Waroma
8 Kwa hiyo wale walio katika muungano na Kristo Yesu hawana hatia. 2 Kwa maana sheria ya roho hiyo ambayo hutoa uhai katika muungano na Kristo Yesu imewaweka nyinyi huru kutoka katika sheria ya dhambi na kifo. 3 Kwa maana, kukiwa na hali ya kutoweza kwa upande wa Sheria, ilipokuwa dhaifu kupitia mwili, Mungu, kwa kumtuma Mwana wake mwenyewe akiwa ufanani wa mwili wenye dhambi na kuhusu dhambi, alihukumu dhambi katika mwili, 4 ili takwa la uadilifu la Sheria lipate kutimizwa katika sisi tutembeo, si kupatana na mwili, bali kupatana na roho. 5 Kwa maana wale wenye kupatana na mwili huweka akili zao juu ya mambo ya mwili, lakini wale wenye kupatana na roho juu ya mambo ya roho. 6 Kwa maana kuweka akili juu ya mwili humaanisha kifo, bali kuweka akili juu ya roho humaanisha uhai na amani; 7 kwa sababu kuweka akili juu ya mwili humaanisha uadui na Mungu, kwa maana mwili hauko chini ya ujitiisho kwa sheria ya Mungu, wala, kwa kweli, hauwezi kuwa. 8 Kwa hiyo wale walio katika upatano na mwili hawawezi kumpendeza Mungu.
9 Hata hivyo, nyinyi mko katika upatano, si na mwili, bali na roho, ikiwa kweli roho ya Mungu yakaa katika nyinyi. Lakini ikiwa yeyote hana roho ya Kristo, huyo si wake. 10 Lakini ikiwa Kristo yuko katika muungano na nyinyi, mwili kwa kweli ni mfu kwa sababu ya dhambi, bali roho ni uhai kwa sababu ya uadilifu. 11 Basi, ikiwa roho ya yule aliyemfufua Yesu kutoka kwa wafu yakaa katika nyinyi, yeye aliyemfufua Kristo Yesu kutoka kwa wafu atafanya pia miili yenu iwezayo kufa kuwa hai kupitia roho yake ikaayo katika nyinyi.
12 Basi, kwa hiyo akina ndugu, sisi ni wadeni, si kwa mwili ili tuishi kupatana na mwili; 13 kwa maana ikiwa mwaishi kupatana na mwili hakika nyinyi mtakufa; bali mkiua mazoea ya mwili kwa roho, mtaishi. 14 Kwa maana wote wenye kuongozwa na roho ya Mungu, hao ndio wana wa Mungu. 15 Kwa maana hamkupokea roho ya utumwa inayosababisha hofu tena, bali mlipokea roho ya tendo la kufanywa kuwa wana, roho ambayo kwayo twapaaza kilio: “Abba, Baba!” 16 Hiyo roho yenyewe hutoa ushahidi pamoja na roho yetu kwamba sisi ni watoto wa Mungu. 17 Basi, ikiwa sisi ni watoto, sisi pia ni warithi: warithi wa Mungu kwelikweli, lakini warithi-washirika pamoja na Kristo, mradi twateseka pamoja ili tupate pia kutukuzwa pamoja.
18 Kwa sababu hiyo nahesabu kwamba mateso ya majira yaliyopo si kitu kwa kulinganisha na utukufu utakaofunuliwa katika sisi. 19 Kwa maana taraja lenye hamu la viumbe linangoja kufunuliwa kwa wana wa Mungu. 20 Kwa maana viumbe vilitiishwa chini ya ubatili, si kwa mapenzi yavyo vyenyewe bali kupitia yeye aliyevitiisha hivyo, juu ya msingi wa tumaini 21 kwamba viumbe vyenyewe pia vitawekwa huru kutoka katika utumwa wa uharibifu na kuwa na uhuru wenye utukufu wa watoto wa Mungu. 22 Kwa maana twajua kwamba viumbe vyote vinafuliza kupiga kite pamoja na kuwa katika maumivu pamoja hadi sasa. 23 Si hilo tu, bali sisi wenyewe pia tulio na matunda ya kwanza, yaani, ile roho, ndiyo, sisi wenyewe twapiga kite katika sisi wenyewe, huku tukingoja kwa bidii tendo la kufanywa kuwa wana, kule kuachiliwa kutoka katika miili yetu kwa njia ya fidia. 24 Kwa maana tuliokolewa katika tumaini hili; lakini tumaini lionwalo si tumaini, kwa maana mtu aonapo kitu, je, hukitumainia? 25 Lakini tukitumainia kile tusichoona, twafuliza kukingojea kwa uvumilivu.
26 Kwa namna hiyo roho pia hujiunga kutoa msaada kwa ajili ya udhaifu wetu, kwa maana tatizo la tupasalo kusali kwa ajili yalo kama tuhitajivyo hatujui, lakini hiyo roho yenyewe hutuombea pamoja na upigaji-kite usiotamkwa. 27 Lakini yeye achunguzaye mioyo ajua ni nini limaanishwalo na roho, kwa sababu inaomba kupatana na Mungu kwa ajili ya watakatifu.
28 Basi twajua kwamba Mungu hufanya kazi zake zote zishirikiane pamoja kwa ajili ya mema ya wale wampendao Mungu, wale ambao ndio walioitwa kulingana na kusudi lake; 29 kwa sababu wale aliowapa utambuzi wake wa kwanza pia aliwaagiza pia kimbele kufanywa kiolezo kufuatia ule mfano wa Mwana wake, ili apate kuwa mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. 30 Zaidi ya hayo, wale aliowaagiza kimbele ndio wale aliowaita pia; na wale aliowaita ndio wale aliowatangaza kuwa waadilifu pia. Mwishowe wale aliowatangaza kuwa waadilifu ndio wale aliowatukuza pia.
31 Basi, tutasema nini kuhusu mambo haya? Ikiwa Mungu yuko upande wetu, nani atakayekuwa dhidi yetu? 32 Yeye ambaye hakumwachilia hata Mwana wake mwenyewe bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, kwa nini pia yeye pamoja naye hatatupa sisi kwa fadhili vitu vingine vyote? 33 Nani atakayeandikisha shtaka dhidi ya wachaguliwa wa Mungu? Mungu Ndiye awatangazaye kuwa waadilifu. 34 Nani yule atakayehukumu kuwa na hatia? Kristo Yesu ndiye aliyekufa, ndiyo, afadhali zaidi kusema ni yeye aliyefufuliwa kutoka kwa wafu, aliye katika mkono wa kuume wa Mungu, ambaye pia hutuombea.
35 Nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je, ni dhiki au taabu au mnyanyaso au njaa au uchi au hatari au upanga? 36 Kama vile imeandikwa: “Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, tumehesabiwa kama kondoo wa kuchinjwa.” 37 Kinyume chake, katika mambo yote haya tunatokea tukiwa wenye kushinda kabisa kupitia yeye aliyetupenda. 38 Kwa maana nasadiki kwamba wala kifo wala uhai wala malaika wala serikali wala mambo yaliyo hapa sasa wala mambo yatakayokuja wala nguvu 39 wala kimo wala kina wala kiumbe kingine chochote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.