1 Petro
2 Basi, wekeni mbali ubaya wote na udanganyaji wote na unafiki na husuda na namna zote za kusengenya, 2 na, kama vitoto vichanga vilivyozaliwa karibuni, fanyizeni hamu sana ya maziwa yasiyoghushiwa yaliyo ya neno, ili kupitia hilo mpate kukua kufikia wokovu, 3 mradi mmeonja kwamba Bwana ni mwenye fadhili.
4 Kwa kumjia yeye kama kwenye jiwe lililo hai, ambalo lilikataliwa, ni kweli, na wanadamu, bali lililochaguliwa, lenye bei, kwa Mungu, 5 nyinyi wenyewe pia mkiwa mawe yaliyo hai mnakuwa wenye kujengwa kuwa nyumba ya kiroho kwa kusudi la ukuhani mtakatifu, ili kutoa dhabihu za kiroho zenye kukubalika kwa Mungu kupitia Yesu Kristo. 6 Kwa maana limo katika Andiko: “Tazama! Ninaweka katika Zayoni jiwe, lililochaguliwa, jiwe la pembeni la msingi, lenye bei; na hakuna mtu anayedhihirisha imani katika hilo ambaye atakuja kukata tamaa kwa vyovyote.”
7 Kwa hiyo, ni kwenu kwamba yeye ni mwenye bei, kwa kuwa nyinyi ni waamini; lakini kwa wale wasioamini, “jiwe lilelile ambalo wajenzi walikataa limekuwa kichwa cha pembeni,” 8 na “jiwe la kukwaza na tungamo-mwamba la udhia.” Hawa wanajikwaa kwa sababu ni wasiotii neno. Kwa madhumuni hayohayo pia waliwekwa rasmi. 9 Lakini nyinyi ni “jamii iliyochaguliwa, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu kwa ajili ya miliki ya pekee, kwamba mpate kutangaza kotekote sifa bora kabisa” za yeye aliyewaita nyinyi kutoka katika giza kuingia katika nuru yake ya ajabu. 10 Kwa kuwa wakati mmoja nyinyi mlikuwa si watu, lakini sasa nyinyi ni watu wa Mungu; mlikuwa wale ambao hawakuwa wameonyeshwa rehema, lakini sasa nyinyi ni wale ambao wameonyeshwa rehema.
11 Wapendwa, nawahimiza nyinyi kwa bidii mkiwa wakaaji wa kigeni na wakazi wa muda mfulize kujiepusha na tamaa za kimwili, ambazo zenyewe ndizo huendesha pambano dhidi ya nafsi. 12 Dumisheni mwenendo wenu ukiwa bora miongoni mwa mataifa, ili, katika jambo ambalo katika hilo wao wanasema dhidi yenu kuwa watenda-maovu, likiwa tokeo la kazi zenu bora ambazo wamekuwa mashahidi wa kujionea wapate kumtukuza Mungu katika siku ya ukaguzi wake.
13 Kwa ajili ya Bwana jitiisheni wenyewe kwa kila kilichoumbwa na binadamu: kama ni kwa mfalme akiwa mkubwa 14 au kwa magavana wakiwa wametumwa naye kupasisha adhabu juu ya watenda-maovu bali kusifu watenda-mema. 15 Kwa maana ndivyo mapenzi ya Mungu yalivyo, kwamba kwa kutenda mema mpate kufunga kinywa yale maongezi yasiyo na ujuzi ya watu wenye kukosa akili. 16 Iweni kama watu huru, na bado mkishika uhuru wenu, si kama kisetiri cha ubaya, bali kama watumwa wa Mungu. 17 Heshimuni watu wa namna zote, iweni na upendo kwa ushirika mzima wa ndugu, iweni katika kuhofu Mungu, iweni wenye kumheshimu mfalme.
18 Acheni watumishi wa nyumbani wawe katika ujitiisho kwa wamiliki wao kwa hofu yote istahiliyo, si kwa walio wema tu na wenye kukubali sababu, bali pia kwa wale ambao ni wagumu kupendeza. 19 Kwa maana ikiwa mtu fulani, kwa sababu ya dhamiri kuelekea Mungu, astahimili chini ya mambo yenye kuleta kihoro na ateseka isivyo haki, hili ni jambo lenye kukubalika. 20 Kwa maana kuna ustahili gani katika hilo ikiwa, mnapofanya dhambi na kupigwa makofi, mwalivumilia? Lakini ikiwa, mnapotenda mema na kuteseka, mwalivumilia, hili ni jambo lenye kukubalika kwa Mungu.
21 Kwa kweli, kwenye mwendo huu mliitwa, kwa sababu hata Kristo aliteseka kwa ajili yenu, akiwaachia kigezo ili nyinyi mfuate hatua zake kwa ukaribu. 22 Yeye hakufanya dhambi, wala udanganyo haukupatikana kinywani mwake. 23 Alipokuwa akitukanwa, hakuwa akitukana kwa kurudisha. Alipokuwa akiteseka, hakutisha, lakini alifuliza kujikabidhi mwenyewe kwa yeye ambaye huhukumu kwa uadilifu. 24 Yeye mwenyewe alichukua dhambi zetu katika mwili wake mwenyewe juu ya mti, ili tupate kuachana kabisa na dhambi na kuishi kuelekea uadilifu. Na “kwa mapigo yake mliponywa.” 25 Kwa maana mlikuwa kama kondoo, mkipotea njia; lakini sasa mmerudi kwa mchungaji na mwangalizi wa nafsi zenu.