1 Petro
4 Kwa hiyo kwa kuwa Kristo aliteseka katika mwili, nyinyi pia jipatieni silaha kwa mwelekeo uleule wa akili; kwa sababu mtu ambaye ameteseka katika mwili ameachana kabisa na dhambi, 2 kwa madhumuni ya kwamba apate kuishi wakati wake uliobaki katika mwili, si tena kwa ajili ya tamaa za wanadamu, bali kwa ajili ya mapenzi ya Mungu. 3 Kwa maana wakati ambao umepita watosha kwenu kuwa mmefanyiza mapenzi ya mataifa wakati mlipoendelea katika vitendo vya mwenendo mlegevu, uchu, mazidio ya kunywa divai, sherehe zenye kelele za ulevi, mashindano ya kunywa, na ibada haramu za sanamu. 4 Kwa sababu nyinyi hamwendelei kukimbia pamoja nao katika mwendo huo kwenye dimbwi lilelile la chini la ufasiki, wao watatanishwa na kuendelea kuwasema nyinyi kwa maneno yenye kuudhi. 5 Lakini watu hao watatoa hesabu kwake yeye aliye tayari kuhukumu wale walio hai na wale walio wafu. 6 Kwa kweli, kwa kusudi hili habari njema ilitangazwa kwa wafu pia, ili wapate kuhukumiwa kuhusiana na mwili kwa maoni ya wanadamu lakini wapate kuishi kama kwa roho kwa maoni ya Mungu.
7 Lakini mwisho wa mambo yote umekaribia. Kwa hiyo, iweni timamu katika akili, na iweni wenye kukesha katika sala. 8 Juu ya mambo yote, iweni na upendo wenye juhudi nyingi nyinyi kwa nyinyi, kwa sababu upendo hufunika wingi wa dhambi. 9 Iweni wakaribishaji-wageni nyinyi kwa nyinyi bila kuguna. 10 Kwa kadiri ambayo kila mmoja amepokea zawadi, itumieni katika kuhudumiana kama wasimamizi-nyumba walio wema wa fadhili isiyostahiliwa ya Mungu iliyoonyeshwa katika njia mbalimbali. 11 Ikiwa yeyote asema, acheni aseme kama kwamba ni matamko matakatifu ya Mungu; ikiwa yeyote ahudumu, acheni ahudumu kama ategemeaye nguvu ambazo Mungu hutoa; ili katika mambo yote Mungu apate kutukuzwa kupitia Yesu Kristo. Utukufu na uweza ni wake milele na milele. Ameni.
12 Wapendwa, msitatanishwe juu ya kuwaka miongoni mwenu, ambako kunatukia kwenu kuwa jaribu, kama kwamba jambo geni linawapata. 13 Kinyume cha hivyo, endeleeni kushangilia kwa maana nyinyi ni washiriki katika mateso ya Kristo, ili mpate kushangilia na kuwa na shangwe mno pia wakati wa ufunuo wa utukufu wake. 14 Ikiwa mnashutumiwa kwa ajili ya jina la Kristo, nyinyi ni wenye furaha, kwa sababu roho ya utukufu, naam, roho ya Mungu, inatulia juu yenu.
15 Hata hivyo, acheni mmoja wenu asiteseke akiwa muuaji-kimakusudi au mwizi au mtenda-maovu au akiwa mjishughulishaji katika mambo ya watu wengine. 16 Lakini ikiwa ateseka akiwa Mkristo, acheni asione aibu, bali acheni afulize kumtukuza Mungu katika jina hili. 17 Kwa maana ni wakati uliowekwa rasmi kwa hukumu kuanza na nyumba ya Mungu. Sasa ikiwa yaanza na sisi kwanza, utakuwa nini mwisho wa wale wasio watiifu kwa habari njema ya Mungu? 18 “Na ikiwa ni kwa shida mtu mwadilifu anaokolewa, mtu asiyemwogopa Mungu na mtenda-dhambi wataonekana wapi?” 19 Kwa hiyo, basi, acheni wale wanaoteseka kwa kupatana na mapenzi ya Mungu wafulize kukabidhi nafsi zao kwa Muumba mwaminifu wanapotenda mema.