Matendo
20 Sasa baada ya hiyo ghasia kutulia, Paulo alituma watu waite wanafunzi, na alipokuwa amewatia moyo na kuwaaga, akaenda kufunga safari kuingia Makedonia. 2 Baada ya kupitia sehemu hizo na kuwatia moyo wale walio huko kwa maneno mengi, akaja kuingia Ugiriki. 3 Na alipokuwa ametumia miezi mitatu huko, kwa sababu njama ilitungwa dhidi yake na Wayahudi alipokuwa karibu kusafiri kwa mashua kwenda Siria, akakata shauri kurudi kupitia Makedonia. 4 Walikuwako wakiandamana naye Sopateri mwana wa Piro wa Berea, Aristarko na Sekundo wa Wathesalonike, na Gayo wa Derbe, na Timotheo, na kutoka wilaya ya Asia Tikiko na Trofimo. 5 Hawa wakaendelea na walikuwa wakitungojea katika Troasi; 6 lakini sisi tukaanza kusafiri baharini kutoka Filipi baada ya siku za keki zisizotiwa chachu, nasi tukawajia wao katika Troasi mnamo siku tano; na huko tukakaa siku saba.
7 Siku ya kwanza ya juma, tulipokuwa tumekusanyika pamoja ili kupata mlo, Paulo akaanza kuwahutubia, kwa kuwa alipaswa kuondoka siku ifuatayo; naye akarefusha hotuba yake mpaka katikati ya usiku. 8 Kwa hiyo kulikuwa na taa nyingi katika chumba cha juu tulikokuwa tumekusanyika pamoja. 9 Akiwa ameketi dirishani, mwanamume fulani kijana aitwaye jina Eutiko aliingia katika usingizi mzito huku Paulo akifuliza kuongea, na, akididimia katika usingizi, akaanguka chini kutoka orofa ya tatu akaokotwa amekufa. 10 Lakini Paulo akashuka orofani, akajitupa mwenyewe juu yake akamkumbatia na kusema: “Komeni kufanya makelele, kwa maana nafsi yake imo ndani yake.” 11 Sasa akapanda orofani na kuanza mlo akala chakula, na baada ya kuongea kwa muda mrefu, mpaka mapambazuko, hatimaye akaondoka. 12 Basi wakachukua huyo mvulana akiwa hai wakafarijiwa kupita kiasi.
13 Sasa tukaenda mbele kwenye mashua na kusafiri kwa mashua hadi Asosi, ambako tulikuwa tukikusudia kumpandisha Paulo katika mashua, kwa maana, baada ya kutoa maagizo hayo, yeye mwenyewe alikuwa akikusudia kwenda kwa miguu. 14 Kwa hiyo alipotufikia katika Asosi, tukampandisha katika mashua na kwenda hadi Mitilene; 15 na, tukisafiri kwa mashua kutoka huko siku yenye kufuatia, tukawasili upande wa pili wa Kiosi, lakini siku iliyofuata tukawasili Samosi, na siku iliyofuata hiyo tukawasili Mileto. 16 Kwa maana Paulo alikuwa ameamua kusafiri kwa mashua kupita Efeso, ili asitumie wakati wowote katika wilaya ya Asia; kwa maana alikuwa akifanya hima kufika Yerusalemu siku ya msherehekeo wa Pentekoste kama angeweza kwa vyovyote.
17 Hata hivyo, kutoka Mileto akatuma watu kwenda Efeso na kuita wanaume wazee wa hilo kutaniko waje. 18 Walipofika kwake akawaambia: “Nyinyi mwajua vema jinsi tangu siku ya kwanza niliyokanyaga wilaya ya Asia nilivyokuwa pamoja nanyi wakati wote, 19 nikitumika kama mtumwa kwa ajili ya Bwana nikiwa na hali ya akili ya kujishusha chini iliyo kubwa zaidi sana na machozi na majaribu yaliyonipata kwa njama za Wayahudi; 20 wakati uleule sikuepuka kuwaambia nyinyi lolote kati ya mambo yaliyokuwa yenye kuleta faida wala kuwafundisha nyinyi hadharani na kutoka nyumba hadi nyumba. 21 Lakini nilitoa ushahidi kikamili kwa Wayahudi na Wagiriki pia juu ya toba kuelekea Mungu na imani katika Bwana wetu Yesu. 22 Na sasa, tazameni! nikiwa nimefungwa katika roho, mimi ninafunga safari kwenda Yerusalemu, ijapokuwa sijui mambo yatakayotukia kwangu katika jiji hilo, 23 ila kwamba kutoka jiji hadi jiji roho takatifu hutoa ushahidi kwangu kwa kurudiarudia isemapo kwamba vifungo na dhiki vinaningojea. 24 Hata hivyo, siifanyi nafsi yangu kuwa kitu chenye thamani sana kwangu, kama tu ningepata kumaliza mwendo wangu na huduma niliyopokea ya Bwana Yesu, kutoa ushahidi kamili kuhusu habari njema ya fadhili isiyostahiliwa ya Mungu.
25 “Na sasa, tazameni! mimi najua kwamba nyinyi nyote ambao nilienda miongoni mwenu nikihubiri ufalme hamtaona uso wangu tena. 26 Kwa sababu hiyo nawaita nyinyi kuona ushahidi siku hiihii kwamba mimi ni safi kutokana na damu ya watu wote, 27 kwa maana sikuepuka kuwaambia nyinyi shauri lote la Mungu. 28 Kazieni uangalifu kwa nyinyi wenyewe na kundi lote, ambalo miongoni mwalo roho takatifu imewaweka nyinyi rasmi kuwa waangalizi, kulichunga kutaniko la Mungu, ambalo alilinunua kwa damu ya Mwana wake mwenyewe. 29 Mimi najua kwamba baada ya kwenda zangu mbwa-mwitu wenye kuonea wataingia miongoni mwenu na hawatalitendea kundi kwa wororo, 30 na kutoka miongoni mwenu nyinyi wenyewe wanaume watainuka na kusema mambo yaliyopotoka ili kuvuta wanafunzi wawafuate wao wenyewe.
31 “Kwa hiyo fulizeni kuwa macho, na zingatieni akilini kwamba kwa miaka mitatu, usiku na mchana, sikukoma kuonya kwa upole kila mmoja kwa machozi. 32 Na sasa nawakabidhi nyinyi kwa Mungu na kwa neno la fadhili yake isiyostahiliwa, neno ambalo laweza kuwajenga nyinyi na kuwapa nyinyi urithi miongoni mwa wale wote waliotakaswa. 33 Sikutamani fedha au dhahabu au vao la mtu. 34 Nyinyi wenyewe mwajua kwamba mikono hii imehudumia mahitaji yangu na ya wale walio pamoja nami. 35 Nimewaonyesha wazi nyinyi katika mambo yote kwamba kwa kufanya kazi ya jasho hivyo ni lazima msaidie wale walio dhaifu, na lazima mzingatie akilini maneno ya Bwana Yesu, wakati yeye mwenyewe aliposema, ‘Kuna furaha zaidi katika kutoa kuliko kulivyo katika kupokea.’”
36 Na alipokuwa amesema mambo haya, akapiga magoti pamoja nao wote na kusali. 37 Kwa kweli, kutoa machozi kwingi kulitokea miongoni mwao wote, nao wakaangukia shingo ya Paulo na kumbusu kwa wororo, 38 kwa sababu waliumizwa hasa na neno alilosema kwamba hawangeona uso wake tena. Basi wakaanza kumsindikiza hadi kwenye mashua.