Utofautiano Wenye Tokeo la Kinyumenyume
ONGEZEKO kubwa ulimwenguni pote la idadi ya watu linatarajiwa kuongeza idadi ya watu wanaokaribia kulingana na jumla ya watu wote wa China wakati wa miaka ya 1990. Ongezeko hilo linaathiri hasa majiji ya ulimwengu. Kwa uhakika, katika miaka 15 ijayo, wenyeji wa majiji ya sayari hii wanatazamiwa kuzidi idadi kupita wale wa mashambani kwa mara ya kwanza. Gazeti International Wildlife linasema kwamba majiji ya ulimwengu yanapofurika kuwa majiji ya mamilioni ya watu, ‘yanaharibu hewa na maji, hunyakua kwa pupa ardhi ya kilimo inayozunguka, humaliza misitu ili kuandaa viwashio na miti, na kukuza uhalifu, magonjwa na mtamauko.’
Wakati ule ule, sehemu nyingi zaidi na zaidi za mashambani zinahamwa. Kwa mfano, katika United States, kuna mamia ya miji mashambani inayokufa kwa ukosefu wa watu. Katika Nyika Kubwa magharibi mwa United States, nchi fulani sasa zina miji mingi iliyo mitupu kuliko ile iliyo na watu. Nchi kumi katika Dakota Kaskazini zina watu wanne tu au wachache zaidi kwa kila kilometa ya mraba; nchi 18 zimepoteza angalau asimilia 50 ya idadi zao za watu tangu 1930. Wengine hata huhisi, kama ambavyo The Wall Street Journal lilivyosema, kwamba sehemu yote ya Nyika Kuu sasa “pasipo kuepukika inarudia ile hali ya kwanza ya kuwa na nyasinyasi.” Kwa nini? Wastadi wanalaumu kutokusimamia vema ardhi, kutumia vibaya maji yaliyo nadra, ukame na uchumi uliodhoofika.
Majiji yenye umayamaya wa watu yakifurika kabisa. Mbuga pana zenye miji mingi iliyohamwa. Katika utofautiano huo wenye tokeo la kinyumenyume kuna ithibati kwamba mwanadamu hatawali eneo la mashambani vema kuliko miji, wala hatawali sayari hii vema kuliko vile atawalavyo watu wayo. Kama ambavyo Biblia huweka jambo hilo kwa kufaa: “Kuelekeza hatua zake si katika uwezo wa mwanadamu.” (Yeremia 10:23) Lakini serikali yenye uwezo na haki haipiti uwezo wa Muumba wa binadamu. Yeye ameahidi kwamba karibuni sasa dunia nzima itatoa mazao, ikilimwa na wenyeji wenye amani badala ya kuharibiwa na wapangaji wasio na usawaziko.—Zaburi 67:6; 72:16; Isaya 65:21-23.