1 Timotheo
4 Hata hivyo, tamko lililopuliziwa lasema wazi kwamba katika vipindi vya wakati vya baadaye wengine wataanguka kutoka kwenye imani, wakikazia uangalifu matamko yaliyopuliziwa yenye kuongoza vibaya na mafundisho ya roho waovu, 2 kwa unafiki wa watu wasemao uwongo, waliotiwa alama katika dhamiri zao kama kwa chuma chenye moto cha kutilia chapa; 3 wakikataza kuoa au kuolewa, wakiamuru kujiepusha na vyakula ambavyo Mungu aliumba vipate kushirikiwa kwa utoaji-shukrani na wale walio na imani na wajuao kweli kwa usahihi. 4 Sababu ya hili ni kwamba kila kiumbe cha Mungu ni bora, na hakuna kitu cha kukataliwa ikiwa chapokewa kwa utoaji-shukrani, 5 kwa maana chatakaswa kupitia neno la Mungu na sala juu yacho.
6 Kwa kuwapa akina ndugu mashauri haya utakuwa mhudumu bora wa Kristo Yesu, mwenye kulishwa maneno ya imani na fundisho bora ambalo umefuata kwa ukaribu. 7 Bali kataa hadithi zisizo za kweli ambazo huhalifu kilicho kitakatifu na ambazo wanawake wazee husimulia. Kwa upande mwingine, uwe ukijizoeza mwenyewe ujitoaji-kimungu ukiwa shabaha yako. 8 Kwa maana mazoezi ya kimwili ni yenye manufaa kidogo; lakini ujitoaji-kimungu ni wenye manufaa kwa mambo yote, kwa kuwa una ahadi ya uhai wa sasa na ule utakaokuja. 9 Ya uaminifu na yenye kustahili ukubalifu kamili ni taarifa hiyo. 10 Kwa maana kwa madhumuni haya tunafanya kazi kwa bidii na kujikakamua wenyewe, kwa sababu tumeweka tumaini letu juu ya Mungu aliye hai, ambaye ni Mwokozi wa namna zote za watu, hasa wa walio waaminifu.
11 Fuliza kutoa amri hizi na kuzifundisha. 12 Usiache kamwe mtu yeyote adharau ujana wako. Kinyume chake, uwe kielelezo kwa waaminifu katika kusema, katika mwenendo, katika upendo, katika imani, katika usafi wa kiadili. 13 Ninapokuwa nikija, endelea kujitahidi mwenyewe kusoma mbele ya watu wote, kuhimiza kwa bidii, kufundisha. 14 Usiwe ukipuuza zawadi iliyo katika wewe uliyopewa kupitia utabiri na wakati baraza la wanaume wazee lilipoweka mikono yalo juu yako. 15 Fikiri kwa uzito juu ya mambo haya; vama katika hayo, ili kusonga mbele kwako kupate kuwa dhahiri kwa watu wote. 16 Daima kaza uangalifu kwako mwenyewe na kwa kufundisha kwako. Kaa katika mambo haya, kwa maana kwa kufanya hivi utajiokoa wewe mwenyewe na wale wakusikilizao pia.