Waroma
Kwa Waroma
1 Paulo, mtumwa wa Yesu Kristo aliyeitwa kuwa mtume, aliyetengwa kwa ajili ya habari njema ya Mungu, 2 aliyoahidi kimbele kupitia manabii wake katika Maandiko matakatifu, 3 kuhusu Mwana wake, aliyechipuka kutokana na mbegu ya Daudi kulingana na mwili, 4 lakini ambaye akiwa na nguvu alitangazwa kuwa Mwana wa Mungu kulingana na ile roho ya utakatifu kwa njia ya ufufuo kutoka kwa wafu—ndiyo, Yesu Kristo Bwana wetu, 5 ambaye kupitia yeye tulipokea fadhili isiyostahiliwa na utume ili kupate kuwa na utii wa imani miongoni mwa mataifa yote kwa habari ya jina lake, 6 mataifa ambao miongoni mwao nyinyi pia ni wale walioitwa kuwa wa Yesu Kristo— 7 kwa wale wote walio katika Roma wakiwa wapendwa wa Mungu, walioitwa wawe watakatifu:
Na mwe na fadhili isiyostahiliwa na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.
8 Kwanza kabisa, namshukuru Mungu wangu kupitia Yesu Kristo kuhusu nyinyi nyote, kwa sababu imani yenu inaongewa kotekote ulimwenguni pote. 9 Kwa maana Mungu, nitoleaye utumishi mtakatifu kwa roho yangu kuhusiana na ile habari njema juu ya Mwana wake, ni shahidi wangu wa jinsi niwatajavyo sikuzote katika sala zangu bila kukoma, 10 nikiomba kwamba ikiwa kwa vyovyote yawezekana sasa mwishowe nipate kufanikiwa katika mapenzi ya Mungu ili nije kwenu. 11 Kwa maana nina hamu sana ya kuwaona nyinyi, ili nipate kuwapa baadhi ya zawadi ya kiroho kusudi mfanywe imara; 12 au, badala ya hivyo, kwamba kupate kuwa na badilishano la kitia-moyo miongoni mwenu, kwa kila mmoja kupitia imani ya mwingine, yenu na yangu pia.
13 Lakini, akina ndugu, sitaki mkose kujua kwamba nyakati nyingi nilikusudia kuja kwenu, lakini nimezuiwa hadi sasa, ili niweze kujipatia baadhi ya matunda miongoni mwenu pia kama vile miongoni mwa yale mataifa mengine. 14 Kwa Wagiriki na kwa Wabaribari pia, kwa wenye hekima na kwa wasio na akili pia mimi ni mdeni: 15 kwa hiyo kuna hamu upande wangu kuitangaza habari njema kwenu pia mlioko Roma. 16 Kwa maana siaibikii habari njema; kwa kweli, hiyo ni nguvu ya Mungu kwa ajili ya wokovu kwa kila mtu mwenye imani, kwa Myahudi kwanza na pia kwa Mgiriki; 17 kwa maana katika hiyo uadilifu wa Mungu unafunuliwa kwa sababu ya imani na kuelekea imani, kama vile imeandikwa: “Lakini mwadilifu—kwa njia ya imani ataishi.”
18 Kwa maana hasira ya kisasi ya Mungu inafunuliwa kutoka mbinguni dhidi ya ukosefu wote wa kumwogopa Mungu na ukosefu wa uadilifu wa watu wanaoikandamiza kweli katika njia isiyo ya uadilifu, 19 kwa sababu lile liwezalo kujulikana juu ya Mungu ni dhahiri miongoni mwao, kwa maana Mungu alilifanya dhahiri kwao. 20 Kwa maana sifa zake zisizoonekana zaonwa waziwazi tangu uumbaji wa ulimwengu na kuendelea, kwa sababu zafahamiwa kwa vitu vilivyofanywa, hata nguvu zake za milele na Uungu, hivi kwamba hawana sababu ya kujitetea; 21 kwa sababu, ijapokuwa walimjua Mungu, hawakumtukuza yeye kama Mungu wala hawakumshukuru, bali wakawa wenye akili haba katika mawazowazo yao na moyo wao usio na akili ukawa wenye giza. 22 Ijapokuwa walisisitiza kuwa ni wenye hekima, wakawa wapumbavu 23 na kugeuza utukufu wa Mungu asiyefisidika kuwa kitu kama sanamu ya mtu afisidikaye na ya ndege na viumbe vyenye miguu minne na vitambaazi.
24 Kwa hiyo Mungu, kwa kupatana na tamaa za mioyo yao, aliwaacha kwenye ukosefu wa usafi, ili miili yao ipate kuvunjiwa heshima miongoni mwao, 25 hata wale walioibadili kweli ya Mungu kwa uwongo nao waliheshimu mno na kutoa utumishi mtakatifu kwa kiumbe badala ya Yeye aliyeumba, ambaye abarikiwa milele. Ameni. 26 Hiyo ndiyo sababu Mungu aliwaacha kwenye hamu za ngono yenye kufedhehesha, kwa maana watu wao wa kike walibadili utumizi wa kiasili wa wao wenyewe kuwa ule ulio kinyume cha asili; 27 na hivyohivyo pia hata watu wa kiume waliacha utumizi wa kiasili wa aliye wa kike na kuwakiana tamaa kali katika uchu wao kuelekea mtu na mwenzake, watu wa kiume kwa watu wa kiume, wakifanya yaliyo yenye aibu na kupokea katika wao wenyewe malipo kamili, yaliyostahili kosa lao.
28 Na kama vile hawakukubali kuwa na Mungu katika ujuzi sahihi, Mungu aliwaacha katika hali ya kiakili iliyokataliwa, ili wafanye mambo yasiyofaa, 29 wakiwa wamejawa na ukosefu wote wa uadilifu, uovu, tamaa, ubaya, wakiwa wamejaa husuda, uuaji-kimakusudi, zogo, udanganyi, mwelekeo wenye nia ya kudhuru, wakiwa wanong’onezi, 30 wasengenyaji, wachukiaji Mungu, wafidhuli, wenye kiburi, wenye kujitanguliza, wabuni wa mambo mabaya, wasiotii wazazi, 31 wasio na uelewevu, wasio wa kweli katika mapatano, wasio na shauku ya asili, wasio na rehema. 32 Ijapokuwa hawa wajua vema kabisa agizo la uadilifu la Mungu, kwamba wale wanaozoea kufanya mambo ya namna hiyo wanastahili kifo, si kwamba tu wao hufuliza kuyafanya bali pia hukubaliana na wale wanaozoea kuyafanya.