1 Wakorintho
14 Fuatieni upendo, na bado fulizeni kwa bidii kuzitafuta sana zawadi za kiroho, lakini afadhali kwamba mpate kutoa unabii. 2 Kwa maana yeye asemaye kwa lugha husema, si na wanadamu, bali na Mungu, kwa maana hakuna asikilizaye, bali kwa roho yeye husema siri zilizo takatifu. 3 Hata hivyo, yeye atoaye unabii hujenga na kutia moyo na kufariji watu kwa usemi wake. 4 Yeye asemaye kwa lugha hujijenga mwenyewe, lakini yeye atoaye unabii hujenga kutaniko. 5 Sasa ningependa nyinyi nyote mseme kwa lugha, lakini napendelea zaidi kwamba mtoe unabii. Kwa kweli, yeye atoaye unabii ni mkubwa zaidi kuliko yeye asemaye kwa lugha, isipokuwa, kwa kweli, yeye atafsiri, ili kutaniko lipate kujengwa. 6 Lakini wakati huu, akina ndugu, ikiwa ningekuja nikisema nanyi kwa lugha, ningewafaidi nini isipokuwa kama ningesema nanyi ama kwa ufunuo au kwa ujuzi au kwa unabii au kwa fundisho fulani?
7 Kama ilivyo, vitu visivyo na uhai hutoa mvumo, kama ni filimbi au kinubi; kisipofanya tofauti baina ya sauti za muziki, itajulikanaje ni nini kinachopigwa kwa filimbi au kwa kinubi? 8 Kwa maana kwa kweli, tarumbeta ikivuma wito usio dhahiri, nani atajitayarisha kwa ajili ya pigano? 9 Katika njia hiyohiyo pia, nyinyi msipotamka usemi wenye kueleweka kwa urahisi kupitia hiyo lugha, linalosemwa litajulikanaje? Kwa kweli, mtakuwa mkisema hewani tu. 10 Huenda ikawa kwamba kuna aina nyingi sana za mivumo ya usemi katika ulimwengu, na bado hakuna aina isiyo na maana. 11 Basi, ikiwa sielewi kani ya mvumo wa usemi, nitakuwa mtoka-ugenini kwa yeye anayesema, na kwangu yule anayesema atakuwa mtoka-ugenini. 12 Ndivyo pia nyinyi wenyewe, kwa kuwa mwatamani kwa bidii zawadi za roho, tafuteni kuzidi katika hizo kwa ajili ya kulijenga kutaniko.
13 Kwa hiyo acheni yeye asemaye katika lugha na asali ili apate kutafsiri. 14 Kwa maana ikiwa ninasali katika lugha, ni zawadi ya roho yangu inayosali, lakini akili yangu ni isiyozaa matunda. 15 Basi, nini lifanywe? Hakika nitasali kwa zawadi ya roho, lakini hakika pia nitasali kwa akili yangu. Hakika nitaimba sifa kwa zawadi ya roho, lakini hakika pia nitaimba sifa kwa akili yangu. 16 Kama sivyo, ukitoa sifa kwa zawadi ya roho, huyo mtu aliyekalia kiti cha mtu wa kawaida atasemaje “Ameni” kwa utoaji wako wa shukrani, kwa kuwa hajui lile unalosema? 17 Kweli, wewe watoa shukrani kwa njia bora, lakini yule mtu mwingine hawi akijengwa. 18 Mimi namshukuru Mungu, nasema kwa lugha zaidi kuliko nyinyi nyote. 19 Hata hivyo, katika kutaniko ingekuwa afadhali niseme maneno matano kwa akili yangu, ili nipate pia kufundisha wengine kwa mdomo, kuliko maneno elfu kumi katika lugha.
20 Akina ndugu, msiwe vitoto katika nguvu za kuelewa, lakini iweni watoto wachanga sana kuhusu ubaya; hata hivyo iweni watu wazima katika nguvu za kuelewa. 21 Katika Sheria imeandikwa: “‘Kwa lugha za watoka-ugenini na kwa midomo ya watu wasiojulikana hakika nitasema na watu hawa, na bado hata wakati huo hawatanisikiliza,’ asema Yehova.” 22 Kwa sababu hiyo lugha zipo kwa ajili ya ishara, si kwa waamini, bali kwa wasio waamini, lakini kutoa unabii kupo, si kwa ajili ya wasio waamini, bali kwa ajili ya waamini. 23 Kwa hiyo, kutaniko lote likija pamoja mahali pamoja nao wote wasema kwa lugha, lakini watu wa kawaida au wasio waamini waingia, je, hawatasema kwamba nyinyi ni wenye kichaa? 24 Lakini ikiwa nyinyi nyote mnatoa unabii na mtu yeyote asiye mwamini au mtu wa kawaida aingia, yeye hukaripiwa nao wote, huchunguzwa sana na wote; 25 siri za moyo wake huwa dhahiri, hivi kwamba ataanguka kifudifudi na kumwabudu Mungu, akitangaza: “Mungu kwa kweli yumo miongoni mwenu.”
26 Basi, nini lifanywe akina ndugu? Mjapo pamoja, mmoja ana zaburi, mwingine ana fundisho, mwingine ana ufunuo, mwingine ana lugha, mwingine ana fasiri. Acheni mambo yote yatukie kwa ajili ya kujenga. 27 Na mtu akisema katika lugha, acheni mpaka uwekwe ziwe mbili au tatu ikiwa ni nyingi zaidi sana, na kwa zamu; na acheni mtu fulani atafsiri. 28 Lakini ikiwa hakuna mtafsiri, acheni afulize kukaa kimya katika kutaniko na aseme kwake mwenyewe na kwa Mungu. 29 Zaidi, acheni manabii wawili au watatu waseme, na acheni wale wengine waifahamu maana. 30 Lakini ikiwa kuna ufunuo kwa mwingine wakati ameketi hapo, acheni yule wa kwanza afulize kukaa kimya. 31 Kwa maana nyote mwaweza kutoa unabii mmoja-mmoja, ili wote wapate kujifunza na wote watiwe moyo. 32 Na zawadi za roho ya manabii zapasa kudhibitiwa na manabii. 33 Kwa maana Mungu ni Mungu, si wa kukosa utaratibu, bali wa amani.
Kama ilivyo katika makutaniko yote ya watakatifu, 34 acheni wanawake wafulize kukaa kimya katika makutaniko, kwa maana hairuhusiwi kwao kusema, bali acheni wawe katika ujitiisho, kama Sheria isemavyo. 35 Basi, ikiwa wao wataka kujifunza jambo fulani, acheni wawaulize waume zao wenyewe nyumbani, kwa maana ni jambo lenye fedheha mwanamke kusema katika kutaniko.
36 Ama je, ilikuwa kutoka kwenu kwamba neno la Mungu lilikuja kutokea, au je, ilikuwa ni hadi kwenu tu lilifika?
37 Ikiwa yeyote afikiri yeye ni nabii au amepewa zawadi ya roho, acheni yeye akiri mambo ninayowaandikia nyinyi, kwa sababu hayo ni amri ya Bwana. 38 Lakini ikiwa yeyote ni mtu asiye na ujuzi, yeye huendelea kuwa asiye na ujuzi. 39 Kwa sababu hiyo, ndugu zangu, fulizeni kwa bidii kutafuta sana kule kutoa unabii, na bado msikataze kusema kwa lugha. 40 Lakini acheni mambo yote yatukie kwa adabu na kwa mpango.