1 Wathesalonike
4 Mwishowe, akina ndugu, twawaomba nyinyi na kuwahimiza kwa bidii kwa njia ya Bwana Yesu, kama vile mlivyopokea agizo kutoka kwetu juu ya jinsi mpaswavyo kutembea na kumpendeza Mungu, kama vile kwa kweli mnavyotembea, kwamba mngefuliza kufanya hilo kwa ukamili zaidi. 2 Kwa maana mwayajua maagizo tuliyowapa nyinyi kupitia Bwana Yesu.
3 Kwa maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu, kule kutakaswa kwenu, kwamba mjiepushe na uasherati; 4 kwamba kila mmoja wenu apaswe kujua jinsi ya kupata umiliki wa chombo chake mwenyewe katika utakaso na heshima, 5 si katika hamu yenye tamaa ya ngono kama ile waliyo nayo pia mataifa wale wasiomjua Mungu; 6 kwamba yeyote asifikie hatua ya kudhuru na kuziingilia haki za ndugu yake katika jambo hilo, kwa sababu Yehova ndiye atozaye adhabu kwa ajili ya mambo yote haya, kama vile tulivyowaambia nyinyi kimbele na pia tukawapa ushahidi kamili. 7 Kwa maana Mungu alituita sisi, si kwa kuruhusu ukosefu wa usafi, bali kwa kuhusiana na utakaso. 8 Kwa hiyo, basi, mtu aonyeshaye kupuuza anapuuza, si mwanadamu bali Mungu, atiaye roho takatifu yake ndani yenu.
9 Hata hivyo, kuhusu upendo wa kidugu, hamhitaji sisi tuwe tukiwaandikia nyinyi, kwa maana nyinyi wenyewe hufundishwa na Mungu kupendana; 10 na, kwa kweli, nyinyi mnafanya hilo kwa ndugu wote katika Makedonia yote. Lakini twawahimiza nyinyi kwa bidii, akina ndugu, mwendelee kufanya hilo kwa kipimo chenye kujaa zaidi, 11 na kufanya iwe shabaha yenu kuishi kwa utulivu na kushughulika na mambo yenu wenyewe na kufanya kazi kwa mikono yenu, kama vile tulivyowaagiza nyinyi; 12 ili mpate kuwa mkitembea kwa adabu kwa habari ya watu walio nje na mkiwa bila kuhitaji kitu chochote.
13 Zaidi ya hayo, akina ndugu, hatutaki nyinyi mwe wasio na ujuzi kuhusu wale ambao wamelala katika kifo; ili msipate kuwa na majonzi kama vile wale wengine wasio na tumaini. 14 Kwa maana ikiwa imani yetu ni kwamba Yesu alikufa na kufufuliwa tena, ndivyo, pia, wale ambao wamelala usingizi katika kifo kupitia Yesu, Mungu atawaleta pamoja naye. 15 Kwa maana hili ndilo tuwaambialo nyinyi kwa neno la Yehova, kwamba sisi tulio hai ambao twabaki hadi kuwapo kwa Bwana hatutawatangulia kwa njia yoyote wale ambao wamelala usingizi katika kifo; 16 kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni akiwa na mwito wa kuamuru, akiwa na sauti ya malaika mkuu na kwa tarumbeta ya Mungu, na wale walio wafu katika muungano na Kristo watafufuliwa kwanza. 17 Baadaye sisi tulio hai tuliobaki tutanyakuliwa, pamoja nao, katika mawingu ili kukutana na Bwana katika hewa; na hivyo tutakuwa sikuzote pamoja na Bwana. 18 Kwa sababu hiyo fulizeni kufarijiana kwa maneno hayo.