Waroma
7 Akina ndugu, je, yaweza kuwa kwamba nyinyi hamjui, (kwa maana ninasema kwa wale wajuao sheria,) kwamba Sheria ni bwana-mkubwa juu ya mtu kwa muda aishio? 2 Kwa mfano, mwanamke aliyeolewa amefungwa na sheria kwa mume wake wakati yuko hai; lakini mume wake akifa, yeye huondolewa katika sheria ya mume wake. 3 Hivyo, basi, wakati mume wake angali hai, yeye angeitwa mwanamke mzinzi kama angepata kuwa wa mwanamume mwingine. Lakini mume wake akifa, yeye yuko huru na sheria ya mume, hivi kwamba yeye si mwanamke mzinzi akipata kuwa mke wa mwanamume mwingine.
4 Hivyo, ndugu zangu, nyinyi pia mlifanywa wafu kwa Sheria kupitia mwili wa Kristo, ili nyinyi mpate kuwa wa mwingine, wa yeye aliyefufuliwa kutoka kwa wafu, ili tumzalie Mungu matunda. 5 Kwa maana tulipokuwa twapatana na mwili, harara zenye dhambi zilizosisimuliwa na Sheria zilikuwa zikifanya kazi katika viungo vyetu ili tutokezee kifo matunda. 6 Lakini sasa tumeondolewa katika Sheria, kwa sababu tumekufa kwa kile ambacho tulikuwa tumeshikwa nacho sana, ili tupate kuwa watumwa katika maana mpya kwa roho, wala si katika maana ya zamani kwa njia ya mfumo wa sheria iliyoandikwa.
7 Basi, tutasema nini? Je, Sheria ni dhambi? Hilo lisipate kuwa hivyo kamwe! Kwa kweli singalikuja kujua dhambi kama isingalikuwa kwa sababu ya Sheria; na, kwa kielelezo, mimi singalijua tamaa kama Sheria haingalisema: “Usitamani.” 8 Lakini dhambi, kwa kupokea kichocheo kupitia hiyo amri, ilifanyiza katika mimi kutamani kwa kila namna, kwa maana bila sheria dhambi ilikuwa imekufa. 9 Kwa kweli, wakati mmoja nilikuwa hai bila sheria; lakini amri ilipowasili, dhambi ilikuja kwenye uhai tena, lakini mimi nikafa. 10 Na amri iliyokuwa ya kuongoza kwenye uhai, niliiona hii kuwa ya kuongoza kwenye kifo. 11 Kwa maana dhambi, ikipokea kichocheo kupitia amri, ilinishawishi na kuniua kupitia yenyewe hiyo. 12 Kwa sababu hii, kwa upande wayo, Sheria ni takatifu, na amri ni takatifu na ya uadilifu na njema.
13 Basi, je, lililo jema lilipata kuwa kifo kwangu? Hilo lisitukie kamwe! Lakini dhambi ilipata kuwa hivyo, ili ipate kuonyeshwa kuwa dhambi yenye kunifanyizia kifo kupitia lile lililo jema; ili dhambi ipate kuwa yenye dhambi zaidi sana kupitia amri. 14 Kwa maana twajua kwamba Sheria ni ya kiroho; lakini mimi ni wa kimwili, niliyeuzwa chini ya dhambi. 15 Kwa maana lile nifanyalo silijui. Kwa maana lile nitakalo, hilo sizoei kulifanya; bali lile nichukialo ndilo nifanyalo. 16 Hata hivyo, ikiwa lile nisilotaka ndilo nifanyalo, nakubali kwamba Sheria ni bora. 17 Lakini sasa anayefanya hilo si mimi tena, bali ni dhambi ikaayo katika mimi. 18 Kwa maana najua kwamba katika mimi, yaani, katika mwili wangu, halikai jambo lolote jema; kwa maana uwezo wa kutaka upo pamoja nami, bali uwezo wa kufanya lililo bora haupo. 19 Kwa maana lile jema nitakalo silifanyi, bali lile baya nisilotaka ndilo nazoea kulifanya. 20 Basi, ikiwa lile nisilotaka ndilo nilifanyalo, anayelifanya hilo si mimi tena, bali ni dhambi inayokaa katika mimi.
21 Basi, mimi naona sheria hii katika kisa changu: kwamba nitakapo kulifanya lililo sawa, lililo baya lipo pamoja nami. 22 Kwa kweli napendezwa na sheria ya Mungu kulingana na mtu niliye kwa ndani, 23 lakini mimi naona katika viungo vyangu sheria nyingine ikifanya vita dhidi ya sheria ya akili yangu na kunichukua mateka kwa sheria ya dhambi iliyo katika viungo vyangu. 24 Mwenye taabu mimi! Ni nani ataniokoa kutoka katika mwili unaopatwa na kifo hiki? 25 Shukrani kwa Mungu kupitia Yesu Kristo Bwana wetu! Basi, kwa hiyo kwa akili yangu mimi mwenyewe ni mtumwa wa sheria ya Mungu, lakini kwa mwili wangu ni mtumwa wa sheria ya dhambi.