Matendo
19 Ikawa, Apolo alipokuwa Korintho, Paulo alipita katika sehemu za barani na kuteremka hadi Efeso, akakuta wanafunzi fulani; 2 naye akawaambia: “Je, mlipokea roho takatifu mlipopata kuwa waamini?” Wakamwambia: “Lo! hatujapata kusikia kamwe kama kuna roho takatifu.” 3 Naye akasema: “Basi, mlibatizwa katika nini?” Wakasema: “Katika ubatizo wa Yohana.” 4 Paulo akasema: “Yohana alibatiza kwa ubatizo katika ufananisho wa toba, akiwaambia watu wamwamini yule aliyekuwa akija baada yake, yaani, Yesu.” 5 Waliposikia hilo, wakapata kubatizwa katika jina la Bwana Yesu. 6 Na Paulo alipowawekea mikono yake, roho takatifu ikaja juu yao, nao wakaanza kusema katika lugha na kutoa unabii. 7 Wote pamoja, kulikuwa na wanaume karibu kumi na wawili.
8 Akiingia katika sinagogi, akasema kwa ujasiri kwa miezi mitatu, akitoa hotuba na kutumia ushawishi kuhusu ufalme wa Mungu. 9 Lakini wengine walipoendelea kujifanya wenyewe wagumu na kutoamini, wakisema vibaya juu ya Ile Njia mbele ya umati, akaondoka kwao na kuwatenga wanafunzi kutoka kwao, kila siku akitoa hotuba nyingi katika jumba la hadhira la shule ya Tirano. 10 Hilo lilitukia kwa miaka miwili, hivi kwamba wote wale wenye kuikaa wilaya ya Asia wakasikia neno la Bwana, Wayahudi na Wagiriki pia.
11 Na Mungu akafuliza kufanya kazi za nguvu zizidizo za kawaida kupitia mikono ya Paulo, 12 hivi kwamba hata nguo na aproni zilichukuliwa kutoka katika mwili wake hadi kwa watu wenye kuugua, na maradhi yakawaacha, na roho waovu wakatoka. 13 Lakini watu fulani kati ya Wayahudi wenye kuzunguka-zunguka waliozoea kazi ya kufukuza roho waovu pia walichukua daraka la kuitia jina la Bwana Yesu juu ya wale wenye roho waovu, wakisema: “Mimi nawaagiza nyinyi kwa uzito kwa Yesu ambaye Paulo huhubiri.” 14 Sasa kulikuwa na wana saba wa Skeva fulani, kuhani mkuu wa Kiyahudi, wakifanya hili. 15 Lakini kwa kujibu roho mwovu akawaambia: “Mimi namjua Yesu nami nafahamu Paulo; lakini nyinyi ni nani?” 16 Ndipo huyo mtu ambaye huyo roho mwovu alikuwa ndani yake akawarukia, akawazidi nguvu mmoja baada ya mwingine, na kuwaweza, hivi kwamba wakakimbia kutoka nyumba hiyo wakiwa uchi na wamejeruhiwa. 17 Hili likawa lenye kujulikana kwa wote, Wayahudi na Wagiriki pia waliokaa katika Efeso; na hofu ikawaingia wao wote, na jina la Bwana Yesu likaendelea kutukuzwa. 18 Na wengi wa wale waliokuwa wamepata kuwa waamini wakawa wanakuja na kuungama na kuripoti mazoea yao waziwazi. 19 Kwa kweli, idadi kubwa ya wale waliozoea kufanya ufundi wa kimzungu wakaleta pamoja vitabu vyao wakavichoma kabisa mbele ya kila mtu. Nao wakapiga pamoja hesabu za bei zavyo na kukuta vikiwa na thamani ya vipande elfu hamsini vya fedha. 20 Hivyo katika njia yenye uweza neno la Yehova likafuliza kukua na kuweza.
21 Sasa mambo hayo yalipokuwa yametimilizwa, Paulo akakusudia katika roho yake kwamba, baada ya kupitia Makedonia na Akaya, angefunga safari kwenda Yerusalemu, akisema: “Baada ya mimi kufika huko lazima pia nione Roma.” 22 Kwa hiyo akatuma kwenda Makedonia wawili wa wale waliomhudumia, Timotheo na Erasto, lakini yeye mwenyewe akakawia kwa wakati fulani katika wilaya ya Asia.
23 Kwenye wakati huo maalumu kulitokea vurugu isiyo ndogo kuhusu Ile Njia. 24 Kwa maana mtu fulani aitwaye jina Demetrio, mfua-fedha, kwa kufanya vihekalu vya fedha vya Artemisi aliwapa wasanii pato la faida isiyo ndogo; 25 naye akawakusanya wao na wale waliofanya kazi ya kutengeneza vitu vya namna hiyo na kusema: “Wanaume, nyinyi mwajua vema kwamba kutokana na biashara hii sisi tuna ufanisi wetu. 26 Pia, mwaona na kusikia jinsi si katika Efeso tu bali pia katika karibu wilaya yote ya Asia Paulo huyu ameshawishi umati mkubwa na kuwageuza kwenye kauli nyingine, akisema kwamba wale waliofanywa kwa mikono si miungu. 27 Zaidi ya hayo, hatari ipo si kwamba tu shughuli hii yetu itaingizwa katika sifa mbaya bali pia kwamba hekalu la mungu-mke mkubwa Artemisi litakadiriwa kuwa si kitu na hata fahari yake ambayo wilaya yote ya Asia na dunia inayokaliwa huiabudu iko karibu kushushwa iwe si kitu.” 28 Waliposikia hilo na wakipata kujaa hasira, hao watu wakaanza kupaaza kilio, wakisema: “Ni Mkubwa Artemisi wa Waefeso!”
29 Kwa hiyo jiji likawa lenye kujawa na mvurugo, na kwa umoja wakatimua mbio kali kuingia mahali pa michezo, wakichukua kwa nguvu pamoja nao Gayo na Aristarko, Wamakedonia, waandamani-wasafiri wa Paulo. 30 Kwa upande wake, Paulo alikuwa anapenda kuingia walimo watu, lakini wanafunzi hawakumruhusu. 31 Hata baadhi ya makamishna wa misherehekeo na michezo, waliokuwa wenye urafiki kwake, wakatuma watu kwake na kuanza kumwomba asijihatarishe mwenyewe mahali pa michezo. 32 Kwa kweli, wengine walikuwa wakipaaza kilio cha jambo moja na wengine cha jingine; kwa maana kusanyiko lilikuwa katika mvurugo, na walio wengi kati yao hawakujua sababu kwa nini walikuwa wamekuja pamoja. 33 Kwa hiyo wakiwa pamoja wakamleta Aleksanda nje ya umati, Wayahudi wakimsukuma kwa nguvu mbele; na Aleksanda akapunga mkono wake naye alikuwa akitaka kujitetea kwa watu. 34 Lakini walipotambua kwamba alikuwa Myahudi, kilio kimoja kikatoka kwao wote walipokuwa wakipaaza sauti kwa karibu saa mbili: “Ni Mkubwa Artemisi wa Waefeso!”
35 Mwishowe, karani wa jiji alipokuwa ameunyamazisha umati kuwa kimya, akasema: “Wanaume wa Efeso, ni nani aliyeko kwa kweli kati ya wanadamu asiyejua kwamba jiji la Efeso ndilo mtunza-hekalu wa Artemisi mkubwa na wa sanamu iliyoanguka kutoka mbinguni? 36 Kwa hiyo kwa kuwa mambo haya ni yasiyokanikana, inafaa nyinyi mwe shwari na msitende haraka bila kufikiri. 37 Kwa maana mmeleta wanaume hawa wasio wapokonya-mahekalu wala wakufuru wa mungu-mke wetu. 38 Kwa hiyo ikiwa Demetrio na wasanii walio pamoja naye wana kesi dhidi ya mtu fulani, siku za mahakama hufanywa na kuna maprokonso; acheni walete mashtaka mtu dhidi ya mwenzake. 39 Lakini, ikiwa mnatafuta sana jambo lolote kupita hilo, lazima liamuliwe katika kusanyiko la kawaida. 40 Kwa maana kwa kweli tuko katika hatari ya kushtakiwa uchochezi wa uasi kuhusu tukio la leo, kukiwa hakuna msingi wowote mmoja ulioko utakaoturuhusu tutoe sababu ya kikundi hiki chenye ghasia kisicho na utaratibu.” 41 Na alipokuwa amesema mambo haya, akaagiza kusanyiko liende.