Ufunuo
6 Nami nikaona Mwana-Kondoo alipofungua mmoja wa mihuri saba, nami nikasikia mmoja kati ya wale viumbe hai wanne akisema kwa sauti kama ya ngurumo: “Njoo!” 2 Nami nikaona, na, tazama! farasi mweupe; na yeye aketiye juu yake alikuwa na upinde; naye akapewa taji, naye akaenda akishinda na kukamilisha ushindi wake.
3 Na alipofungua muhuri wa pili, nikasikia kiumbe hai wa pili akisema: “Njoo!” 4 Na mwingine akatokea, farasi mwenye rangi-moto; na kwa yeye aketiye juu yake akapewa ruhusa kuondolea mbali amani katika dunia ili wachinjane; naye akapewa upanga mkubwa.
5 Na alipofungua muhuri wa tatu, nikasikia kiumbe hai wa tatu akisema: “Njoo!” Nami nikaona, na, tazama! farasi mweusi; na yeye aketiye juu yake alikuwa na jozi ya mizani mkononi mwake. 6 Nami nikasikia sauti kama kwamba ni katikati ya wale viumbe hai wanne ikisema: “Kisaga cha ngano kwa dinari moja, na visaga vitatu vya shayiri kwa dinari moja; na usidhuru mafuta ya zeituni na divai.”
7 Na alipofungua muhuri wa nne, nikasikia sauti ya kiumbe hai wa nne akisema: “Njoo!” 8 Nami nikaona, na, tazama! farasi wa rangi ya kijivujivu; na yeye aketiye juu yake alikuwa na jina Kifo. Na Hadesi ilikuwa ikimfuata karibu-karibu. Nao walipewa mamlaka juu ya sehemu ya nne ya dunia, ili kuua kwa upanga mrefu na kwa upungufu wa chakula na kwa tauni ya kufisha na kwa mahayawani-mwitu wa dunia.
9 Na alipofungua muhuri wa tano, nikaona chini ya madhabahu nafsi za wale waliochinjwa kwa sababu ya neno la Mungu na kwa sababu ya kazi ya ushahidi iliyokuwa kawaida yao. 10 Nazo zikalia kwa sauti kubwa, zikisema: “Ni hadi wakati gani, Bwana Mwenye Enzi Kuu mtakatifu na wa kweli, utajiepusha kuhukumu na kulipizia kisasi damu yetu juu ya wale wakaao juu ya dunia?” 11 Na kila mmoja wao akapewa kanzu nyeupe; nao wakaambiwa wapumzike muda kidogo zaidi, mpaka idadi iwe imejazwa pia ya watumwa wenzao na ndugu zao waliokuwa karibu kuuawa kama wao pia walivyokuwa wameuawa.
12 Nami nikaona alipofungua muhuri wa sita, na tetemeko kubwa la dunia likatukia; na jua likawa jeusi kama gunia la nywele, na mwezi mzima ukawa kama damu, 13 na nyota za mbinguni zikaanguka kwenye dunia, kama wakati mtini utikiswao na upepo mkali upukusapo tini zake zisizoiva. 14 Na mbingu ikaondoka kama hati-kunjo inayoviringishwa, na kila mlima na kila kisiwa vikaondolewa mahali pavyo. 15 Na wafalme wa dunia na wenye daraja la juu na makamanda wa kijeshi na matajiri na wenye nguvu na kila mtumwa na kila mtu huru wakajificha wenyewe katika mapango na katika matungamo-miamba ya milima. 16 Nao wafuliza kuiambia milima na matungamo-miamba: “Tuangukieni mtufiche kutoka uso wa Yeye aketiye juu ya hicho kiti cha ufalme na kutoka hasira ya kisasi ya Mwana-Kondoo, 17 kwa sababu siku kubwa ya hasira ya kisasi yao imekuja, na ni nani awezaye kusimama?”