Waroma
3 Basi, Myahudi ana ubora gani, au ni nini iliyo manufaa ya tohara? 2 Ni nyingi katika kila njia. Kwanza kabisa, kwa sababu wao walikabidhiwa matamko yaliyo matakatifu ya Mungu. 3 Basi, kisa ni nini? Ikiwa wengine hawakuonyesha imani, je, ukosefu wao wa imani labda utafanya uaminifu wa Mungu usiwe na matokeo? 4 Hilo lisitukie kamwe! Bali acheni Mungu apate kuonekana kuwa wa kweli, lakini kila binadamu apate kuonekana kuwa mwongo, kama vile imeandikwa: “Ili upate kuthibitishwa kuwa mwadilifu katika maneno yako na upate kushinda unapohukumiwa.” 5 Hata hivyo, ikiwa ukosefu wetu wa uadilifu watokeza wazi uadilifu wa Mungu, tutasema nini? Mungu hakosi kuwa mwenye haki afunguliapo hasira ya kisasi yake, sivyo? (Ninasema kama binadamu asemavyo.) 6 Hilo lisitukie kamwe! Kama sivyo, Mungu atauhukumuje ulimwengu?
7 Lakini ikiwa kwa sababu ya uwongo wangu kweli ya Mungu imefanywa kuwa yenye kutokeza zaidi kwa utukufu wake, kwa nini bado mimi pia ninahukumiwa kuwa mtenda-dhambi? 8 Na kwa nini si kusema, kama vile twashtakiwa isivyo kweli na kama vile watu fulani hutaarifu kwamba sisi husema: “Acheni tufanye mambo mabaya ili mambo mema yapate kuja”? Hukumu dhidi ya watu hao inapatana na haki.
9 Ni nini basi? Je, sisi tumo katika hali bora? Sivyo hata kidogo! Kwa maana hapo juu tumefanya shtaka kwamba Wayahudi na vilevile Wagiriki wako chini ya dhambi; 10 kama vile imeandikwa: “Hakuna mtu mwadilifu, hakuna hata mmoja; 11 hakuna yeyote aliye na ufahamu wowote wenye kina, hakuna yeyote amtafutaye Mungu. 12 Watu wote wamekengeuka, wote pamoja wamekuwa wasiofaa kitu; hakuna yeyote atendaye fadhili, hakuna hata mmoja.” 13 “Koo yao ni kaburi lililofunguliwa, wametumia udanganyi kwa ndimi zao.” “Sumu ya swila wadogo iko nyuma ya midomo yao.” 14 “Na kinywa chao kimejaa kulaani na usemi wenye uchungu.” 15 “Miguu yao yafanya kasi kumwaga damu.” 16 “Uangamizo na taabu zimo katika njia zao, 17 nao hawajaijua njia ya amani.” 18 “Hakuna kumhofu Mungu mbele ya macho yao.”
19 Sasa twajua kwamba mambo yote iyasemayo Sheria, hiyo huwaambia wale walio chini ya Sheria, ili kila kinywa kipate kukomeshwa na ulimwengu wote upate kuwa wastahili kupasishwa adhabu na Mungu. 20 Kwa hiyo kwa kazi za sheria hakuna mwili utakaotangazwa kuwa wenye uadilifu mbele yake, kwa maana ujuzi sahihi juu ya dhambi ni kwa njia ya sheria.
21 Lakini sasa bila sheria uadilifu wa Mungu umefanywa dhahiri, kama vile utolewavyo ushahidi na Sheria na Manabii; 22 ndiyo, uadilifu wa Mungu kupitia imani katika Yesu Kristo, kwa ajili ya wote wale walio na imani. Kwa maana hakuna tofauti. 23 Kwa maana wote wamefanya dhambi na hupungukiwa na utukufu wa Mungu, 24 nayo ni kama zawadi ya bure kwamba wao wanatangazwa kuwa waadilifu kwa fadhili yake isiyostahiliwa kupitia kuachiliwa kwa njia ya fidia iliyolipwa na Kristo Yesu. 25 Mungu alimtokeza kuwa toleo la kufunika kupitia imani katika damu yake. Hiyo ilikuwa kusudi aonyeshe wazi uadilifu wake mwenyewe, kwa sababu alikuwa akizisamehe dhambi zilizotokea wakati uliopita Mungu alipokuwa akitumia uvumilivu wenye subira; 26 ili kuonyesha wazi uadilifu wake mwenyewe katika majira haya yaliyopo, ili apate kuwa mwadilifu hata anapomtangaza kuwa mwadilifu mtu aliye na imani katika Yesu.
27 Basi, kuko wapi kujisifu? Kumefungiwa nje. Kupitia sheria gani? Ile ya kazi? La hasha, bali kupitia sheria ya imani. 28 Kwa maana twahesabu kwamba mtu hutangazwa kuwa mwadilifu kwa imani bila kazi za sheria. 29 Au je, yeye ndiye Mungu wa Wayahudi tu? Je, yeye si wa watu wa mataifa pia? Ndiyo, wa watu wa mataifa pia, 30 ikiwa kwa kweli Mungu ni mmoja, atakayetangaza watu waliotahiriwa kuwa waadilifu likiwa tokeo la imani na watu wasiotahiriwa kuwa waadilifu kwa njia ya imani yao. 31 Basi, je! twaibatilisha sheria kwa njia ya imani yetu? Hilo lisitukie kamwe! Kinyume cha hilo, sisi twaiimarisha sheria.