Matendo
21 Sasa tulipokuwa tumejibandua kutoka kwao kwa nguvu na kusafiri baharini, tulikwenda kwa mwendo wa moja kwa moja tukaja hadi Kosi, lakini siku iliyofuata tukaja hadi Rodesi, na kutoka huko hadi Patara. 2 Na tulipokuwa tumepata mashua iliyokuwa ikivuka kwenda Foinike, tukapanda ndani tukasafiri kwenda zetu. 3 Baada ya kuja mahali tulipoweza kuona kisiwa cha Saiprasi tukakiacha nyuma upande wa kushoto tukasafiri kwa mashua hadi Siria, tukateremka hadi Tiro, kwa maana hapo mashua ilipaswa ipakue shehena yayo. 4 Kwa kutafuta tukawapata wanafunzi na kukaa hapo siku saba. Lakini kupitia roho wakarudiarudia kumwambia Paulo asiweke mguu katika Yerusalemu. 5 Kwa hiyo tulipokuwa tumekamilisha hizo siku, tukatoka na kuanza kushika njia yetu twende; lakini wao wote, pamoja na wanawake na watoto, wakatuongoza hadi nje ya jiji. Na tukipiga magoti pwani tukasali 6 na kuambiana kwaheri, nasi tukapanda kwenda ndani ya mashua lakini wao wakarudi nyumbani kwao.
7 Ndipo sisi tukakamilisha safari ya baharini kutoka Tiro tukawasili Tolemai, nasi tukasalimu akina ndugu na kukaa siku moja pamoja nao. 8 Siku iliyofuata tukaondoka tukawasili Kaisaria, nasi tukaingia katika nyumba ya Filipo mweneza-evanjeli, aliyekuwa mmoja wa wale watu saba, nasi tukakaa pamoja naye. 9 Mtu huyu alikuwa na mabinti wanne, mabikira, waliotoa unabii. 10 Lakini tulipokuwa tukikaa siku kadhaa, nabii fulani aitwaye jina Agabo akateremka kutoka Yudea, 11 naye akatujia na kuuchukua mshipi wa Paulo, akafunga miguu na mikono yake mwenyewe na kusema: “Hivi ndivyo isemavyo roho takatifu, ‘Mwanamume ambaye mshipi huu ni wake Wayahudi watamfunga kwa namna hii katika Yerusalemu na kumkabidhi mikononi mwa watu wa mataifa.’” 12 Sasa tuliposikia hili, sisi na pia wale wa mahali hapo tukaanza kumsihi sana asipande kwenda Yerusalemu. 13 Ndipo Paulo akajibu: “Mnafanya nini kwa kutoa machozi na kunifanya dhaifu moyoni? Mwe na uhakikishio, mimi niko tayari si kufungwa tu bali pia kufa Yerusalemu kwa ajili ya jina la Bwana Yesu.” 14 Alipokataa kushawishwa, tukakubali kwa kimya haya maneno: “Mapenzi ya Yehova na yatendeke.”
15 Sasa baada ya siku hizi tukajitayarisha kwa ajili ya safari tukaanza kupanda kwenda Yerusalemu. 16 Lakini wengine kati ya wanafunzi kutoka Kaisaria wakaenda pamoja nasi pia, ili kutuleta kwa mtu ambaye nyumbani mwake tulipaswa kupokewa, Mnasoni fulani wa Saiprasi, mwanafunzi wa mapema. 17 Tulipoingia Yerusalemu, akina ndugu wakatupokea kwa mteremo. 18 Lakini siku iliyofuata Paulo akaingia pamoja nasi kwa Yakobo; na wanaume wote wazee walikuwapo. 19 Naye akawasalimu na kuanza kusimulia kirefu juu ya mambo ambayo Mungu alifanya miongoni mwa mataifa kupitia huduma yake.
20 Baada ya kusikia hili wakaanza kumtukuza Mungu, nao wakamwambia: “Waona, ndugu, jinsi kulivyo na maelfu mengi ya waamini walio miongoni mwa Wayahudi; nao wote ni wenye bidii kuhusu Sheria. 21 Lakini wamesikia uvumi ukitolewa juu yako kwamba wewe umekuwa ukiwafundisha Wayahudi wote miongoni mwa mataifa uasi-imani wa kumwacha Musa, ukiwaambia wasitahiri watoto wao wala kujiendesha katika desturi za kisherehe. 22 Basi, ni nini kipaswacho kufanywa juu yalo? Kwa vyovyote vile watasikia umewasili. 23 Kwa hiyo fanya hili tukuambialo: Tuna wanaume wanne wenye nadhiri juu yao wenyewe. 24 Chukua watu hawa pamoja nawe ujisafishe mwenyewe kisherehe pamoja nao na kuwagharamia, ili wapate kunyolewa vichwa vyao. Na kwa hiyo kila mtu atajua kwamba uvumi mwingi walioambiwa juu yako hauna kitu, bali kwamba unatembea kwa utaratibu, wewe mwenyewe pia ukishika Sheria. 25 Kwa habari ya wale waamini kutoka miongoni mwa mataifa, tumetuma watu, tukitoa uamuzi wetu kwamba wao wapaswa kujiepusha wenyewe na kile ambacho kimetolewa dhabihu kwa sanamu vilevile na damu na kile ambacho kimenyongwa, na uasherati.”
26 Ndipo Paulo akawachukua hao wanaume pamoja naye siku iliyofuata akajisafisha mwenyewe kisherehe pamoja nao na kuingia ndani ya hekalu, kutoa taarifa juu ya siku ambazo zingetimizwa kwa huo utakaso wa kisherehe, mpaka toleo litolewe kwa ajili ya kila mmoja wao.
27 Sasa zile siku saba zilipokuwa karibu kumalizika, Wayahudi kutoka Asia walipomwona katika hekalu wakaanza kuutupa umati wote ndani ya mvurugo, nao wakamwekea mikono yao ili wamshike, 28 wakipaaza kilio: “Wanaume wa Israeli, saidieni! Huyu ni yule mwanamume afundishaye kila mtu kila mahali dhidi ya watu na Sheria na mahali hapa na, isitoshe, yeye hata aliingiza Wagiriki katika hekalu na amepatia unajisi mahali patakatifu hapa.” 29 Kwa maana hapo kwanza walikuwa wamemwona Trofimo Mwefeso katika jiji akiwa pamoja naye, lakini walikuwa wakiwazia Paulo alikuwa amemwingiza katika hekalu. 30 Na jiji lote likatiwa katika ghasia, na kukimbia pamoja kwa watu kukatukia; nao wakamshika Paulo wakamkokota nje ya hekalu. Na mara milango ikafungwa. 31 Na walipokuwa wakitafuta sana kumuua, habari ikamjia kamanda wa kikosi kwamba Yerusalemu lote lilikuwa katika mvurugo; 32 naye mara moja akachukua askari-jeshi na maofisa-jeshi na kuwakimbilia huko chini. Walipomwona mara hiyo huyo kamanda wa kijeshi na askari-jeshi, wakakoma kumpiga Paulo.
33 Ndipo kamanda wa kijeshi akaja karibu akamshika na kutoa amri afungwe minyororo miwili; naye akaanza kuulizia habari huenda huyo akawa nani na ni nini alilokuwa amefanya. 34 Lakini wengine katika umati wakaanza kupaaza sauti kuhusu jambo moja, na wengine jingine. Kwa hiyo, yeye mwenyewe akiwa hawezi kujua lolote la hakika kwa sababu ya hiyo fujo, akaamuru aletwe kwenye makao ya askari-jeshi. 35 Lakini alipofika juu ya ngazi, hali ikawa kwamba alikuwa akichukuliwa na wale askari-jeshi kwa sababu ya jeuri ya umati; 36 kwa maana umati wa watu ulifuliza kufuata, ukipaaza kilio: “Mwondolee mbali!”
37 Na alipokuwa karibu kuongozwa kuingia katika makao ya askari-jeshi, Paulo akamwambia kamanda wa kijeshi: “Je, naruhusiwa kukuambia jambo fulani?” Akasema: “Je, waweza kusema Kigiriki? 38 Je, kwa kweli wewe si yule Mmisri ambaye kabla ya siku hizi alichochea uchochezi wa uasi akaongoza watoke wale wanaume watumia-sime elfu nne kwenda kuingia nyikani?” 39 Ndipo Paulo akasema: “Mimi, kwa kweli, ni Myahudi wa Tarso katika Kilikia, raia wa jiji ambalo si lenye kukosa umashuhuri. Kwa hiyo nakuomba wewe, niruhusu niseme na hawa watu.” 40 Baada ya yeye kutoa ruhusa, Paulo, akiwa amesimama juu ya ngazi, akawapungia watu mkono wake. Kimya kikubwa kilipoingia, akawahutubia kwa lugha ya Kiebrania, akisema: