1 Wakorintho
7 Sasa kuhusu mambo mliyoandika juu yayo, ni vema kwa mwanamume kutogusa mwanamke; 2 lakini, kwa sababu ya kuenea kwa uasherati, acheni kila mwanamume awe na mke wake mwenyewe na kila mwanamke awe na mume wake mwenyewe. 3 Acha mume ampe mke wake haki yake; lakini acha mke pia afanye hivyohivyo kwa mume wake. 4 Mke hatumii mamlaka juu ya mwili wake mwenyewe, bali mume wake hutumia; hivyohivyo, pia, mume hatumii mamlaka juu ya mwili wake mwenyewe, bali mke wake hutumia. 5 Msiwe mkinyimana hiyo, ila kwa makubaliano kwa wakati uliowekwa rasmi, ili mpate kutumia wakati kwa sala na mpate kuja pamoja tena, ili Shetani asipate kufuliza kuwashawishi kwa sababu ya kukosa kwenu kujirekebisha. 6 Hata hivyo, nasema hilo kwa kutoa ruhusa maalumu, si kwa kutoa amri. 7 Lakini nataka watu wote wawe kama mimi mwenyewe nilivyo. Hata hivyo, kila mmoja ana zawadi yake mwenyewe kutoka kwa Mungu, mmoja kwa njia hii, mwingine kwa njia hii.
8 Basi nawaambia waseja na wajane, ni vema kwao wabaki kama mimi nilivyo. 9 Lakini ikiwa hawana kujidhibiti, acheni waoe au kuolewa, kwa maana ni bora kuoa na kuolewa kuliko kuwashwa na harara.
10 Kwa watu waliooa au kuolewa natoa maagizo, lakini si mimi bali Bwana, kwamba mke hapaswi kuondoka kwa mume wake; 11 lakini kwa kweli akiondoka, acha akae bila kuolewa au sivyo apatane tena na mume wake; na mume hapaswi kumwacha mke wake.
12 Lakini kwa wale wengine nawaaambia, ndiyo, mimi, si Bwana: Ikiwa ndugu yeyote ana mke asiyeamini, na bado ni mwenye kukubali kukaa pamoja naye, asimwache; 13 na mwanamke aliye na mume asiyeamini, na bado ni mwenye kukubali kukaa pamoja naye, na asimwache mume wake. 14 Kwa maana mume asiyeamini hutakaswa katika uhusiano na mke wake, na mke asiyeamini hutakaswa katika uhusiano na huyo ndugu; kama sivyo, watoto wenu kwa kweli wangekuwa si safi, lakini sasa wao ni watakatifu. 15 Lakini yule asiyeamini akiendelea kuondoka, acha aondoke; ndugu au dada hayumo katika utumwa chini ya hali za namna hiyo, lakini Mungu amewaita nyinyi kwenye amani. 16 Kwa maana, mke, wajuaje kama utaokoa mume wako? Au, mume, wajuaje kama utaokoa mke wako?
17 Ila tu, kama vile Yehova amempa kila mmoja fungu, acheni kila mmoja ajiendeshe kama vile Mungu amemwita. Na ndivyo niagizavyo rasmi katika makutaniko yote. 18 Je, mtu yeyote aliitwa akiwa ametahiriwa? Acheni asipate kuwa asiyetahiriwa. Je, mtu yeyote ameitwa akiwa katika kutotahiriwa? Acheni asitahiriwe. 19 Tohara haimaanishi kitu, na kutotahiriwa hakumaanishi kitu, bali kushika amri za Mungu humaanisha kitu. 20 Katika hali yoyote ile ambayo kila mmoja aliitwa, acheni abaki katika hiyo. 21 Je, uliitwa ulipokuwa mtumwa? Usiache hilo likutie wasiwasi; lakini ikiwa waweza pia kuwa huru, afadhali utwae fursa hiyo. 22 Kwa maana yeyote katika Bwana aliyeitwa alipokuwa mtumwa ndiye mtu mwekwa-huru wa Bwana; hivyohivyo yeye aliyeitwa alipokuwa mtu-huru ni mtumwa wa Kristo. 23 Mlinunuliwa kwa bei; komeni kuwa watumwa wa wanadamu. 24 Katika hali yoyote ile ambayo kila mmoja aliitwa, akina ndugu, acheni abaki katika hiyo akishirikiana na Mungu.
25 Sasa kuhusu mabikira sina amri kutoka kwa Bwana, lakini natoa kauli yangu nikiwa mtu aliyeonyeshwa rehema na Bwana kuwa mwaminifu. 26 Kwa hiyo nafikiria hili kuwa jema kwa sababu ya uhitaji ulio hapa pamoja nasi, kwamba ni vema kwa mtu kuendelea kama alivyo. 27 Je, umefungwa kwa mke? Koma kutafuta sana kufunguliwa. Je, umefunguliwa kutoka kwa mke? Koma kutafuta sana mke. 28 Lakini hata kama ungeoa, hungefanya dhambi. Na kama mtu-bikira angeoa, huyo hangefanya dhambi. Hata hivyo, wale wafanyao hivyo watakuwa na dhiki katika mwili wao. Lakini mimi ninawaepusha nyinyi.
29 Zaidi ya hayo, nisemalo ni hili, akina ndugu, wakati ubakio umepunguzwa. Tangu sasa acheni wale walio na wake wawe kama kwamba hawana, 30 na pia wale watoao machozi wawe kama wale wasiotoa machozi, na wale washangiliao kama wale wasioshangilia, na wale wanunuao kama wale wasio na kitu, 31 na wale wanaoutumia ulimwengu kama wale wasioutumia kwa ukamili; kwa maana mandhari ya ulimwengu huu inabadilika. 32 Kwa kweli, nataka msihangaike. Mtu ambaye hajaoa huhangaikia mambo ya Bwana, jinsi awezavyo kupata kibali cha Bwana. 33 Lakini mtu aliyeoa huhangaikia mambo ya ulimwengu, jinsi awezavyo kupata kibali cha mke wake, 34 naye amegawanyika. Zaidi, mwanamke ambaye hajaolewa, na bikira, huhangaikia mambo ya Bwana, apate kuwa mtakatifu katika mwili wake na pia katika roho yake. Hata hivyo, mwanamke aliyeolewa huhangaikia mambo ya ulimwengu, jinsi awezavyo kupata kibali cha mume wake. 35 Lakini hili nasema kwa faida yenu ya kibinafsi, si ili nitupe tanzi juu yenu nyinyi, bali ili niwasukume nyinyi kwenye lile linalofaa na lile limaanishalo kuhudumia Bwana daima bila kukengeushwa fikira.
36 Lakini ikiwa yeyote afikiri anajiendesha isivyofaa kuelekea ubikira wake, ikiwa huo umepita mchanuko wa ujana, na hiyo ndiyo njia ambayo yapasa kutukia, acheni afanye lile atakalo; hafanyi dhambi. Acheni waoe au waolewe. 37 Lakini ikiwa yeyote asimama ametulia katika moyo wake, akiwa hana uhitaji wowote, lakini ana mamlaka juu ya nia yake mwenyewe na amefanya uamuzi huu katika moyo wake mwenyewe, kutunza ubikira wake mwenyewe, yeye atafanya vema zaidi. 38 Kwa sababu hiyo yeye pia aozaye ubikira wake afanya vema, lakini yeye asiyeuoza atafanya bora.
39 Mke amefungwa wakati wote ambao mume wake yuko hai. Lakini iwapo mume wake alala usingizi katika kifo, yuko huru kuolewa na yeyote atakaye, katika Bwana tu. 40 Lakini yeye ni mwenye furaha zaidi akibaki kama alivyo, kulingana na kauli yangu. Hakika nafikiri mimi pia nina roho ya Mungu.