1 Petro
5 Kwa hiyo, kwa wanaume wazee miongoni mwenu natoa himizo hili lenye bidii, kwa kuwa mimi pia ni mwanamume mzee pamoja nao na shahidi wa mateso ya Kristo, mshiriki hata wa utukufu utakaofunuliwa: 2 Lichungeni kundi la Mungu lililo katika utunzaji wenu, si kwa kushurutishwa, bali kwa nia ya kupenda; wala si kwa kupenda pato lisilo la haki, bali kwa hamu; 3 wala si kama kwa kupiga ubwana juu ya wale ambao ni urithi wa Mungu, bali mwe vielelezo kwa kundi. 4 Na mchungaji mkuu akiisha kuwa amefanywa dhahiri, mtapokea taji la utukufu lisiloweza kufifia.
5 Kwa namna kama hiyo, nyinyi wanaume vijana zaidi, iweni katika ujitiisho kwa wanaume wazee. Lakini nyinyi nyote jifungeni hali ya akili ya kujishusha chini kuelekea mtu na mwenzake, kwa sababu Mungu hupinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu fadhili isiyostahiliwa.
6 Kwa hiyo, jinyenyekezeni chini ya mkono wa Mungu wenye uweza, ili apate kuwakweza nyinyi katika wakati upasao; 7 huku mkitupa hangaiko lenu lote juu yake, kwa sababu yeye huwajali nyinyi. 8 Tunzeni akili zenu, iweni wenye kulinda. Mpinzani wenu, Ibilisi, hutembea huku na huku kama simba anayenguruma, akitafuta sana kunyafua mtu fulani. 9 Lakini chukueni msimamo wenu dhidi yake, mkiwa thabiti katika imani, mkijua kwamba mambo yaleyale kwa njia ya mateso yanatimizwa katika ushirika mzima wa ndugu zenu katika ulimwengu. 10 Lakini, mkiisha kuteseka muda kidogo, Mungu wa fadhili yote isiyostahiliwa, ambaye aliwaita nyinyi kwenye utukufu wake udumuo milele katika muungano na Kristo, yeye mwenyewe atamaliza mazoezi yenu, atawafanya imara, atawafanya kuwa wenye nguvu. 11 Kwake na kuwe uweza milele. Ameni.
12 Kupitia Silvano, ndugu mwaminifu, kama vile namhesabu yeye, nimewaandikia nyinyi katika maneno machache, kutoa kitia-moyo na ushahidi wa bidii kwamba hii ndiyo fadhili isiyostahiliwa ya Mungu iliyo ya kweli; katika hiyo simameni imara. 13 Mwanamke ambaye yuko Babiloni, mchaguliwa kama nyinyi, apeleka kwenu salamu zake, na ndivyo afanyavyo Marko mwanangu. 14 Salimianeni kwa busu la upendo.
Na mwe na amani nyinyi nyote mlio katika muungano na Kristo.