1 Wakorintho
6 Je, kuna yeyote kati yenu aliye na kesi dhidi ya mwingine athubutu kwenda mahakamani mbele ya watu wasio waadilifu, na si mbele ya watakatifu? 2 Au je, hamjui kwamba watakatifu watauhukumu ulimwengu? Na ikiwa ulimwengu utahukumiwa nanyi, je, nyinyi hamstahili kuamua mambo yaliyo madogo sana? 3 Je, hamjui kwamba tutahukumu malaika? Kwa nini, basi, isiwe mambo ya maisha haya? 4 Basi, ikiwa nyinyi mna mambo ya maisha haya ya kuamuliwa, je, ni watu wadharauliwao katika kutaniko ambao mwawaweka kuwa mahakimu? 5 Ninasema ili kuwasukuma mwone aibu. Je, ni kweli kwamba hakuna hata mtu mmoja mwenye hekima miongoni mwenu atakayeweza kuhukumu kati ya ndugu zake, 6 bali ndugu aenda mahakamani pamoja na ndugu, na tena mbele ya wasio waamini?
7 Basi, kwa kweli, yamaanisha kushindwa kabisa kwenu kwamba mnakuwa na mashtaka ya kisheria mtu na mwenzake. Kwa nini badala ya hivyo hamjiachi mkosewe nyinyi wenyewe? Kwa nini badala ya hivyo hamjiachi mpunjwe nyinyi wenyewe? 8 Kinyume cha hilo, mwawakosea na kuwapunja ndugu zenu hasa.
9 Ama! Je, hamjui kwamba watu wasio waadilifu hawatarithi ufalme wa Mungu? Msiongozwe vibaya. Wala waasherati, wala waabudu-sanamu, wala wazinzi, wala wanaume watunzwao kwa makusudi yasiyo ya asili, wala wanaume walalao pamoja na wanaume, 10 wala wezi, wala watu wenye pupa, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang’anyi hawatarithi ufalme wa Mungu. 11 Na hata hivyo baadhi yenu ndivyo mlivyokuwa. Lakini mmeoshwa mkawa safi, lakini mmetakaswa, lakini mmetangazwa kuwa waadilifu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo na kwa roho ya Mungu wetu.
12 Mambo yote yaruhusika kisheria kwangu; lakini si mambo yote yenye faida. Mambo yote yaruhusika kisheria kwangu; lakini hakika mimi sitajiacha mwenyewe niletwe chini ya mamlaka na kitu chochote. 13 Vyakula kwa ajili ya tumbo, na tumbo kwa ajili ya vyakula; lakini Mungu atafanya hilo na pia hivyo viwe si kitu. Basi mwili si kwa ajili ya uasherati, bali kwa ajili ya Bwana; na Bwana ni kwa ajili ya mwili. 14 Lakini Mungu alimfufua Bwana na pia atatufufua sisi kutoka kwenye kifo kupitia nguvu yake.
15 Je, hamjui kwamba miili yenu ni viungo vya Kristo? Basi, je, nitavichukua viungo vya Kristo na kuvifanya viwe viungo vya kahaba? Hilo lisitukie kamwe! 16 Ama! Je, hamjui kwamba yeye aunganaye na kahaba ni mwili mmoja? Kwa maana, “Hao wawili,” asema yeye, “watakuwa mwili mmoja.” 17 Lakini yeye aunganaye na Bwana ni roho moja. 18 Ukimbieni uasherati. Kila dhambi nyingine ambayo mtu huenda akafanya iko nje ya mwili wake, lakini yeye azoeaye uasherati anafanya dhambi dhidi ya mwili wake mwenyewe. 19 Ama! Je, hamjui kwamba mwili wenu nyinyi watu ni hekalu la roho takatifu katika nyinyi, mliyo nayo kutoka kwa Mungu? Pia, nyinyi si mali yenu wenyewe, 20 kwa maana mlinunuliwa kwa bei. Kwa vyovyote, mtukuzeni Mungu katika mwili wenu nyinyi watu.