1 Wakorintho
5 Kwa kweli uasherati waripotiwa miongoni mwenu, tena uasherati wa namna ambayo haimo hata miongoni mwa mataifa, kwamba mtu fulani anaye mke wa baba yake. 2 Na je, nyinyi mmejitutumua, na je, badala ya hivyo hamkuomboleza, ili mtu aliyefanya kitendo hicho aondolewe mbali kutoka katikati yenu? 3 Mimi kwa kweli, ijapokuwa sipo katika mwili bali nipo katika roho, hakika nimehukumu tayari huyo mtu ambaye amefanya kwa njia hii, kama kwamba nipo, 4 kwamba katika jina la Bwana wetu Yesu, wakati mwapo mmekusanyika pamoja, pia roho yangu pamoja na nguvu ya Bwana wetu Yesu ipo, 5 mkabidhini Shetani mtu wa namna hiyo kwa ajili ya uangamizi wa mwili, ili roho ipate kuokolewa katika siku ya Bwana.
6 Sababu ya kujisifu kwenu si bora. Je, hamjui kwamba chachu kidogo huchachisha donge lote? 7 Ondoeni mbali chachu ya zamani, ili mpate kuwa donge jipya, kulingana na mlivyo bila chachu. Kwa maana, kwa kweli, Kristo kafara wetu wa sikukuu ya kupitwa amefanywa dhabihu. 8 Kwa sababu hiyo acheni tushike msherehekeo, si kwa chachu ya zamani, wala si kwa chachu ya ubaya na uovu, bali kwa keki zisizotiwa chachu za weupe wa moyo na kweli.
9 Katika barua yangu niliwaandikia nyinyi mkome kuchangamana katika ushirika na waasherati, 10 si kumaanisha kabisa na waasherati wa ulimwengu huu au watu wenye pupa na wanyang’anyi au waabudu-sanamu. Kama ndivyo, kwa kweli ingewabidi kutoka nje ya ulimwengu. 11 Lakini sasa ninawaandikia nyinyi mkome kuchangamana katika ushirika pamoja na yeyote aitwaye ndugu ambaye ni mwasherati au mtu mwenye pupa au mwabudu-sanamu au mtukanaji au mlevi au mnyang’anyi, wala hata kula pamoja na mtu wa namna hiyo. 12 Kwa maana nina jambo gani kwa kuhukumu wale walio nje? Je, nyinyi hamhukumu wale walio ndani, 13 huku Mungu akihukumu wale walio nje? “Ondoeni yule mtu mwovu miongoni mwenu wenyewe.”