1 Wakorintho
8 Sasa kuhusu vyakula vitolewavyo kwa sanamu: twajua sisi sote tuna ujuzi. Ujuzi hututumuka, lakini upendo hujenga. 2 Ikiwa yeyote afikiri amejipatia ujuzi juu ya kitu fulani, bado hajakijua kama vile apaswavyo kukijua. 3 Lakini ikiwa yeyote ampenda Mungu, huyo ajulikana naye.
4 Sasa kuhusu kula vyakula vitolewavyo kwa sanamu, twajua kwamba sanamu si kitu katika ulimwengu, na kwamba hakuna Mungu ila mmoja. 5 Kwa maana hata ingawa kuna wale waitwao “miungu,” kama wako mbinguni au duniani, kama vile kulivyo na “miungu” mingi na “mabwana” wengi, 6 kwa kweli kwetu kuna Mungu mmoja Baba, ambaye kutokana naye vitu vyote vipo, na sisi kwa ajili yake; na kuna Bwana mmoja, Yesu Kristo, ambaye kupitia yeye vitu vyote vipo, na sisi kupitia yeye.
7 Hata hivyo, hakuna ujuzi huu katika watu wote; bali wengine, wakiwa na desturi ya sanamu hadi sasa, hula chakula kama kitu kilichofanywa dhabihu kwa sanamu, na dhamiri yao, ikiwa dhaifu, imetiwa unajisi. 8 Lakini chakula hakitatupendekeza kwa Mungu; ikiwa hatuli, hatupungukiwi, na, ikiwa twala, hatupati sifa sisi wenyewe. 9 Lakini fulizeni kuangalia kwamba mamlaka yenu hii isipate kwa njia fulani kuwa kipingamizi chenye kukwaza kwa wale walio dhaifu. 10 Kwa maana iwapo yeyote akuona wewe, uliye na ujuzi, ukiwa umeegama kwenye mlo katika hekalu la sanamu, je, dhamiri ya huyo aliye dhaifu haitajengwa kufikia hatua ya kula vyakula vilivyotolewa kwa sanamu? 11 Kwa kweli, kwa ujuzi wako, mtu ambaye ni dhaifu anaharibiwa, ndugu yako ambaye kwa ajili yake Kristo alikufa. 12 Lakini nyinyi watu mtendapo dhambi hivyo dhidi ya ndugu zenu na kujeruhi dhamiri yao iliyo dhaifu, mnatenda dhambi dhidi ya Kristo. 13 Kwa hiyo, ikiwa chakula chafanya ndugu yangu akwazike, hakika mimi sitakula nyama tena kamwe hata kidogo, ili nisipate kufanya ndugu yangu akwazike.