Ufunuo
4 Baada ya mambo haya nikaona, na, tazama! mlango uliofunguliwa mbinguni, na sauti ya kwanza niliyoisikia ilikuwa kama ya tarumbeta, ikisema nami, ikiniambia: “Panda uje huku, nami nitakuonyesha mambo ambayo lazima yatukie.” 2 Baada ya mambo haya mara nikaja kuwa katika nguvu ya roho: na, tazama! kiti cha ufalme kilikuwa katika mahali pacho mbinguni, na kuna yule aketiye juu ya kiti cha ufalme. 3 Na yeye aliyeketi, kwa kuonekana, ni kama jiwe la yaspi na jiwe la rangi nyekundu lenye bei, na kuzunguka hicho kiti cha ufalme kuna upinde-mvua kama zumaridi katika kuonekana.
4 Na kuzunguka hicho kiti cha ufalme kuna viti vya ufalme ishirini na vinne, na juu ya hivyo viti vya ufalme niliona wameketi wazee ishirini na wanne wakiwa wamevaa mavazi meupe ya nje, na juu ya vichwa vyao mataji ya dhahabu. 5 Na meme na sauti na ngurumo zinatoka katika hicho kiti cha ufalme; na kuna taa saba za moto zenye kuwaka mbele ya hicho kiti cha ufalme, na hizi zamaanisha roho saba za Mungu. 6 Na mbele ya hicho kiti cha ufalme kuna, kama kwamba, bahari yenye kufanana na kioo kama fuwele.
Na katikati ya hicho kiti cha ufalme na kuzunguka kiti cha ufalme kuna viumbe hai wanne wenye kujaa macho mbele na nyuma. 7 Na kiumbe hai wa kwanza ni kama simba, na kiumbe hai wa pili ni kama fahali mchanga, na kiumbe hai wa tatu ana uso kama wa mwanadamu, na kiumbe hai wa nne ni kama tai anayeruka. 8 Na kwa habari ya wale viumbe hai wanne, kila mmoja wao peke yake ana mabawa sita; kuwazunguka na chini yao wamejaa macho. Nao hawana pumziko lolote mchana na usiku wasemapo: “Mtakatifu, mtakatifu, mtakatifu ni Yehova Mungu, Mweza-Yote, aliyekuwako na aliyeko na anayekuja.”
9 Na wakati wowote hao viumbe hai wamtoleapo utukufu na heshima na utoaji-shukrani Yeye aketiye juu ya hicho kiti cha ufalme, yeye aliye hai milele na milele, 10 wale wazee ishirini na wanne huanguka chini mbele ya Yeye aketiye juu ya hicho kiti cha ufalme na kumwabudu Yeye aliye hai milele na milele, nao watupa mataji yao mbele ya hicho kiti cha ufalme, wakisema: 11 “Wewe wastahili, Yehova, naam, Mungu wetu, kupokea utukufu na heshima na nguvu, kwa sababu uliumba vitu vyote, na kwa sababu ya mapenzi yako vilikuwako na vikaumbwa.