1 Wakorintho
13 Nikisema kwa lugha za wanadamu na za malaika lakini sina upendo, nimekuwa kipande cha shaba-nyeupe inayovuma au toazi lenye kulia. 2 Na ikiwa nina zawadi ya kutoa unabii nami nazijua sana siri takatifu zote na ujuzi wote, na ikiwa nina imani yote ili kung’oa na kuhamisha milima, lakini sina upendo, mimi si kitu. 3 Nami nikitoa mali zangu zote kulisha wengine, nami nikiutoa mwili wangu, ili nipate kujisifu, lakini sina upendo, sifaidiki hata kidogo.
4 Upendo ni wenye ustahimilivu na wenye fadhili. Upendo hauna wivu, haujigambi, haujitutumui, 5 haujiendeshi bila adabu, hautafuti masilahi yao wenyewe, haupati kuwa wenye kuchokozeka. Hauweki hesabu ya ubaya. 6 Haushangilii ukosefu wa uadilifu, bali hushangilia pamoja na kweli. 7 Huhimili mambo yote, huamini mambo yote, hutumaini mambo yote, huvumilia mambo yote.
8 Upendo haushindwi kamwe. Lakini kama kuna zawadi za kutoa unabii, zitaondolewa mbali; kama kuna lugha, zitaacha kuwako; kama kuna ujuzi, utaondolewa mbali. 9 Kwa maana tuna ujuzi wa sehemu tu nasi twatoa unabii kwa sehemu tu; 10 lakini wakati kile kilicho kamili kiwasilipo, kile kilicho cha sehemu tu kitaondolewa mbali. 11 Nilipokuwa kitoto, nilikuwa nikisema kama kitoto, nikifikiri kama kitoto, nikiwazawaza kama kitoto; lakini kwa kuwa sasa nimekuwa mtu mzima, nimeziondolea mbali tabia za kitoto. 12 Kwa maana wakati wa sasa twaona katika njia isiyo ya waziwazi kupitia kioo cha madini, lakini wakati huo itakuwa uso kwa uso. Wakati wa sasa najua kwa sehemu tu, lakini wakati huo nitajua kwa usahihi kama vile nijulikanavyo kwa usahihi. 13 Hata hivyo, sasa kwabaki imani, tumaini, upendo, matatu haya; lakini lililo kubwa zaidi sana kati ya haya ni upendo.