Waroma
6 Kwa sababu hiyo, tutasema nini? Je, tutaendelea katika dhambi, ili fadhili isiyostahiliwa ipate kuzidi? 2 Hilo lisitukie kamwe! Kwa kuwa tulikufa kuhusiana na dhambi, tutafulizaje kuishi tena katika hiyo? 3 Au je, hamjui kwamba sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika kifo chake? 4 Kwa hiyo tulizikwa pamoja naye kupitia ubatizo wetu katika kifo chake, ili, kama vile Kristo alivyofufuliwa kutoka kwa wafu kupitia utukufu wa Baba, hivyohivyo sisi pia twapaswa kujiendesha katika upya wa uhai. 5 Kwa maana ikiwa tumekuwa wenye kuungana pamoja naye katika ufanani wa kifo chake, hakika sisi pia tutaunganishwa pamoja naye katika ufanani wa ufufuo wake; 6 kwa sababu twajua kwamba utu wetu wa zamani ulitundikwa mtini pamoja naye, ili mwili wetu wenye dhambi upate kufanywa usiotenda, ili tusipate kuendelea tena kuwa watumwa wa dhambi. 7 Kwa maana yeye ambaye amekufa ameondolewa hatia ya dhambi yake.
8 Zaidi ya hayo, ikiwa tumekufa pamoja na Kristo, twaamini kwamba tutaishi pia pamoja naye. 9 Kwa maana twajua kwamba Kristo, kwa kuwa sasa amekwisha kufufuliwa kutoka kwa wafu, hafi tena; kifo si bwana-mkubwa juu yake tena. 10 Kwa maana kifo alichokufa, alikufa kuhusiana na dhambi mara moja kwa wakati wote; lakini uhai ambao yeye aishi, yeye huishi kuhusiana na Mungu. 11 Hivyohivyo nyinyi pia: jihesabuni nyinyi wenyewe kuwa wafu kwa kweli kuhusiana na dhambi lakini wenye kuishi kuhusiana na Mungu kwa njia ya Kristo Yesu.
12 Kwa hiyo msiache dhambi iendelee kutawala ikiwa mfalme katika miili yenu iwezayo kufa hivi kwamba mzitii tamaa zayo. 13 Wala msiendelee kutoa viungo vyenu kwa dhambi kuwa silaha za ukosefu wa uadilifu, bali jitoeni nyinyi wenyewe kwa Mungu kama walio hai kutoka kwa wafu, pia viungo vyenu kwa Mungu kuwa silaha za uadilifu. 14 Kwa maana ni lazima dhambi isiwe bwana-mkubwa juu yenu, kwa kuwa nyinyi hamko chini ya sheria bali chini ya fadhili isiyostahiliwa.
15 Basi lafuata nini? Je, tutafanya dhambi kwa sababu hatuko chini ya sheria bali chini ya fadhili isiyostahiliwa? Hilo lisitukie kamwe! 16 Je, hamjui kwamba ikiwa mnafuliza kujitoa nyinyi wenyewe kwa yeyote kuwa watumwa ili kumtii yeye, nyinyi ni watumwa wake kwa sababu mwamtii yeye, ama watumwa wa dhambi kwa tazamio la kifo ama wa utii kwa tazamio la uadilifu? 17 Lakini shukrani kwa Mungu kwamba mlikuwa watumwa wa dhambi lakini kutoka moyoni mkawa wenye kutii namna ile ya kufundisha mlikokabidhiwa kwayo. 18 Ndiyo, kwa kuwa mliwekwa huru kutoka katika dhambi, mlipata kuwa watumwa wa uadilifu. 19 Ninasema kwa maneno ya kibinadamu kwa sababu ya udhaifu wa mwili wenu: kwa maana kama vile mlivyotoa viungo vyenu kuwa watumwa wa ukosefu wa usafi na uasi-sheria kwa tazamio la uasi-sheria, basi sasa toeni viungo vyenu viwe watumwa kwa uadilifu kwa tazamio la utakatifu. 20 Kwa maana mlipokuwa watumwa wa dhambi, mlikuwa huru kwa habari ya uadilifu.
21 Basi, ni nini lililokuwa tunda ambalo mlikuwa na kawaida ya kuwa nalo wakati huo? Mambo ambayo sasa mwaaibikia. Kwa maana mwisho wa mambo hayo ni kifo. 22 Hata hivyo, sasa, kwa sababu mliwekwa huru kutoka katika dhambi lakini mkapata kuwa watumwa kwa Mungu, mnapata tunda lenu kwa njia ya utakatifu, na mwisho uhai udumuo milele. 23 Kwa maana mshahara ambao dhambi hulipa ni kifo, lakini zawadi ambayo Mungu hutoa ni uhai udumuo milele kwa njia ya Kristo Yesu Bwana wetu.