1 Wakorintho
9 Je, mimi si huru? Je, mimi si mtume? Je, mimi sijamwona Yesu Bwana wetu? Je, nyinyi si kazi yangu katika Bwana? 2 Ikiwa mimi si mtume kwa wengine, hakika kabisa niko hivyo kwenu, kwa maana nyinyi ndio muhuri unaothibitisha utume wangu katika uhusiano na Bwana.
3 Kujitetea kwangu kwa wale wanichunguzao ni kama ifuatavyo: 4 Sisi tuna mamlaka ya kula na kunywa, sivyo? 5 Sisi tuna mamlaka ya kuongoza dada huku na huku akiwa mke, hata kama vile wale wengine wa mitume na ndugu za Bwana na Kefa, sivyo? 6 Au je, ni Barnaba na mimi tu tusio na mamlaka ya kujiepusha kufanya kazi ya kimwili? 7 Ni nani atumikaye wakati wowote akiwa askari kwa gharama yake mwenyewe? Ni nani apandaye shamba la mizabibu na asile katika matunda yalo? Au ni nani achungaye kundi na asile kiasi fulani cha maziwa ya kundi?
8 Je, ninasema mambo haya kwa viwango vya kibinadamu? Au je, Sheria haisemi mambo haya pia? 9 Kwa maana katika sheria ya Musa imeandikwa: “Lazima usimfunge kinywa fahali anapopura nafaka.” Je, ni mafahali ambao Mungu anajali? 10 Au yeye asema hilo kwa ajili yetu tu? Kwa kweli ni kwa ajili yetu hilo liliandikwa, kwa sababu mtu alimaye kwa plau apaswa kulima kwa plau akiwa na tumaini na mtu apuraye apaswa kufanya hivyo akiwa na tumaini la kuwa mshiriki.
11 Ikiwa tumepanda vitu vya kiroho kwenu, je, ni jambo kubwa ikiwa tutavuna kutoka kwenu vitu vilivyo kwa ajili ya mwili? 12 Ikiwa watu wengine hushiriki kutokana na mamlaka hii juu yenu, je, sisi si zaidi sana hivyo? Hata hivyo, sisi hatujafanya utumizi wa mamlaka hii, bali tunahimili mambo yote, ili tusipate kutoa kizuizi chochote kwa habari njema juu ya Kristo. 13 Je, hamjui kwamba watu wanaofanya wajibu mbalimbali mtakatifu hula vitu vya hekalu, na wale wanaohudumu daima kwenye madhabahu hupata fungu lao wenyewe pamoja na madhabahu? 14 Katika njia hiyo, pia, Bwana aliagiza rasmi kwa ajili ya wale wanaotangaza habari njema kuishi kwa njia ya habari njema.
15 Lakini mimi sijafanya utumizi wa hata mmoja wa maandalizi hayo. Kwa kweli, sijaandika mambo haya ili iwe hivyo katika kisa changu, kwa maana ingekuwa vizuri zaidi nife kuliko—hakuna mtu atakayefanya sababu yangu ya kujisifu iwe bure! 16 Ikiwa, sasa, ninatangaza habari njema, hiyo si sababu ya mimi kujisifu, kwa maana nimewekewa sharti. Kwa kweli, ole wangu mimi ikiwa sikutangaza habari njema! 17 Ikiwa nafanya hilo kwa kupenda, nina thawabu; lakini ikiwa nafanya hilo dhidi ya kupenda kwangu, vyovyote vile nina usimamizi-nyumba niliokabidhiwa. 18 Basi, thawabu yangu ni nini? Kwamba ninapokuwa nikitangaza habari njema nipate kuitoa habari njema bila gharama, kwa madhumuni ya kwamba nisipate kutumia vibaya mamlaka yangu katika habari njema.
19 Kwa maana, ingawa niko huru na watu wote, nimejifanya mwenyewe mtumwa kwa wote, ili nipate kuwapata watu walio wengi zaidi sana. 20 Na kwa hiyo kwa Wayahudi nilipata kuwa kama Myahudi, ili niweze kuwapata Wayahudi; kwa wale walio chini ya sheria nilipata kuwa kama aliye chini ya sheria, ingawa mimi mwenyewe siko chini ya sheria, ili niweze kuwapata wale walio chini ya sheria. 21 Kwa wale wasio na sheria nilipata kuwa kama aliye bila sheria, ijapokuwa mimi siko bila sheria kuelekea Mungu bali niko chini ya sheria kuelekea Kristo, ili niweze kuwapata wale wasio na sheria. 22 Kwa walio dhaifu nilipata kuwa dhaifu, ili niweze kuwapata walio dhaifu. Nimekuwa mambo yote kwa watu wa namna zote, ili nipate kwa vyovyote kuokoa wengine. 23 Lakini nafanya mambo yote kwa ajili ya habari njema, ili nipate kuwa mshiriki wayo pamoja na wengine.
24 Je, hamjui kwamba wakimbiaji katika mbio wote hukimbia, lakini ni mmoja tu apokeaye tuzo? Kimbieni kwa njia ambayo mwaweza kuipata tuzo. 25 Zaidi ya hayo, kila mtu anayeshiriki katika shindano hutumia kujidhibiti katika mambo yote. Sasa wao, bila shaka hufanya hilo ili waweze kupata taji lenye kuharibika, lakini sisi lisiloharibika. 26 Kwa hiyo, jinsi ninavyokimbia si bila uhakika; jinsi ninavyoelekeza ngumi zangu ni ili nisiwe nikipiga hewa; 27 lakini napiga-piga mwili wangu ngumi na kuuongoza kama mtumwa, ili, baada ya mimi kuwa nimewahubiria wengine, mimi mwenyewe nisiwe mwenye kukataliwa kwa njia fulani.