Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g90 10/8 uku. 30
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1990
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • MIKAWIZO GHALI
  • KUSHINDA NA KUSHINDWA
  • ARUSI ZAUZWA
  • NZIGE WA MASAFA MAREFU
  • “MWUAJI MKUBWA KULIKO UKIMWI”
  • MSTADI WA KUCHUNGUZA MAJI
  • Ole wa Kwanza—Nzige
    Ufunuo—Upeo Wao Mtukufu U Karibu!
  • Utiaji-damu Mishipani—Ni Salama Kadiri Gani?
    Damu Yaweza Kuokoaje Uhai Wako?
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1997
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1994
Amkeni!—1990
g90 10/8 uku. 30

Kuutazama Ulimwengu

MIKAWIZO GHALI

Mikawizo ya kuchelewa kwa ndege katika Ulaya hukadiriwa kugharimu mashirika ya ndege na abiria wao dola milioni elfu 4 kwa mwaka, kulingana na ripoti moja kutoka German Airspace Users Association. Ripoti hiyo yashikilia kwamba sababu ya matatizo hayo ni utumizi mbaya wa nafasi ya anga. Ulaya ina vitovu 44 vya udhibiti wa ndege, kwa kulinganishwa na 20 vilivyopo kwa United States nzima. Kufanyiza mfumo mmoja tu uliounganishwa pamoja wa kudhibiti ndege angani kwa ajili ya Ulaya nzima kungegharimu kati ya dola milioni elfu 5 na dola milioni elfu 10, lakini utumizi huo wa pesa ungekuwa ni kama umeondoa kabisa mikawizo yote iliyopo ya kudhibiti ndege angani, lasema Financial Times la London. Ukosefu uliopo wa uratibishaji mzuri hufanya ndege zipewe kiasi kisichotosha cha kimo na njia ya kurukia, hiyo ikifanya safari ya kawaida ya ndege kuruka Ulaya irefuke kwa asilimia 10 kuliko ihitajiwavyo.

KUSHINDA NA KUSHINDWA

Chini ya kichwa “Kupata Bahati Kwaweza Kuleta Msiba,” gazeti la Kibrazili O Estado de São Paulo liliripoti juu ya msiba uliopata mtu aliyeshinda mchezo wa nasibu huko. Akiwa ndiye mshindi pekee wa mchezo wa nasibu, alipokea Novos Cruzados 930,000 (karibu dola 400,000 za United States). Hata hivyo, baadaye mwanamume huyo alipokea pia habari za kuhuzunisha kwamba watu watatu wa ukoo wake waliuawa na wevi waliokuwa wakitafuta baadhi ya pesa za tuzo la mchezo wa nasibu.

ARUSI ZAUZWA

Watalii Wajapani wenye kusafiri kwenda Ulaya wameweza kununua vifurushi vya utalii vyenye arusi za kanisa Katoliki pia ndani yavyo. Kujapokuwa na mateteo kutoka Vatikani dhidi ya “kufanya biashara na desturi takatifu ya ndoa,” hesabu inayoongezeka ya waume na wake Wajapani wasio Wakatoliki “wamefanya sherehe ya ndoa makanisani katika Italia na Ufaransa,” laripoti The Daily Yomiuri. Vatikani imeudhika kwa sababu mapadri wayo waelekezwa wafanye arusi kwa ajili ya Wakatoliki Waroma tu au wale ambao wamepokea maagizo katika imani ya Kikatoliki. Hata hivyo, mashirika ya Kijapani ya usafiri yaliweza kuepa mwongozo wa kanisa kwa kuchagua “makanisa yasiyofuatilia sana sheria ili yafanye arusi hizo.”

NZIGE WA MASAFA MAREFU

Mwaka uliopita, wakati nzige wahamaji milioni mia moja walipovamia visiwa vya Carribea, Guyana, na Venezuela, hiyo ilizusha swali miongoni mwa wataalamu: “Nzige wangaliwezaje kufanikiwa kuivuka Bahari Kuu Atlantiki?” Hapo mbele wadudu hao hawakujulikana kwenye sehemu hizo za ulimwengu. Safari hiyo ya siku nne hadi sita, kwa umbali wa kuanzia kilometa 4,000 hadi 4,800, ilikuwa kitendo hodari mtu afikiriapo kwamba nzige wahamaji kwa kawaida huruka wakati wa mchana, urukaji wao ukiwa rahisi zaidi katika hewa yenye joto. Wao hutua wakati hewa iingiapo baridi jioni-jioni. Kulingana na gazeti la Kifaransa Le Monde, watafiti wakata shauri kwamba labda nzige hao walibaki angani wakati wa mruko wao wa kuvuka Atlantiki, kwa maana hawakuwa na kitu cha kutulia wala cha kula. Hata hivyo, wao wana uhakika juu ya jambo moja, kwamba wadudu walioangamia baharini ni wengi kuliko waliookoka mvuko wa hiyo bahari kuu.

“MWUAJI MKUBWA KULIKO UKIMWI”

Baada ya kuchunguza ugonjwa wa ini kwa miaka 15, mkurugenzi ambaye hufanya utafiti wa kikliniki kwa ajili ya hospitali moja kubwa katika Australia alionya hivi majuzi kwamba ugonjwa wa mchochota-ini ni “mwuaji aliye mkubwa sana hata kuliko UKIMWI.” Aliongezea hivi: “Yakadiriwa kwamba karibu watu milioni mbili hufa kwa mwaka kutokana na ugonjwa wa mchochota-ini na kwa kadiri mimi nijuavyo UKIMWI bado haujafikia kiasi hicho.” Yeye awaweka watu chonjo juu ya ile vairasi hatari ya ugonjwa wa mchochota-ini wa aina ya “C,” ambao hushambulia ini na ambao kufikia sasa hauna njia ya kuugundulia. Watafiti huamini kwamba kila mwaka kati ya watu 10 na 15 hufa katika Australia kutokana na ugonjwa wa mchochota-ini wa aina ya “C” kwa kuupata kutokana na kutiwa mishipani damu yenye viini vibaya. The Australian, ambalo ni gazeti la Sydney, laripoti kwamba mfuko 1 kati ya 400 ya damu ambayo hutumiwa kutia damu mishipani katika Australia ina viini vibaya vya ule ugonjwa hatari wa mchochota-ini wa aina ya “C.”

MSTADI WA KUCHUNGUZA MAJI

“Njia bora kabisa ya kuchunguza maji ni kuleta mstadi,” lasema tangazo moja la Mamlaka Inayohusiana na Maji katika Wales. Ingawa hivyo, mstadi huyo ni samaki—yule troti-upinde-mvua wa hali ya chini. Kwa asili samaki hugundua kwa urahisi ikiwa maji yana uchafuzi. Wapumuapo, vishimo vya hewa shavuni huwasha mikondo midogo sana ya umeme. Uchafuzi huvuruga upumuaji huo na pia ile mikondo. Wakati mikondo hiyo ya umeme ibadilikapo-badilikapo, kompyuta yaweza kujua na kuirekebi hali hiyo. Ofisa mmoja wa Kitovu cha Utafiti wa Maji Uingereza asema kwamba troti “atagundua pia na kukuonya juu ya vitu fulani ambavyo wewe hujapata hata kuviwazia, na hiyo ni faida kubwa.” Kulingana na The Times la London, sasa mbinu hii ya kurekebi hali inavutia upendezi wa kimataifa wala si wa kitaifa tu.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki