1 Petro
3 Kwa namna kama hiyo, nyinyi wake, iweni katika ujitiisho kwa waume zenu wenyewe, ili, ikiwa wowote si watiifu kwa neno, wapate kuvutwa bila neno kupitia mwenendo wa wake zao, 2 kwa sababu wamekwisha kuwa mashahidi wa kujionea mwenendo wenu ulio safi kiadili pamoja na staha yenye kina kirefu. 3 Na msiache urembo wenu uwe ule wa kusuka nywele kwa nje na wa kuvalia madoido ya dhahabu au kuvalia mavazi ya nje, 4 bali acheni uwe yule mtu wa siri wa moyoni katika vao lisilofisidika la roho ya utulivu na ya upole, ambayo ni ya thamani kubwa machoni pa Mungu. 5 Kwa maana, pia, ndivyo wanawake watakatifu hapo zamani waliokuwa wakitumaini katika Mungu walivyokuwa na kawaida ya kujiremba, wakijitiisha wenyewe kwa waume zao wenyewe, 6 kama Sara alivyokuwa na kawaida ya kumtii Abrahamu, akimwita “bwana.” Nanyi mmekuwa watoto wake, mradi mwafuliza kutenda mema na kutohofu sababu yoyote ya ogofyo.
7 Nyinyi waume, endeleeni kukaa pamoja nao kwa namna kama hiyo kulingana na ujuzi, mkiwapa heshima kama chombo dhaifu zaidi, kile cha kike, kwa kuwa nyinyi pia ni warithi pamoja nao wa pendeleo lisilostahiliwa la uhai, kusudi sala zenu zisizuiwe.
8 Mwishowe, nyinyi nyote mwe wenye akili zenye kufanana, mkionyesha hisia-mwenzi, mkiwa na shauku ya kidugu, wenye huruma kwa njia ya wororo, wanyenyekevu katika akili, 9 mkiwa hamlipi ubaya kwa ubaya au tukano kwa tukano, bali, kinyume cha hivyo, mkitoa baraka, kwa sababu mliitwa kwenye mwendo huu, ili mpate kurithi baraka.
10 Kwa maana, “yeye ambaye angependa uhai na kuona siku zilizo njema, acheni azuie ulimi wake kutokana na lililo baya na midomo yake isiseme udanganyo, 11 lakini acheni ageuke mbali kutoka lililo baya na kufanya lililo jema; acheni atafute sana amani na kuifuatia. 12 Kwa maana macho ya Yehova yako juu ya waadilifu, na masikio yake yaelekea dua zao; bali uso wa Yehova uko dhidi ya wale wanaofanya mambo mabaya.”
13 Kwa kweli, ni nani huyo mtu ambaye atawadhuru nyinyi ikiwa mwawa wenye bidii kwa lililo jema? 14 Lakini hata mkiteseka kwa ajili ya uadilifu, nyinyi ni wenye furaha. Hata hivyo, kitu cha hofu yao nyinyi msikihofu, wala msiwe wenye kufadhaika. 15 Bali mtakaseni Kristo kuwa Bwana katika mioyo yenu, sikuzote mkiwa tayari kujitetea mbele ya kila mtu ambaye hudai kwenu sababu ya tumaini lililo katika nyinyi, lakini mkifanya hivyo kwa tabia-pole na staha yenye kina kirefu.
16 Iweni na dhamiri njema, ili katika jambo lile hasa ambalo lasemwa dhidi yenu waweze kupata kuaibika hao wanaosema kwa kushushia heshima mwenendo wenu mwema kuhusiana na Kristo. 17 Kwa maana ni bora kuteseka kwa sababu mnatenda mema, ikiwa mapenzi ya Mungu yataka hivyo, kuliko kwa sababu mnatenda ovu. 18 Naam, hata Kristo alikufa mara moja kwa wakati wote kuzihusu dhambi, mtu mwadilifu kwa ajili ya wasio waadilifu, ili apate kuwaongoza nyinyi kwa Mungu, yeye akiuawa katika mwili wenye nyama, lakini akifanywa kuwa hai katika roho. 19 Katika hali hiyo pia alienda akishika njia yake kwenda akawahubiria roho walio gerezani, 20 ambao wakati mmoja walikuwa wamekuwa wasiotii wakati subira ya Mungu ilipokuwa ikingoja katika siku za Noa, huku safina ilipokuwa ikijengwa, ambayo ndani yayo watu wachache, yaani, nafsi nane, walichukuliwa salama kupitia maji.
21 Lile ambalo hulingana na hili linaokoa nyinyi sasa pia, yaani, ubatizo, (si kule kuwekewa mbali kwa uchafu wenye kuchukiza wa mwili, bali ombi lifanywalo kwa Mungu ili kupata dhamiri njema,) kupitia ufufuo wa Yesu Kristo. 22 Yeye yuko kwenye mkono wa kuume wa Mungu, kwa maana alienda akishika njia yake kuelekea mbinguni; na malaika na mamlaka na nguvu vilifanywa kuwa vyenye kutiishwa kwake.