Waroma
4 Kwa kuwa iko hivyo, tutasema nini juu ya Abrahamu baba yetu wa zamani kulingana na mwili? 2 Kwa mfano, kama Abrahamu angetangazwa kuwa mwadilifu likiwa tokeo la kazi, angekuwa na sababu ya kujisifu; lakini si kwa Mungu. 3 Kwa maana andiko lasema nini? “Abrahamu alidhihirisha imani katika Yehova, na hilo likahesabiwa kwake kuwa uadilifu.” 4 Basi kwa mtu afanyaye kazi, malipo yahesabiwa, si yakiwa fadhili isiyostahiliwa, bali yakiwa deni. 5 Kwa upande mwingine, kwa mtu asiyefanya kazi bali awekaye imani katika yeye amtangazaye kuwa mwadilifu yule asiyemwogopa Mungu, imani yake yahesabiwa kuwa uadilifu. 6 Kama vile Daudi pia asemavyo juu ya furaha ya mtu ambaye Mungu humhesabia uadilifu bila kazi: 7 “Wenye furaha ni wale ambao vitendo vyao vya kuasi sheria vimesamehewa na ambao dhambi zao zimefunikwa; 8 mwenye furaha ni mtu ambaye Yehova hatahesabu dhambi yake kwa vyovyote.”
9 Basi, je, furaha hiyo huja juu ya watu waliotahiriwa au pia juu ya watu wasiotahiriwa? Kwa maana twasema: “Imani yake ilihesabiwa kwa Abrahamu kuwa uadilifu.” 10 Basi, ilihesabiwa chini ya hali gani? Alipokuwa katika tohara au katika kutotahiriwa? Si katika tohara, bali katika kutotahiriwa. 11 Naye alipokea ishara, yaani, tohara, kuwa muhuri wa uadilifu kwa imani aliyokuwa nayo alipokuwa katika hali yake ya kutotahiriwa, ili yeye apate kuwa baba ya wote wale walio na imani wakiwa katika kutotahiriwa, kusudi wahesabiwe uadilifu; 12 na baba ya uzao uliotahiriwa, si kwa wale tu washikamanao sana na tohara, bali pia kwa wale watembeao kwa utaratibu katika hatua za imani hiyo wakiwa katika hali ya kutotahiriwa ambayo baba yetu Abrahamu alikuwa nayo.
13 Kwa maana haikuwa kupitia sheria kwamba Abrahamu au mbegu yake akawa na ahadi kwamba awe mrithi wa ulimwengu, bali ilikuwa kupitia uadilifu kwa njia ya imani. 14 Kwa maana ikiwa wale ambao hushikamana sana na sheria ni warithi, imani imefanywa kuwa isiyofaa kitu na ahadi imebatilishwa. 15 Kwa kweli Sheria hutokeza hasira ya kisasi, lakini pasipo sheria, hapana pia mkiuko-sheria wowote.
16 Kwa ajili ya hilo ilikuwa kama tokeo la imani, ili ipate kuwa kulingana na fadhili isiyostahiliwa, kusudi ahadi iwe hakika kwa mbegu yake yote, si kwa ile tu ishikamanayo sana na Sheria, bali pia kwa ile ishikamanayo sana na imani ya Abrahamu. (Yeye ni baba yetu sote, 17 kama vile imeandikwa: “Nimekuweka wewe rasmi kuwa baba ya mataifa mengi.”) Hili lilikuwa mbele ya macho ya Yule ambaye katika yeye alikuwa na imani, naam, ya Mungu, afanyaye wafu kuwa hai na huita mambo yasiyokuwako kama kwamba yamekuwako. 18 Ajapopita hali ya kuwa na tumaini, bado kwa kutegemea tumaini alikuwa na imani, ili apate kuwa baba ya mataifa mengi kwa kupatana na yale yaliyokuwa yamesemwa: “Ndivyo mbegu yako itakavyokuwa.” 19 Na, ijapokuwa hakupata kudhoofika katika imani, alifikiria mwili wake mwenyewe, ukiwa sasa tayari umefishwa, kwa kuwa alikuwa mwenye umri wa karibu miaka mia moja, pia ufu wa tumbo la uzazi la Sara. 20 Lakini kwa sababu ya ahadi ya Mungu yeye hakusitasita kwa ukosefu wa imani, bali akawa mwenye nguvu nyingi kwa imani yake, akimpa Mungu utukufu 21 na akisadikishwa kikamili kwamba alilokuwa ameahidi alikuwa na uwezo pia wa kufanya. 22 Kwa sababu hiyo “ilihesabiwa kwake kuwa uadilifu.”
23 Hata hivyo, haikuandikwa kwa ajili yake tu kwamba “ilihesabiwa kwake,” 24 bali pia kwa ajili yetu ambao imekusudiwa kuhesabiwa, kwa sababu twamwamini yeye aliyemfufua Yesu Bwana wetu kutoka kwa wafu. 25 Yeye alitolewa kwa ajili ya makosa yetu na kufufuliwa kwa ajili ya kututangaza kuwa waadilifu.