Waroma
5 Basi, kwa kuwa sasa tumetangazwa kuwa waadilifu likiwa tokeo la imani, acheni tuonee shangwe amani pamoja na Mungu kupitia Bwana wetu Yesu Kristo, 2 ambaye kupitia yeye pia tumepata karibio letu kwa njia ya imani kuingia katika fadhili hii isiyostahiliwa ambayo katika hiyo sasa twasimama; na acheni tuchachawe, kwa kutegemea tumaini la utukufu wa Mungu. 3 Na si hilo tu, bali acheni tuchachawe tuwapo katika dhiki, kwa kuwa twajua kwamba dhiki hutokeza uvumilivu; 4 nao uvumilivu, hali yenye kukubaliwa; nayo hali yenye kukubaliwa, tumaini, 5 nalo tumaini haliongozi kwenye kukata tamaa; kwa sababu upendo wa Mungu umemwagwa ndani ya mioyo yetu kupitia roho takatifu, tuliyopewa.
6 Kwa maana, kwa kweli, tulipokuwa tungali bado dhaifu, Kristo alikufa wakati uliowekwa rasmi kwa ajili ya watu wasiomwogopa Mungu. 7 Kwa maana ni vigumu kwa yeyote kufa kwa ajili ya mtu mwadilifu; kwa kweli, kwa ajili ya mtu mwema, labda, mtu fulani hata atathubutu kufa. 8 Lakini Mungu apendekeza upendo wake mwenyewe kwetu kwa kuwa, tulipokuwa tungali watenda-dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu. 9 Kwa hiyo, ni zaidi sana kwa kuwa tumetangazwa kuwa waadilifu sasa kwa damu yake, kwamba tutaokolewa kutokana na hasira ya kisasi kupitia yeye. 10 Kwa maana, ikiwa tulipokuwa maadui, tulipata kuwa wenye kupatanishwa na Mungu kupitia kifo cha Mwana wake, ni zaidi sana sisi tutaokolewa kwa uhai wake, kwa kuwa sasa tumepata kuwa wenye kupatanishwa. 11 Na si hilo tu, bali pia tunachachawa katika Mungu kupitia Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kupitia yeye sasa tumepokea huo upatanisho.
12 Hiyo ndiyo sababu, kama vile kupitia mtu mmoja dhambi iliingia katika ulimwengu na kifo kupitia dhambi, na hivyo kifo kikasambaa kwa watu wote kwa sababu wote walikuwa wamefanya dhambi—. 13 Kwa maana hadi Sheria dhambi ilikuwa katika ulimwengu, lakini dhambi haihesabiwi dhidi ya yeyote wakati hakuna sheria. 14 Hata hivyo, kifo kilitawala kikiwa mfalme tangu Adamu hadi Musa, hata juu ya wale ambao hawakuwa wamefanya dhambi kwa ufanani wa mkiuko-sheria wa Adamu, afananaye na yeye aliyepaswa kuja.
15 Lakini sivyo ilivyo kwa ile zawadi kama ilivyokuwa kwa lile kosa. Kwa maana ikiwa kwa kosa la mtu mmoja wengi walikufa, fadhili isiyostahiliwa ya Mungu na zawadi yake ya bure ikiwa pamoja na fadhili isiyostahiliwa kupitia mtu mmoja Yesu Kristo ilizidi sana kwa wengi. 16 Pia, sivyo ilivyo kwa ile zawadi ya bure kama ilivyokuwa kwa njia ambayo mambo yalitendeka kupitia mtu mmoja aliyefanya dhambi. Kwa maana hukumu ilitokana na kosa moja katika hatia, lakini zawadi ilitokana na wingi wa makosa katika tangazo la uadilifu. 17 Kwa maana ikiwa kwa kosa la mtu mmoja kifo kilitawala kikiwa mfalme kupitia mmoja huyo, ni zaidi sana wale wapokeao wingi wa fadhili isiyostahiliwa na zawadi ya bure ya uadilifu watatawala wakiwa wafalme katika uhai kupitia mtu mmoja, Yesu Kristo.
18 Kwa hiyo, basi, kama vile kupitia kosa moja tokeo kwa watu wa namna zote lilikuwa ni hatia, hivyohivyo pia kupitia tendo moja la kutetewa kuwa haki tokeo kwa watu wa namna zote ni kutangazwa kwao kuwa waadilifu kwa ajili ya uhai. 19 Kwa maana kama vile kupitia kutotii kwa mtu mmoja wengi walifanywa watenda-dhambi, hivyohivyo pia kupitia utii wa mtu mmoja wengi watafanywa waadilifu. 20 Basi Sheria iliingia kando ili ukosaji upate kuzidi. Lakini mahali ambapo dhambi ilizidi, fadhili isiyostahiliwa ilizidi hata zaidi. 21 Kwa madhumuni gani? Kwamba, kama vile dhambi ilivyotawala ikiwa mfalme pamoja na kifo, hivyohivyo pia fadhili isiyostahiliwa ipate kutawala ikiwa mfalme kupitia uadilifu kwa tazamio la uhai udumuo milele kupitia Yesu Kristo Bwana wetu.