Ufunuo
5 Nami nikaona katika mkono wa kuume wa Yeye aketiye juu ya hicho kiti cha ufalme hati-kunjo iliyoandikwa ndani na upande wa nyuma, imefungwa kwa kukazwa kwa mihuri saba. 2 Nami nikaona malaika mwenye nguvu akipiga mbiu kwa sauti kubwa: “Nani anastahili kuifungua hati-kunjo na kufungua mihuri yayo?” 3 Lakini wala mbinguni wala juu ya dunia wala chini ya dunia hakukuwako hata mmoja awezaye kufungua hiyo hati-kunjo au kutazama ndani yayo. 4 Nami nikatokwa na machozi kwa wingi kwa sababu hakuna yeyote aliyepatikana kuwa astahili kufungua hiyo hati-kunjo au kutazama ndani yayo. 5 Lakini mmoja kati ya wale wazee aniambia: “Acha kutoa machozi. Tazama! Simba ambaye ni wa kabila la Yuda, mzizi wa Daudi, ameshinda ili kuifungua hati-kunjo na mihuri saba yayo.”
6 Nami nikaona amesimama katikati ya kiti cha ufalme na ya wale viumbe hai wanne na katikati ya wale wazee mwana-kondoo kama kwamba alikuwa amechinjwa, mwenye pembe saba na macho saba, macho ambayo yamaanisha roho saba za Mungu ambazo zimetumwa kuingia katika dunia nzima. 7 Naye akaenda na mara moja akaichukua kutoka katika mkono wa kuume wa Yeye aketiye juu ya hicho kiti cha ufalme. 8 Na wakati alipochukua hiyo hati-kunjo, wale viumbe hai wanne na wale wazee ishirini na wanne walianguka chini mbele ya Mwana-Kondoo, kila mmoja akiwa na kinubi na mabakuli ya dhahabu yaliyokuwa yamejaa uvumba, na huo uvumba wamaanisha sala za watakatifu. 9 Nao waimba wimbo mpya, wakisema: “Wewe wastahili kuchukua hiyo hati-kunjo na kufungua mihuri yayo, kwa sababu ulichinjwa na kwa damu yako ukanunua watu kwa ajili ya Mungu kutoka kila kabila na ulimi na watu na taifa, 10 nawe ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu, nao watatawala wakiwa wafalme juu ya dunia.”
11 Nami nikaona, nami nikasikia sauti ya malaika wengi kuzunguka hicho kiti cha ufalme na wale viumbe hai na wale wazee, na idadi yao ilikuwa makumi ya maelfu ya makumi ya maelfu na maelfu ya maelfu, 12 wakisema kwa sauti kubwa: “Mwana-Kondoo aliyechinjwa astahili kupokea uwezo na utajiri na hekima na nguvu na heshima na utukufu na baraka.”
13 Na kila kiumbe kilichomo mbinguni na juu ya dunia na chini ya dunia na juu ya bahari, na vitu vyote ndani yavyo, nikasikia vikisema: “Kwake Yeye anayekaa juu ya hicho kiti cha ufalme na kwa Mwana-Kondoo kuwe na baraka na heshima na utukufu na uweza milele na milele.” 14 Na wale viumbe hai wanne wakaanza kusema: “Ameni!” na wale wazee wakaanguka chini na kuabudu.