Ufunuo
8 Na alipofungua muhuri wa saba, kimya kikatukia mbinguni kwa karibu nusu saa. 2 Nami nikaona malaika saba wasimamao mbele ya Mungu, nao wakapewa tarumbeta saba.
3 Na malaika mwingine akawasili na kusimama kwenye madhabahu, akiwa na chombo cha uvumba cha dhahabu; naye akapewa kiasi kikubwa cha uvumba akitoe pamoja na sala za watakatifu wote juu ya madhabahu ya dhahabu ambayo ilikuwa mbele ya kiti cha ufalme. 4 Na moshi wa huo uvumba ukapanda kutoka katika mkono wa huyo malaika pamoja na sala za watakatifu mbele ya Mungu. 5 Lakini saa hiyohiyo huyo malaika akachukua chombo cha uvumba, akakijaza baadhi ya moto wa madhabahu na kukivurumisha kwenye dunia. Na ngurumo zikatukia na sauti na meme na tetemeko la dunia. 6 Na wale malaika saba wenye tarumbeta saba wakajitayarisha kuzipuliza.
7 Na wa kwanza akapuliza tarumbeta yake. Na kulitukia mvua ya mawe na moto uliochangamana na damu, nao ukavurumishwa kwenye dunia; na theluthi moja ya dunia ikachomwa kabisa, na theluthi moja ya miti ikachomwa kabisa, na mimea yote ya kijani kibichi ikachomwa kabisa.
8 Na malaika wa pili akapuliza tarumbeta yake. Na kitu fulani kama mlima mkubwa unaowaka moto kikavurumishwa ndani ya bahari. Na theluthi moja ya bahari ikawa damu; 9 na theluthi moja ya viumbe vilivyomo katika bahari vilivyo na nafsi ikafa, na theluthi moja ya mashua ikavunjwa-vunjwa.
10 Na malaika wa tatu akapuliza tarumbeta yake. Na nyota kubwa inayowaka kama taa ikaanguka kutoka mbinguni, nayo ikaanguka juu ya theluthi moja ya mito na juu ya mabubujiko ya maji. 11 Na jina la hiyo nyota laitwa Pakanga. Na theluthi moja ya maji ikageuka kuwa pakanga, na wengi kati ya wanadamu wakafa kutokana na hayo maji, kwa sababu yalikuwa yamefanywa kuwa machungu.
12 Na malaika wa nne akapuliza tarumbeta yake. Na theluthi moja ya jua ikapigwa na theluthi moja ya mwezi na theluthi moja ya nyota, ili theluthi moja ya hizo ipate kutiwa giza, na mchana usipate kuwa na mmuliko kwa theluthi moja ya huo, na usiku hivyohivyo.
13 Nami nikaona, nami nikasikia tai akiruka katika mbingu ya kati akisema kwa sauti kubwa: “Ole, ole, ole wao wanaokaa juu ya dunia kwa sababu ya mipulizo mingine ya tarumbeta ya malaika watatu walio karibu kupuliza tarumbeta zao!”