1 Wakorintho
11 Iweni waigaji wangu, kama vile mimi nilivyo mwigaji wa Kristo.
2 Sasa nawasifu nyinyi kwa sababu katika mambo yote mwanikumbuka na mnayashika sana mapokeo kama vile nilivyowapa nyinyi. 3 Lakini nataka mjue kwamba kichwa cha kila mwanamume ni Kristo; nacho kichwa cha mwanamke ni mwanamume; nacho kichwa cha Kristo ni Mungu. 4 Kila mwanamume ambaye husali au hutoa unabii akiwa na kitu juu ya kichwa chake huaibisha kichwa chake; 5 lakini kila mwanamke ambaye husali au hutoa unabii kichwa chake kikiwa hakijafunikwa huaibisha kichwa chake, kwa maana ni mamoja na kama angekuwa mwanamke mwenye kichwa kilichonyolewa. 6 Kwa maana ikiwa mwanamke hajifuniki mwenyewe, acheni akatwe nywele pia; lakini ikiwa ni jambo lenye fedheha mwanamke kukatwa nywele au kunyolewa, acheni afunikwe.
7 Kwa maana mwanamume hapaswi kufunikwa kichwa chake, kwa kuwa yeye ni mfano na utukufu wa Mungu; lakini mwanamke ni utukufu wa mwanamume. 8 Kwa maana mwanamume hakutokana na mwanamke, bali mwanamke alitokana na mwanamume; 9 na, isitoshe, mwanamume hakuumbwa kwa ajili ya mwanamke, bali mwanamke kwa ajili ya mwanamume. 10 Hiyo ndiyo sababu mwanamke apaswa kuwa na ishara ya mamlaka juu ya kichwa chake kwa sababu ya malaika.
11 Mbali na hilo, kuhusiana na Bwana mwanamke si bila mwanamume wala mwanamume si bila mwanamke. 12 Kwa maana kama vile mwanamke ni kutokana na mwanamume, vivyo pia mwanamume ni kupitia mwanamke; lakini vitu vyote ni kutokana na Mungu. 13 Hukumuni nyinyi wenyewe: Je, yafaa mwanamke asali kwa Mungu akiwa bila kufunikwa kichwa? 14 Je, asili yenyewe haiwafundishi nyinyi kwamba ikiwa mwanamume ana nywele ndefu, ni fedheha; 15 lakini ikiwa mwanamke ana nywele ndefu, ni utukufu kwake? Kwa sababu nywele zake amepewa ziwe badala ya vazi la kichwani. 16 Hata hivyo, ikiwa mtu yeyote aonekana kubishania desturi fulani nyingine, sisi hatuna nyingine, wala makutaniko ya Mungu hayana.
17 Lakini, ingawa ninatoa maagizo haya, siwasifu nyinyi kwa sababu mwakutana pamoja, si kwa ajili ya lililo jema zaidi, bali kwa ajili ya lililo baya zaidi. 18 Kwa maana kwanza kabisa, nyinyi mjapo pamoja katika kutaniko, nasikia migawanyiko imo miongoni mwenu; na kwa kadiri fulani naamini hilo. 19 Kwa maana lazima pia yaweko mafarakano miongoni mwenu nyinyi, ili watu waliokubaliwa wapate pia kuwa dhahiri miongoni mwenu.
20 Kwa hiyo, nyinyi mjapo pamoja mahali pamoja, haiwezekani kula mlo wa jioni wa Bwana. 21 Kwa maana, mlapo huo, kila mtu hula kimbele mlo wake mwenyewe wa jioni, hivi kwamba mmoja ni mwenye njaa lakini mwingine ameingiwa na kileo. 22 Hakika mna nyumba za kulia na kunywea, sivyo? Au je, mwalidharau kutaniko la Mungu na kufanya wale wasio na kitu waaibike? Nitawaambia nyinyi nini? Je, nitawasifu nyinyi? Katika hilo siwasifu nyinyi.
23 Kwa maana nilipokea kutoka kwa Bwana kile nilichowapa nyinyi pia, kwamba Bwana Yesu katika usiku aliokuwa akielekea kukabidhiwa alitwaa mkate 24 na, baada ya kutoa shukrani, akaumega na kusema: “Huu wamaanisha mwili wangu ulio kwa ajili yenu. Fulizeni kufanya hili katika ukumbuko wangu.” 25 Akafanya hivyohivyo kwa habari ya kikombe pia, baada ya yeye kula mlo wa jioni, akisema: “Kikombe hiki chamaanisha agano jipya kwa msingi wa damu yangu. Fulizeni kufanya hili, mara nyingi kadiri mkinywavyo, katika ukumbuko wangu.” 26 Kwa maana mara nyingi kwa kadiri mlavyo mkate huu na kunywa kikombe hiki, mwafuliza kutangaza kifo cha Bwana, mpaka awasilipo.
27 Kwa sababu hiyo yeyote yule aulaye mkate au akinywaye kikombe cha Bwana isivyostahili atakuwa mwenye hatia kwa habari ya mwili na damu ya Bwana. 28 Kwanza acheni mtu ajikubali mwenyewe baada ya uchunguzi, na hivyo acheni ale ya mikate na anywe ya kikombe. 29 Kwa maana yeye alaye na anywaye ala na anywa hukumu dhidi yake mwenyewe ikiwa hafahamu mwili. 30 Hiyo ndiyo sababu wengi miongoni mwenu ni dhaifu na wagonjwa-wagonjwa, na wengi wamelala katika kifo. 31 Lakini kama tungefahamu kile tulicho sisi wenyewe, hatungehukumiwa. 32 Hata hivyo, tuhukumiwapo, twatiwa nidhamu na Yehova, ili tusipate kuhukumiwa pamoja na ulimwengu. 33 Kwa sababu hiyo, ndugu zangu, mjapo pamoja kula huo mlo, ngojaneni. 34 Ikiwa yeyote ni mwenye njaa, acheni ale nyumbani, ili msipate kuja pamoja kwenye hukumu. Lakini mambo yaliyobaki hakika nitayaweka katika utaratibu nifikapo hapo.