1 Wakorintho
15 Sasa nawajulisha nyinyi, akina ndugu, habari njema niliyowatangazia, mliyoipokea pia, ambayo katika hiyo mwasimama pia, 2 ambayo kupitia hiyo nyinyi pia mnaokolewa, kwa usemi ambao kwa huo niliwatangazia nyinyi habari njema, ikiwa mnaishika sana, isipokuwa, kwa kweli, mwe mlipata kuwa waamini bila kusudi lolote.
3 Kwa maana niliwapa nyinyi, miongoni mwa mambo ya kwanza, lile nililolipokea pia, kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu kulingana na Maandiko; 4 na kwamba alizikwa, ndiyo, kwamba amefufuliwa siku ya tatu kulingana na Maandiko; 5 na kwamba alionekana kwa Kefa, kisha kwa wale kumi na wawili. 6 Baada ya hilo alionekana kwa zaidi ya ndugu mia tano kwa wakati mmoja, ambao walio wengi kati yao wabaki hadi wakati wa sasa, lakini baadhi yao wamelala usingizi katika kifo. 7 Baada ya hilo alionekana kwa Yakobo, kisha kwa mitume wote; 8 lakini mwisho wa wote alionekana pia kwangu kama kwamba kwa mmoja aliyezaliwa kabla ya wakati wake.
9 Kwa maana mimi ni mdogo zaidi sana kati ya wale mitume, nami sistahili kuitwa mtume, kwa sababu nililinyanyasa kutaniko la Mungu. 10 Lakini kwa fadhili isiyostahiliwa ya Mungu mimi niko kile nilicho. Na fadhili yake isiyostahiliwa iliyonielekea mimi haikuthibitika kuwa bure, bali nilifanya kazi ya jasho kwa kuwazidi wote, lakini si mimi bali ni fadhili isiyostahiliwa ya Mungu iliyo pamoja nami. 11 Hata hivyo, kama ni mimi au wao, ndivyo sisi tunavyohubiri na ndivyo nyinyi mmeamini.
12 Sasa ikiwa Kristo anahubiriwa kwamba amefufuliwa kutoka kwa wafu, ni jinsi gani wengine miongoni mwenu husema hakuna ufufuo wa wafu? 13 Ikiwa, kwa kweli, hakuna ufufuo wa wafu, wala Kristo hajafufuliwa. 14 Lakini ikiwa Kristo hajafufuliwa, kuhubiri kwetu ni bure hakika, na imani yetu ni bure. 15 Zaidi ya hayo, twaonekana pia kuwa mashahidi wasio wa kweli wa Mungu, kwa sababu tumetoa ushahidi dhidi ya Mungu kwamba yeye alimfufua Kristo, lakini ambaye hakumfufua ikiwa kwa kweli wafu hawatafufuliwa. 16 Kwa maana ikiwa wafu hawapaswi kufufuliwa, wala Kristo hajafufuliwa. 17 Zaidi, ikiwa Kristo hajafufuliwa, imani yenu haifai kitu; nyinyi bado mumo katika dhambi zenu. 18 Kwa kweli, pia, wale waliolala usingizi katika kifo katika muungano na Kristo waliangamia. 19 Ikiwa ni katika maisha haya tu tumetumaini Kristo, sisi ndio wa kusikitikiwa zaidi sana kati ya watu wote.
20 Hata hivyo, sasa Kristo amefufuliwa kutoka kwa wafu, matunda ya kwanza kati ya wale ambao wamelala usingizi katika kifo. 21 Kwa maana kwa kuwa kifo ni kupitia mwanadamu, ufufuo wa wafu pia ni kupitia mwanadamu. 22 Kwa maana kama vile katika Adamu wote wanakufa, ndivyo pia katika Kristo wote watafanywa kuwa hai. 23 Lakini kila mmoja katika daraja lake mwenyewe: Kristo aliye matunda ya kwanza, baadaye wale walio wa Kristo wakati wa kuwapo kwake. 24 Halafu, mwisho, wakati amkabidhipo ufalme Mungu wake aliye Baba, wakati akiwa amefanya serikali yote na mamlaka yote na nguvu kuwa si kitu. 25 Kwa maana ni lazima yeye atawale akiwa mfalme mpaka Mungu awe ameweka maadui wote chini ya miguu yake. 26 Kikiwa ni adui wa mwisho, kifo kitafanywa kuwa si kitu. 27 Kwa maana Mungu “alitiisha vitu vyote chini ya miguu yake.” Lakini wakati asemapo kwamba ‘vitu vyote vimetiishwa,’ ni dhahiri kwamba iko hivyo isipokuwa kwa yule aliyetiisha vitu vyote kwake. 28 Lakini vitu vyote vitakapokuwa vimetiishwa kwake, ndipo Mwana mwenyewe atakapojitiisha pia kwa Yule aliyetiisha vitu vyote kwake, ili Mungu apate kuwa vitu vyote kwa kila mtu.
29 Kama sivyo, watafanya nini wao wanaobatizwa kwa kusudi la kuwa wafu? Ikiwa wafu hawapaswi kufufuliwa hata kidogo, kwa nini pia wanabatizwa kwa kusudi la kuwa hivyo? 30 Kwa nini sisi pia tumo hatarini kila saa? 31 Kila siku nakabili kifo. Hili nathibitisha kwa mchachawo nilio nao juu yenu, akina ndugu, katika Kristo Yesu Bwana wetu. 32 Ikiwa, kama wanadamu, nimepigana na mahayawani-mwitu katika Efeso, hiyo ina faida gani kwangu? Ikiwa wafu hawapaswi kufufuliwa, “acheni tule na tunywe, kwa maana kesho tutapaswa kufa.” 33 Msiongozwe vibaya. Mashirika mabaya huharibu mazoea yenye mafaa. 34 Amkeni mwe na utimamu wa akili katika njia ya uadilifu na msizoee dhambi, kwa maana wengine hawana ujuzi juu ya Mungu. Ninasema ili kuwasukuma mwone aibu.
35 Hata hivyo, mtu fulani atasema: “Wafu watafufuliwaje? Ndiyo, wanakuja wakiwa na mwili wa namna gani?” 36 Wewe mtu asiye na akili! Kile upandacho hakifanywi kuwa hai isipokuwa kwanza kife; 37 na kwa habari ya kile upandacho, wapanda, si mwili utakaositawi, bali punje tupu, huenda ikawa, ya ngano au yoyote moja kati ya zile nyingine; 38 lakini Mungu huipa mwili kama vile imempendeza, na kwa kila moja ya hizo mbegu mwili wayo yenyewe. 39 Si mwili wote ulio mwili uleule, bali kuna mmoja wa wanadamu, na kuna mwili mwingine wa mifugo, na mwili mwingine wa ndege, na mwingine wa samaki. 40 Na kuna miili ya kimbingu, na miili ya kidunia; lakini utukufu wa miili ya kimbingu ni wa namna moja, na ule wa miili ya kidunia ni wa namna tofauti. 41 Utukufu wa jua ni wa namna moja, na utukufu wa mwezi ni mwingine, na utukufu wazo nyota ni mwingine; kwa kweli, nyota hutofautiana na nyota kwa utukufu.
42 Ndivyo pia ulivyo ufufuo wa wafu. Hupandwa katika uharibifu, hufufuliwa katika kutoharibika. 43 Hupandwa katika fedheha, hufufuliwa katika utukufu. Hupandwa katika udhaifu, hufufuliwa katika nguvu. 44 Hupandwa ukiwa mwili wa nyama, hufufuliwa ukiwa mwili wa kiroho. Ikiwa kuna mwili wa nyama, kuna wa kiroho pia. 45 Hata imeandikwa hivi: “Mtu wa kwanza Adamu akawa nafsi hai.” Adamu wa mwisho akawa roho ipayo uhai. 46 Hata hivyo, wa kwanza si ule ulio wa kiroho, bali ni ule ulio wa nyama, baadaye ule ulio wa kiroho. 47 Mtu wa kwanza ni wa kutoka duniani na amefanywa kwa mavumbi; mtu wa pili ni wa kutoka mbinguni. 48 Kama alivyo yule aliyefanywa kwa mavumbi, ndivyo walivyo wale waliofanywa kwa mavumbi pia; na kama alivyo yule wa kimbingu, ndivyo walivyo wale wa kimbingu pia. 49 Na kama vile tumeuchukua mfano wa yeye aliyefanywa kwa mavumbi, tutauchukua pia mfano wa yule wa kimbingu.
50 Hata hivyo, hili nasema, akina ndugu, kwamba nyama na damu haviwezi kurithi ufalme wa Mungu, wala uharibifu haurithi kutoharibika. 51 Tazama! Nawaambia nyinyi siri takatifu: Hatutalala usingizi katika kifo sisi sote, bali sisi sote tutabadilishwa, 52 kwa dakika, katika kupepeseka kwa jicho, wakati wa tarumbeta ya mwisho. Kwa maana hiyo tarumbeta itavuma, na wafu watafufuliwa wakiwa wasioharibika, nasi tutabadilishwa. 53 Kwa maana huu ulio wa kuharibika lazima uvae kutoharibika, na huu uwezao kufa lazima uvae hali ya kutokufa. 54 Lakini wakati huu ulio wenye kuharibika uvaapo kutoharibika na huu uwezao kufa uvaapo hali ya kutokufa, ndipo usemi utakapotukia ambao umeandikwa: “Kifo kimemezwa milele.” 55 “Kifo, ushindi wako uko wapi? Kifo, kichomeo chako kiko wapi?” 56 Kichomeo chenye kutokeza kifo ni dhambi, lakini nguvu ya dhambi ni Sheria. 57 Lakini shukrani kwa Mungu, kwa maana yeye hutupa sisi ushindi kupitia Bwana wetu Yesu Kristo!
58 Kwa sababu hiyo, ndugu zangu wapendwa, iweni imara, wasioondoleka, sikuzote mkiwa na mengi ya kufanya katika kazi ya Bwana, mkijua kwamba kazi yenu ya jasho si bure kuhusiana na Bwana.