeye hakufaa kuishi!” 23 Na kwa sababu walikuwa wakipaaza kilio na kutupa mavazi yao ya nje huku na huku na kurusha mavumbi hewani, 24 yule kamanda wa kijeshi akaagiza aingizwe katika makao ya askari-jeshi na kusema apaswa kuchunguzwa kwa kupigwa mijeledi, ili apate kujua kabisa ni kwa sababu gani walikuwa wakipaaza sauti dhidi yake kwa njia hii. 25 Lakini walipokuwa wamemnyoosha ili apigwe mijeledi, Paulo akamwambia ofisa-jeshi aliyesimama hapo: “Je, yaruhusika kisheria kwa nyinyi watu kupiga mijeledi mtu ambaye ni Mroma na ambaye hajahukumiwa kuwa mwenye hatia?” 26 Basi, huyo ofisa-jeshi aliposikia hili, akaenda hadi kwa kamanda wa kijeshi na kutoa ripoti, akisema: “Unakusudia kufanya nini? Kwani, mtu huyu ni Mroma.” 27 Kwa hiyo kamanda wa kijeshi akakaribia na kumwambia: “Niambie, Je, wewe ni Mroma?” Akasema: “Ndiyo.” 28 Kamanda wa kijeshi akajibu: “Mimi nilinunua haki hizi kama raia kwa jumla kubwa ya fedha.” Paulo akasema: “Lakini mimi hata nilizaliwa katika hizo.”
29 Kwa hiyo, mara hiyo watu waliokuwa karibu kumchunguza kwa kutumia utesi-tesi wakajiondoa kwake; na kamanda wa kijeshi akawa mwenye kuogopa alipohakikisha kwamba alikuwa ni Mroma na kwamba alikuwa amemfunga.
30 Kwa hiyo, siku iliyofuata, kwa kuwa alitaka kujua kwa hakika ni kwa nini hasa alikuwa akishtakiwa na Wayahudi, akamfungua na kuwaamuru makuhani wakuu na Sanhedrini yote wakusanyike. Naye akamleta Paulo chini na kumsimamisha miongoni mwao.