Ufunuo
7 Baada ya hili nikaona malaika wanne wamesimama juu ya pembe nne za dunia, wakiwa wameshika sana pepo nne za dunia, ili upepo wowote usipate kuvuma juu ya dunia au juu ya bahari au juu ya mti wowote. 2 Nami nikaona malaika mwingine akipanda kutoka macheo ya jua, akiwa na muhuri wa Mungu aliye hai; naye akalia kwa sauti kubwa kwa wale malaika wanne waliopewa ruhusa kudhuru dunia na bahari, 3 akisema: “Msidhuru dunia au bahari au miti, mpaka baada ya sisi tuwe tumetia muhuri watumwa wa Mungu wetu katika vipaji vya nyuso zao.”
4 Nami nikasikia idadi ya wale waliotiwa muhuri, mia arobaini na nne elfu, waliotiwa muhuri kutoka katika kila kabila la wana wa Israeli:
5 Kutoka katika kabila la Yuda kumi na mbili elfu waliotiwa muhuri;
kutoka katika kabila la Reubeni kumi na mbili elfu;
kutoka katika kabila la Gadi kumi na mbili elfu;
6 kutoka katika kabila la Asheri kumi na mbili elfu;
kutoka katika kabila la Naftali kumi na mbili elfu;
kutoka katika kabila la Manase kumi na mbili elfu;
7 kutoka katika kabila la Simeoni kumi na mbili elfu;
kutoka katika kabila la Lawi kumi na mbili elfu;
kutoka katika kabila la Isakari kumi na mbili elfu;
8 kutoka katika kabila la Zebuloni kumi na mbili elfu;
kutoka katika kabila la Yosefu kumi na mbili elfu;
kutoka katika kabila la Benyamini kumi na mbili elfu waliotiwa muhuri.
9 Baada ya mambo haya nikaona, na, tazama! umati mkubwa, ambao hakuna mtu aliyeweza kuuhesabu, kutoka katika mataifa yote na makabila na vikundi vya watu na lugha, wamesimama mbele ya kiti cha ufalme na mbele ya Mwana-Kondoo, wamevaa kanzu nyeupe; na kulikuwa na matawi ya mitende mikononi mwao. 10 Nao wafuliza kulia kwa sauti kubwa, wakisema: “Sisi tunawiwa wokovu na Mungu wetu, aketiye juu ya hicho kiti cha ufalme, na kwa Mwana-Kondoo.”
11 Na malaika wote walikuwa wamesimama kuzunguka hicho kiti cha ufalme na wale wazee na wale viumbe hai wanne, nao wakaanguka kifudifudi mbele ya kiti cha ufalme na kumwabudu Mungu, 12 wakisema: “Ameni! Baraka na utukufu na hekima na utoaji-shukrani na heshima na uwezo na nguvu ziwe kwa Mungu wetu milele na milele. Ameni.”
13 Na kwa kujibu mmoja wa wale wazee akaniambia: “Hawa waliovaa kanzu nyeupe, wao ni nani nao walitoka wapi?” 14 Kwa hiyo saa hiyohiyo nikamwambia: “Bwana wangu, wewe ndiwe ujuaye.” Naye akaniambia: “Hawa ndio wale watokao katika dhiki kubwa, nao wamefua kanzu zao na kuzifanya nyeupe katika damu ya Mwana-Kondoo. 15 Hiyo ndiyo sababu wako mbele ya hicho kiti cha ufalme cha Mungu; nao wanamtolea utumishi mtakatifu mchana na usiku katika hekalu lake; na Yeye aketiye juu ya kiti cha ufalme atatandaza hema lake juu yao. 16 Hawatakuwa na njaa tena wala kuwa na kiu tena kamwe, wala jua halitawapiga wala joto lolote lenye kuunguza, 17 kwa sababu Mwana-Kondoo, ambaye yuko katikati ya kiti cha ufalme, atawachunga, na kuwaongoza kwenye mabubujiko ya maji ya uhai. Na Mungu atafuta kabisa kila chozi kutoka katika macho yao.”