Wafilipi
Kwa Wafilipi
1 Paulo na Timotheo, watumwa wa Kristo Yesu, kwa watakatifu wote katika muungano na Kristo Yesu walio katika Filipi, pamoja na waangalizi na watumishi wa huduma:
2 Na mwe na fadhili isiyostahiliwa na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.
3 Namshukuru Mungu wangu sikuzote kila niwakumbukapo nyinyi 4 katika kila dua yangu kwa ajili yenu nyote, nitoapo dua yangu kwa shangwe, 5 kwa sababu ya mchango ambao mmefanyia habari njema tangu siku ya kwanza hadi dakika hii. 6 Kwa maana nina hakika juu ya jambo hilihili, kwamba yeye aliyeanza kazi njema katika nyinyi ataiendeleza kwenye ukamilisho hadi siku ya Yesu Kristo. 7 Ni sawa kwangu kufikiri hili kuhusu nyinyi nyote, kwa sababu yangu kuwa nanyi katika moyo wangu, nyinyi nyote mkiwa washiriki pamoja nami katika fadhili isiyostahiliwa, katika vifungo vyangu vya gereza na katika kutetea na kuthibitisha kisheria habari njema.
8 Kwa maana Mungu ni shahidi wangu wa jinsi ninavyowatamani sana nyinyi nyote katika namna ya shauku nyororo kama aliyo nayo Kristo Yesu. 9 Na hili ndilo mimi huendelea kusali, kwamba upendo wenu upate kuzidi bado hata zaidi na zaidi pamoja na ujuzi sahihi na ufahamu kamili; 10 kwamba mpate kuhakikisha mambo yaliyo ya maana zaidi, ili mpate kuwa bila dosari na kutowakwaza wengine hadi siku ya Kristo, 11 na mpate kujazwa matunda ya uadilifu, ambayo ni kupitia Yesu Kristo, kwa utukufu na sifa ya Mungu.
12 Sasa nataka nyinyi mjue, akina ndugu, kwamba mambo yangu yamegeuka kuwa kwa ajili ya kusonga mbele kwa habari njema badala ya kuwa vingine, 13 hivi kwamba vifungo vyangu vimejulikana kwa watu wote kwa kushirikiana na Kristo miongoni mwa Walindaji wa Praetori wote na wale wengine wote; 14 na walio wengi zaidi kati ya akina ndugu katika Bwana, wakihisi uhakika kwa sababu ya vifungo vyangu vya gereza, wanaonyesha moyo mkuu hata zaidi kulisema neno la Mungu bila hofu.
15 Kweli, wengine wanahubiri Kristo kupitia husuda na ushindani, lakini wengine pia kupitia nia njema. 16 Hao wa mwisho wanamtangaza Kristo hadharani kutokana na upendo, kwa maana wao wajua mimi nimewekwa hapa kwa ajili ya kutetea habari njema; 17 lakini wale wa kwanza hufanya hivyo kutokana na ugomvi, si kwa madhumuni safi, kwa maana wao wanadhania kuchochea dhiki kwangu katika vifungo vyangu vya gereza. 18 Nini basi? Si kitu, ila kwamba katika kila njia, kama ni katika kisingizio au ni katika kweli, Kristo anatangazwa mbele ya watu wote, na katika hili mimi nashangilia. Kwa kweli, hakika nitafuliza pia kushangilia, 19 kwa maana najua hili litatokeza wokovu wangu kupitia dua yenu na gawio la roho ya Yesu Kristo, 20 kwa kupatana na taraja langu lenye hamu na tumaini kwamba sitaaibika katika habari yoyote, bali kwamba katika uhuru wote wa usemi, Kristo atatukuzwa hivyo sasa kama sikuzote hapo mbele, kwa njia ya mwili wangu, iwe ni kupitia uhai au kupitia kifo.
21 Kwa maana katika kisa changu kuishi ni Kristo, na kufa, ni kupata faida. 22 Basi ikiwa ni kuendelea kuishi katika mwili, hilo ni tunda la kazi yangu—na bado jambo lililo la kuteua silijulishi. 23 Niko chini ya mkazo kutokana na mambo mawili haya; lakini nitamanicho ni kule kuachiliwa na kule kuwa pamoja na Kristo, kwa maana hili, kwa hakika, ni bora zaidi. 24 Hata hivyo, kwangu mimi kukaa katika mwili ni lazima zaidi kwa sababu yenu. 25 Kwa hiyo, nikiwa na hakika juu ya hili, mimi najua nitabaki na kukaa na nyinyi nyote kwa ajili ya kusonga mbele kwenu na shangwe iliyo ya imani yenu, 26 ili mchachawo wenu upate kufurika katika Kristo Yesu kwa sababu yangu kupitia kuwapo kwangu tena pamoja nanyi.
27 Ila tu jiendesheni kwa namna yenye kustahili habari njema juu ya Kristo, ili, iwe kama naja na kuwaona nyinyi au iwe sipo, nipate kusikia juu ya mambo ambayo yawahusu nyinyi, kwamba mnasimama imara katika roho moja, kwa nafsi moja mkipigana sambamba kwa ajili ya imani ya habari njema, 28 na mkiwa hamwogopeshwi sana katika jambo lolote na wapinzani wenu. Jambo hilihili ni ithibati kwao ya uangamizo, lakini ya wokovu kwenu; na wonyesho huu ni kutoka kwa Mungu, 29 kwa sababu nyinyi mlipewa pendeleo kwa ajili ya Kristo, si kuweka tu imani yenu katika yeye, bali pia kuteseka kwa ajili yake. 30 Kwa maana mna shindano lilelile kama mlivyoona katika kisa changu na kama msikiavyo sasa katika kisa changu.