1 Petro
Ya Kwanza ya Petro
1 Petro, mtume wa Yesu Kristo, kwa wakazi wa muda waliotawanyika huku na huku katika Ponto, Galatia, Kapadokia, Asia, na Bithinia, kwa wale wachaguliwa 2 kulingana na ujuzi wa kimbele wa Mungu aliye Baba, kwa utakaso na roho, kwa kusudi la kuwa kwao watiifu na wenye kunyunyiziwa damu ya Yesu Kristo:
Fadhili isiyostahiliwa na amani ziongezwe kwenu.
3 Mbarikiwa awe Mungu na Baba ya Bwana wetu Yesu Kristo, kwa maana kulingana na rehema yake kubwa alitupa sisi uzaliwa mpya kwenye tumaini lililo hai kupitia ufufuo wa Yesu Kristo kutoka kwa wafu, 4 kwenda kwenye urithi usiofisidika na usiotiwa unajisi na usiofifia. Umewekwa akiba katika mbingu kwa ajili yenu nyinyi, 5 mnaolindwa salama na nguvu ya Mungu kupitia imani kwa wokovu ulio tayari kufunuliwa katika kipindi cha wakati cha mwisho. 6 Katika uhakika huu mnashangilia sana, ingawa kwa muda kidogo mmetiwa kihoro wakati wa sasa, ikiwa ni lazima, kwa namna mbalimbali za majaribu, 7 ili ubora wa imani yenu uliojaribiwa, ulio na thamani kubwa zaidi sana kuliko dhahabu ambayo huharibika ijapokuwa kuthibitishwa kwayo na moto, upatikane kuwa sababu ya sifa na utukufu na heshima wakati wa ufunuo wa Yesu Kristo. 8 Ingawa hamkumwona yeye kamwe, mwampenda. Ingawa hamwi mkimtazama wakati wa sasa, bado mwadhihirisha imani katika yeye na mnashangilia sana kwa shangwe isiyosemeka na iliyotukuzwa, 9 huku mkipokea mwisho wa imani yenu, ule wokovu wa nafsi zenu.
10 Kuhusu wokovu huu wenyewe kuulizia habari kwa bidii yenye kuendelea na utafutaji wa uangalifu sana ulifanywa na manabii ambao walitoa unabii juu ya fadhili isiyostahiliwa iliyokusudiwa kwa ajili yenu. 11 Walifuliza kupeleleza-peleleza ni majira gani maalumu au ni namna gani ya majira roho iliyo ndani yao ilikuwa ikionyesha kuhusu Kristo ilipokuwa ikitoa ushahidi kimbele juu ya mateso ya Kristo na juu ya matukufu ambayo yangefuata hayo. 12 Ilifunuliwa kwao kwamba, si kwao wenyewe, bali kwenu, wao walikuwa wakihudumu mambo ambayo sasa yametangazwa kwenu kupitia wale ambao wamewatangazia nyinyi habari njema kwa roho takatifu iliyotumwa kutoka mbinguni. Ndani ya mambo hayohayo malaika wanatamani kuchungulia.
13 Kwa sababu hiyo kazeni akili zenu kwa ajili ya utendaji, tunzeni akili zenu kikamili; wekeni tumaini lenu juu ya fadhili isiyostahiliwa itakayoletwa kwenu wakati wa ufunuo wa Yesu Kristo. 14 Kama watoto watiifu, komeni kuwa mkifanyizwa kulingana na mtindo wa tamaa zenu mlizokuwa nazo hapo zamani katika kutokuwa kwenu na ujuzi, 15 bali, kwa kupatana na Mtakatifu aliyewaita, nyinyi wenyewe pia iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote, 16 kwa sababu imeandikwa: “Lazima mwe watakatifu, kwa sababu mimi ni mtakatifu.”
17 Zaidi ya hilo, ikiwa mnamwita Baba ambaye huhukumu bila ubaguzi wowote kulingana na kazi ya kila mmoja, jiendesheni wenyewe kwa hofu katika wakati wa ukaaji wenu wa kigeni. 18 Maana mwajua kwamba haikuwa kwa vitu vyenye kuharibika, kwa fedha au dhahabu, kwamba mlikombolewa kutoka kwenye namna ya mwenendo usio na matunda uliopokewa kupitia pokeo kutoka kwa baba zenu wa zamani. 19 Bali ilikuwa kwa damu yenye bei, kama ile ya mwana-kondoo asiye na waa na asiye na doa, naam, ya Kristo. 20 Kweli, yeye alijulikana mbele kabla ya kuwekwa msingi wa ulimwengu, lakini akafanywa dhahiri kwenye mwisho wa nyakati kwa ajili yenu nyinyi 21 ambao kupitia yeye nyinyi ni waamini katika Mungu, yeye aliyemfufua kutoka kwa wafu na kumpa utukufu; hivi kwamba imani na tumaini lenu zipate kuwa katika Mungu.
22 Sasa kwa kuwa mmetakasa nafsi zenu kwa kutii kwenu ile kweli tokeo likiwa shauku ya kidugu isiyo na unafiki, mpendane kwa juhudi nyingi kutoka moyoni. 23 Kwa maana mmepewa uzaliwa mpya, si kupitia mbegu ya uzazi yenye kufisidika, bali kupitia isiyofisidika, kupitia neno la Mungu aliye hai na anayedumu daima. 24 Kwa maana “mwili wote wenye nyama ni kama nyasi, na utukufu wao wote ni kama chanuo la nyasi; nyasi huwa yenye kunyauka, na ua huanguka, 25 bali usemi wa Yehova hudumu milele.” Basi, huu ndio “usemi,” huu ambao umetangazwa kwenu kuwa habari njema.