1 Wakorintho
12 Sasa kuhusu zawadi za kiroho, akina ndugu, sitaki nyinyi mwe wasio na ujuzi. 2 Mwajua kwamba mlipokuwa watu wa mataifa, mlikuwa mkiongozwa kwenye zile sanamu zisizo na sauti kama vile mlivyotukia kuongozwa. 3 Kwa hiyo ningetaka nyinyi mjue kwamba hakuna mtu anaposema kwa roho ya Mungu asemaye: “Yesu ni mwenye kulaaniwa!” na hakuna mtu awezaye kusema: “Yesu ni Bwana!” ila kwa roho takatifu.
4 Basi kuna zawadi za namna namna, lakini kuna roho ileile; 5 na kuna huduma za namna namna, na bado kuna Bwana yuleyule; 6 na kuna utendaji wa namna namna, na bado ni Mungu yuleyule afanyaye utendaji wote katika watu wote. 7 Lakini kila mmoja hupewa udhihirisho wa roho kwa kusudi lenye manufaa. 8 Kwa kielelezo, mmoja hupewa usemi wa hekima kupitia ile roho, mwingine usemi wa ujuzi kulingana na roho ileile, 9 mwingine imani kwa roho ileile, mwingine zawadi za maponyo kwa roho moja hiyo, 10 mwingine bado utendaji wa kazi zenye nguvu, mwingine kutoa unabii, mwingine ufahamu wa matamko yaliyopuliziwa, mwingine lugha tofauti, na mwingine fasiri ya lugha. 11 Lakini kazi hizi zote roho ile moja tena ileile ndiyo huzifanya, ikigawanyia kila mmoja peke yake kama vile ipendavyo.
12 Kwa maana kama vile mwili ni mmoja lakini una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili huo, ijapokuwa ni vingi, ni mwili mmoja, ndivyo pia alivyo Kristo. 13 Kwa maana kwa kweli kwa roho moja sote tulibatizwa katika mwili mmoja, kama ni Wayahudi au Wagiriki, kama ni watumwa au walio huru, nasi sote tulifanywa kunywa roho moja.
14 Kwa maana mwili, kwa kweli, si kiungo kimoja, bali vingi. 15 Ikiwa mguu ungesema: “Kwa sababu mimi si mkono, mimi si sehemu ya mwili,” hauwi si sehemu ya mwili kwa sababu hiyo. 16 Na ikiwa sikio lingesema: “Kwa sababu mimi si jicho, mimi si sehemu ya mwili,” haliwi si sehemu ya mwili kwa sababu hiyo. 17 Kama mwili wote ungekuwa jicho, hisi ya kusikia ingekuwa wapi? Kama huo wote ungekuwa kusikia, kunusa kungekuwa wapi? 18 Lakini sasa Mungu ameviweka viungo katika mwili, kila kimoja chavyo, kama vile alivyopendezwa.
19 Kama vyote vingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi? 20 Lakini sasa hivyo ni viungo vingi, lakini mwili mmoja. 21 Jicho haliwezi kuuambia mkono: “Sikuhitaji wewe”; au, tena, kichwa hakiwezi kuambia miguu: “Siwahitaji nyinyi.” 22 Lakini badala yake ni kwamba vile viungo vya mwili vionekanavyo kuwa dhaifu zaidi ni vya lazima, 23 na zile sehemu za mwili ambazo twafikiri zaheshimika kidogo, hizo twazizingira kwa heshima nyingi zaidi, na kwa hiyo sehemu zetu zisizoonekana kuwa zenye kuvutia zina upendezi mwingi zaidi, 24 lakini sehemu zetu zenye upendezi hazihitaji kitu chochote. Hata hivyo, Mungu aliuungamanisha mwili, akiipa heshima iliyo nyingi zaidi sehemu iliyokuwa na upungufu, 25 ili kusiwe na mgawanyiko katika mwili, bali viungo vyao viwe na utunzaji uleule kimoja na chenzake. 26 Na kiungo kimoja kikiteseka, viungo vingine vyote huteseka pamoja nacho; au kiungo kikitukuzwa, viungo vingine vyote hushangilia pamoja nacho.
27 Basi nyinyi ni mwili wa Kristo, na viungo kimoja-kimoja. 28 Na Mungu amewaweka watu fulani mmoja-mmoja katika kutaniko, kwanza, mitume; pili, manabii; tatu, walimu, kisha kazi zenye nguvu; kisha zawadi za maponyo; utumishi mbalimbali wenye msaada, uwezo mbalimbali wa kuelekeza, lugha tofauti. 29 Si wote walio mitume, ndivyo? Si wote walio manabii, ndivyo? Si wote walio walimu, ndivyo? Si wote wafanyao kazi zenye nguvu, ndivyo? 30 Si wote walio na zawadi za maponyo, ndivyo? Si wote wasemao kwa lugha, ndivyo? Si wote walio watafsiri, ndivyo? 31 Lakini fulizeni kutafuta kwa bidii zawadi zilizo kubwa zaidi. Na bado nawaonyesha nyinyi njia izidiyo.