Matendo
23 Akikazia macho Sanhedrini Paulo akasema: “Wanaume, akina ndugu, mimi nimejiendesha mbele ya Mungu kwa dhamiri iliyo safi kikamilifu hadi siku hii.” 2 Ndipo kuhani wa cheo cha juu Anania akawaagiza wale waliosimama kando yake wampige kinywani. 3 Ndipo Paulo akamwambia: “Mungu atakupiga wewe, ewe ukuta uliopakwa chokaa. Je, wakati uleule mmoja waketi kunihukumu kupatana na Sheria na, kwa kukiuka Sheria, waamuru nipigwe?” 4 Wale waliosimama kando wakasema: “Je, wewe unamtukana kuhani wa cheo cha juu wa Mungu?” 5 Na Paulo akasema: “Akina ndugu, sikujua yeye ni kuhani wa cheo cha juu. Kwa maana imeandikwa, ‘Wewe hupaswi kusema vibaya juu ya mtawala wa watu wako.’”
6 Sasa Paulo alipojua kwamba sehemu moja ilikuwa ya Masadukayo lakini ile nyingine ya Mafarisayo, akaanza kupaaza kilio katika hiyo Sanhedrini: “Wanaume, akina ndugu, mimi ni Farisayo, mwana wa Mafarisayo. Juu ya tumaini la ufufuo wa wafu ninahukumiwa.” 7 Kwa sababu alisema hili, mtengano ukatokea kati ya Mafarisayo na Masadukayo, na umati ukagawanyika. 8 Kwa maana Masadukayo husema hakuna ufufuo wala malaika wala roho, lakini Mafarisayo hutangaza yote hadharani. 9 Kwa hiyo kukatokea kupiga yowe kwa sauti kubwa, na wengine kati ya waandishi wa chama cha Mafarisayo wakainuka na kuanza kushindana vikali, wakisema: “Sisi hatupati kosa lolote katika mtu huyu; lakini ikiwa roho au malaika alisema naye,—.” 10 Basi mtengano ulipokuwa mkubwa, kamanda wa kijeshi akawa mwenye kuogopa kwamba Paulo angeraruliwa nao vipande-vipande, naye akaamuru jeshi la askari literemke liende limmnyakue kutoka katikati yao na kumleta ndani ya makao ya askari-jeshi.
11 Lakini usiku uliofuata Bwana akasimama kando yake na kusema: “Uwe mwenye moyo mkuu! Kwa maana kama ambavyo umekuwa ukitoa ushahidi kamili katika Yerusalemu juu ya mambo yanihusuyo, ndivyo lazima pia utoe ushahidi katika Roma.”
12 Sasa ilipopata kuwa mchana, Wayahudi wakafanya njama na kujifunga wenyewe kwa laana, wakisema hawangekula wala kunywa mpaka wawe wamemuua Paulo. 13 Kulikuwa na zaidi ya watu arobaini waliofanya njama hii iliyofungwa kwa kiapo; 14 nao wakaenda kwa makuhani wakuu na wanaume wazee na kusema: “Sisi tumejifunga wenyewe chini ya laana kwa uzito kutouma chakula mpaka tuwe tumemuua Paulo. 15 Kwa hiyo, basi, nyinyi pamoja na Sanhedrini mfanyeni kamanda wa kijeshi aelewe ni kwa nini apaswa kumleta chini kwenu kama kwamba mwakusudia kuhakikisha kwa usahihi zaidi mambo yanayomhusu. Lakini kabla hajafika karibu hakika sisi tutakuwa tayari kummaliza.”
16 Hata hivyo, mwana wa dada ya Paulo akasikia juu ya kuotea kwao, naye akaja na kuingia katika makao ya hao askari-jeshi akaripoti hilo kwa Paulo. 17 Basi Paulo akamwita kwake mmoja wa maofisa-jeshi na kusema: “Peleka mwanamume huyu kijana kwa kamanda wa kijeshi, kwa maana ana jambo fulani la kuripoti kwake.” 18 Kwa hiyo mtu huyu akamchukua na kumpeleka kwa kamanda wa kijeshi na kusema: “Mfungwa Paulo aliniita kwake na kuniomba nimlete mwanamume huyu kijana kwako, kwa kuwa ana jambo fulani la kukuambia.” 19 Kamanda wa kijeshi akampeleka kwa mkono kisha akajiondoa, akaanza kuulizia habari kwake kwa faragha: “Ni nini ulilo nalo la kuripoti kwangu?” 20 Akasema: “Wayahudi wamepatana kukuomba umshushe Paulo kwenye Sanhedrini kesho kama kwamba wanakusudia kujifunza jambo fulani sahihi zaidi juu yake. 21 Zaidi ya mambo yote, usiwaache wakushawishi, kwa maana wanaume wao zaidi ya arobaini wanamwotea, nao wamejifunga wenyewe kwa laana kutokula wala kunywa mpaka wawe wamemmaliza; nao sasa wako tayari, wakingojea ahadi kutoka kwako.” 22 Kwa hiyo huyo kamanda wa kijeshi akaacha huyo mwanamume kijana aende baada ya kumwagiza: “Usipayuke-payuke kwa yeyote kwamba umenielewesha mambo haya.”
23 Naye akawaita watu fulani wawili wa maofisa-jeshi na kusema: “Tayarisheni askari-jeshi mia mbili ili waende moja kwa moja hadi Kaisaria, pia wapanda-farasi sabini na watu mia mbili wachukua-mikuki, kwenye saa ya tatu ya usiku. 24 Pia, andaeni hayawani wachukua-mizigo yenye kulemea ili wampandishe Paulo na kumpeleka salama kwa Feliksi gavana.” 25 Naye akaandika barua ya namna hii:
26 Klaudio Lisiasi kwa mtukuzwa wake, Gavana Feliksi: Salamu! 27 Mwanamume huyu alikamatwa na Wayahudi na alikuwa karibu kumalizwa nao, lakini nikaja ghafula nikiwa pamoja na jeshi la askari na kumwokoa, kwa sababu nilipata kujua yeye ni Mroma. 28 Nami nikitaka kuhakikisha sababu waliyokuwa wakimshtaki, nikamleta ndani ya Sanhedrini yao. 29 Nilikuta ameshtakiwa juu ya maswali ya Sheria yao, lakini hajashtakiwa hata jambo moja la kustahili kifo au vifungo. 30 Lakini kwa sababu njama itakayofanywa dhidi ya huyu mwanamume imefunuliwa kwangu, ninamtuma kwako mara moja, na kuwaamuru washtaki waseme dhidi yake mbele yako.”
31 Kwa hiyo askari-jeshi hao wakamchukua Paulo kulingana na walivyoagizwa wakamleta wakati wa usiku hadi Antipatrisi. 32 Siku iliyofuata wakaruhusu wapanda-farasi waendelee pamoja naye, nao wakarudi kwenye makao ya askari-jeshi. 33 Hao wapanda-farasi wakaingia katika Kaisaria na kumkabidhi gavana hiyo barua na pia wakamtoa Paulo mbele yake. 34 Basi akaisoma na kuulizia habari alikuwa ametoka jimbo gani, akapata kujua hakika kwamba alikuwa ametoka Kilikia. 35 “Nitasikia kesi yako vilivyo,” akasema, “washtaki wako wawasilipo pia.” Naye akaamuru kwamba awekwe chini ya ulinzi katika ikulu ya praetori ya Herode.