Waroma
2 Kwa hiyo wewe huna sababu ya kujitetea, Ewe mtu, hata uwe nani, ukihukumu; kwa maana katika jambo lile ambalo wahukumu mwingine, wajihukumu kuwa mwenye hatia mwenyewe, kwa sababu wewe uhukumuye wazoea kufanya mambo hayohayo. 2 Sasa twajua kwamba, kupatana na kweli, hukumu ya Mungu iko dhidi ya wale wazoeao kufanya mambo ya namna hiyo.
3 Lakini je, wewe una wazo hili, Ewe mtu, kwamba utaponyoka hukumu ya Mungu wakati uhukumupo wale wazoeao kufanya mambo ya namna hiyo na bado wayafanya? 4 Au je, wewe wadharau utajiri wa fadhili yake na uvumilivu wenye subira na ustahimilivu, kwa sababu hujui kwamba sifa ya fadhili ya Mungu inajaribu kukuongoza wewe kwenye toba? 5 Lakini kulingana na ugumu wako na moyo wako usiotubu unajiwekea mwenyewe akiba ya hasira ya kisasi katika siku ya hasira ya kisasi na ya kufunuliwa kwa hukumu ya uadilifu ya Mungu. 6 Naye atamlipa kila mmoja kulingana na kazi zake: 7 uhai udumuo milele kwa wale wanaotafuta sana utukufu na heshima na kutofisidika kwa kuvumilia katika kazi iliyo njema; 8 hata hivyo, kwa wale wenye ugomvi na wale wasioitii kweli bali hutii ukosefu wa uadilifu kutakuwa na hasira ya kisasi na hasira, 9 dhiki na taabu, juu ya nafsi ya kila mtu afanyaye lililo baya, ya Myahudi kwanza na pia ya Mgiriki; 10 bali utukufu na heshima na amani kwa kila mtu afanyaye lililo jema, kwa Myahudi kwanza na pia kwa Mgiriki. 11 Kwa maana hakuna ubaguzi kwa Mungu.
12 Kwa mfano, wale wote waliofanya dhambi bila sheria wataangamia pia bila sheria; bali wale wote waliofanya dhambi chini ya sheria watahukumiwa kwa sheria. 13 Kwa maana wasikiaji wa sheria sio walio waadilifu mbele ya Mungu, bali watendaji wa sheria watatangazwa kuwa waadilifu. 14 Kwa maana wakati wowote ule watu wa mataifa wasio na sheria wafanyapo kwa asili mambo ya sheria, watu hawa, ijapokuwa hawana sheria, wao ni sheria kwao wenyewe. 15 Wao ndio walewale waonyeshao kiini cha sheria kuwa imeandikwa katika mioyo yao, huku dhamiri yao ikitoa ushahidi pamoja nao na, kati ya fikira zao wenyewe, wanashtakiwa au hata wanatetewa. 16 Hili litakuwa katika siku Mungu ahukumupo kupitia Kristo Yesu mambo ya siri ya wanadamu, kulingana na habari njema niitangazayo.
17 Sasa, ikiwa wewe ni Myahudi kwa jina na unategemea sheria na waona fahari katika Mungu, 18 nawe wajua mapenzi yake na wayakubali mambo yaliyo bora kabisa kwa sababu wafundishwa kwa mdomo kutokana na Sheria; 19 nawe umeshawishwa kwamba wewe ni kiongozi wa walio vipofu, nuru kwa wale walio katika giza, 20 msahihishaji wa wale wasio na akili, mwalimu wa vitoto, na mwenye muundo wa ujuzi na wa kweli katika Sheria— 21 hata hivyo, je, wewe unayemfundisha mtu mwingine, hujifundishi mwenyewe? Wewe, unayehubiri “Usiibe,” je, wewe huiba? 22 Wewe, unayesema “Usifanye uzinzi,” je, wewe hufanya uzinzi? Wewe, unayeonyesha chukio kubwa la sanamu, je, wewe hupokonya mahekalu? 23 Wewe, uonaye fahari katika sheria, je, kwa ukiukaji wako wa Sheria wewe huvunjia Mungu heshima? 24 Kwa maana “jina la Mungu linafanyiwa kufuru miongoni mwa mataifa kwa sababu ya nyinyi watu”; kama vile imeandikwa.
25 Kwa kweli, tohara ni yenye manufaa ikiwa wewe wazoea tu kufuata sheria; lakini ikiwa wewe ni mkiukaji wa sheria, tohara yako imekuwa kutotahiriwa. 26 Kwa hiyo, ikiwa mtu asiyetahiriwa hushika matakwa ya uadilifu ya Sheria, kutotahiriwa kwake kutahesabiwa kuwa tohara, sivyo? 27 Na mtu asiyetahiriwa aliye hivyo kwa asili, kwa kutekeleza Sheria, atakuhukumu wewe ambaye ukiwa na mfumo wayo wa sheria iliyoandikwa na ukiwa na tohara ni mkiukaji wa sheria. 28 Kwa maana yeye si Myahudi aliye hivyo kwa nje, wala tohara si ile ambayo ni ya nje juu ya mwili. 29 Bali yeye ni Myahudi aliye hivyo kwa ndani, na tohara yake ni ile ya moyo kwa roho, wala si kwa mfumo fulani wa sheria iliyoandikwa. Sifa ya huyo huja, si kutoka kwa wanadamu, bali kutoka kwa Mungu.