Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g92 7/8 kur. 3-5
  • Familia Karibianeni Kabla Haijawa Kuchelewa Mno

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Familia Karibianeni Kabla Haijawa Kuchelewa Mno
  • Amkeni!—1992
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Zitatusumbua Tena na Tena
  • Takataka Ndani, Takataka Nje
  • Kuwalinda Watoto Wetu na Magenge
    Amkeni!—1998
  • Familia—Binadamu Wanaihitaji!
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1998
  • Kutumia Neno la Mungu Katika Jamaa Zetu Wenyewe
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1976
  • Ilinde Familia Yako Dhidi ya Mavutano Yaletayo Uharibifu
    Siri ya Furaha ya Familia
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1992
g92 7/8 kur. 3-5

Familia Karibianeni Kabla Haijawa Kuchelewa Mno

“Jamaa ndicho chama cha kibinadamu ambacho ni cha kale sana kuliko vyote. Ndicho cha maana kuliko vyote katika njia nyingi. Ndio msingi wa jamii ya watu. Mambo yote ya ustaarabu yameendelea au yakatoweka, yakitegemea nguvu au udhaifu wa maisha ya jamaa.”—The World Book Encyclopedia (Chapa ya 1973).

FAMILIA ni mwavuli wa ulinzi kwa watoto. Katika sehemu nyingi leo, mwavuli huo umejawa na matundu; katika mahali pengine pengi, unafungwa na kuwekwa kabatini. Familia ya zamani mara nyingi huachiliwa mbali kuwa isiyo ya mtindo wa kisasa. Vipindi vya televisheni vya ucheshi mara nyingi huonyesha akina baba kuwa mabaradhuli, akina mama kuwa welekevu, lakini watoto wajua zaidi.

Uzinzi katika ndoa umeenea sana. Katika nchi nyingi zenye kusitawi, moja kati ya kila ndoa mbili humalizikia katika talaka. Kadiri talaka zinavyoongezeka, ndivyo familia zenye mzazi mmoja zinavyozidi. Katika hesabu zenye kuongezeka, wawili wanakuwa kitu kimoja bila faida ya ndoa. Wagoni jinsia-moja hutafuta kuutukuza uhusiano wao kwa viapo vya ndoa. Ngono, ya kawaida na isiyo ya kawaida, ndiyo hukaziwa sana katika sinema na video. Shule huona usafi wa kiadili kuwa usiofaa na hupeana kondomu ili kufanya uasherati uwe salama—na kondomu hizo haziufanyi uwe salama. Magonjwa ya kuambukiza kingono na mimba za matineja huongezeka kwa kiwango cha juu sana. Wanaopatwa na hayo ni watoto—ikiwa wanaruhusiwa kuzaliwa. Familia ya zamani ikiwa imepotelea mbali, watoto ndio wanaopatwa na hasara.

Miaka iliyopita, mshindi wa zawadi ya Nobeli Alexis Carel, katika kitabu chake Man, the Unknown, alitoa onyo hili: “Jamii ya ki-siku-hizi imefanya kosa kubwa sana kwa kuruhusu shule ichukue mahali pa mazoezi ya kifamilia. Akina mama wanaacha watoto wao kwenye chuo cha watoto wadogo [sasa, kukiwa na vituo vya utunzi wa mchana na nasari] ili washughulikie kazi-maisha zao, fahari zao za kijamii, raha zao za kingono, mapendezi yao ya kichuo au ya kisanii, au kucheza mchezo wa karata tu, kwenda sinemani, na kupoteza wakati wao wakiwa wazembe wenye shughuli nyingi. Hivyo, basi, wanahusika katika kupotea kwa kikundi cha familia ambapo mtoto alikuwa na ukaribu sana pamoja na watu wazima na akajifunza mambo mengi sana kutoka kwao. . . . Ili kufikia uwezo wake kamili, mtu mmoja mmoja anahitaji kule kutengwa kwa kadiri na ule uangalifu wa kikundi kidogo cha kijamii kinachofanyiza familia.”—Ukurasa 176.

Hivi karibuni, mwigizaji wa michezo ya ucheshi Steve Allen alisema juu ya shambulio la televisheni juu ya familia, ikishughulikia sana lugha chafu na ukosefu wa adili. Yeye alisema: “Mtiririko huo unatupeleka hadi kwenye uchafu mwingi. Aina ile ile ya lugha ambayo wazazi wanakataza watoto wao wasitumie ndiyo sasa inayotiwa moyo si na wasambazaji programu za aina yoyote tu kupitia nyuzi za simu bali na stesheni zilizokuwa zenye kanuni za juu sana wakati mmoja. Programu zinazoonyesha watoto na wengine wakitumia lugha ya matusi huonyesha tu poromoko la familia ya Kiamerika.”

Ni urithi gani ambao jamii inaachia watoto wayo? Soma magazeti, tazama televisheni, angalia video, fungulia habari za jioni, sikiliza muziki wenye kudundadunda, ona mifano ya watu wazima kila mahali kukuzunguka. Akili na hisia za watoto zinajawa na mambo yasiyofaa. “Ikiwa unataka kuharibu nchi,” akasema Bwana Keith Joseph, aliyekuwa mwandishi wa elimu wa Uingereza, “fisidi fedha zayo.” Na akaongezea: “Njia ya kuharibu jamii ni kufisidi watoto.” “Kufisidi” kulingana na Webster’s humaanisha “kupotoa kutoka maadili na ubora.” Hilo lafanywa kwa kisasi leo. Mengi yanasemwa kuhusu uhalifu wa watoto; mengi zaidi yapasa kusemwa kuhusu uhalifu wa watu wazima.

Zitatusumbua Tena na Tena

Geneva B. Johnson, msimamizi na ofisa mtendaji mkuu wa Family Service America (Utumishi wa Familia Amerika), alisema katika hotuba iliyotolewa mapema mwaka huu: “Familia ni gonjwa sana, labda kiasi cha kufa.” Akiita hiyo kuwa “hali yenye kuogopesha kwa wengi wa watoto wetu,” ndipo aliposema kwa kutazamia mabaya: “Nia ya taifa ya kuwapa waliotupwa katika jamii iliyo tajiri daraka la kutunza watoto wetu wengi sana wasio na makao mazuri, chakula kizuri, itatusumbua tena na tena.” Tayari inatusumbua. Unaweza kuisoma katika magazeti, kusikia juu yayo katika habari, na kuiona kwenye televisheni yako. Hiki ni kielelezo kidogo:

Judonne atoa bunduki na kumfyatulia risasi Jermaine mara tatu kifuani. Jermaine amekufa; alikuwa na miaka 15. Judonne ana miaka 14. Walikuwa wamekuwa marafiki wakubwa sana. Walikuwa wakigombania msichana.

Watu mia moja walikusanyika kwenye maziko ya Michael Hilliard mwenye umri wa miaka 16. Alikuwa amepigwa risasi nyuma ya kichwa chake; alipokuwa akiondokea bishano kwenye mchezo wa mpira wa vikapu.

Katika Brooklyn, New York, matineja watatu walichoma nyumba ya wenzi wa ndoa wasio na makao. Alkoholi ya kusugua ilipokosa kufaulu, walijaribu petroli. Hiyo ikafaulu.

Katika Florida mtoto mwenye umri wa miaka mitano alimsukuma mtoto anayetambaa kutoka kwenye ngazi ya orofa ya tano akafa.

Katika Texas mtoto mwenye umri wa miaka kumi alichukua bunduki akamfyatulia risasi mchezaji mwenzake akaushindilia mwili wake chini ya nyumba.

Katika Georgia mvulana mwenye umri wa miaka 15 alimchoma Mwalimu wake mkuu kwa kisu alipokuwa akiadhibiwa.

Katika Jiji la New York, wanagenge wenye kumaliza umri wao wa utineja na wenye miaka ya mapema ya 20, wakiwa na vibao vya kuchezea mpira, mabomba, mashoka, visu, na chombo cha kukatia nyama, walienda kufanya tendo la “jeuri” karibu na kao moja la wanaume wasio na makao wakiumiza wengi na kuacha mmoja akiwa amekatwa kooni. Kusudi lilikuwa nini? Mchunguzi mmoja alieleza: “Walikuwa wakifurahia kuwashambulia wasio na makao.”

Katika Detroit, Michigan, mvulana mwenye umri wa miaka 11 alijiunga na mvulana wa miaka 15 kumlala kinguvu kisichana cha umri wa miaka 2. Yasemekana walimwacha mjeruhiwa wao ndani ya pipa la takataka.

Katika Cleveland, Ohio, wavulana wanne wenye umri wa miaka sita hadi tisa walimlala kinguvu msichana mwenye umri wa miaka tisa katika shule ya msingi. Akizungumza juu ya hilo, mwandikaji safu za magazeti Brent Larkin, akiandika katika Cleveland Plain Dealer, alisema: “Hilo lasema mambo mengi yanayotendeka katika nchi hii, jinsi mifumo yetu ya thamani inavyoelekea kwenye hali mbaya sana.”

Dakt. Leslie Fisher, profesa wa saikolojia katika Cleveland State University, alilaumu televisheni. Aliiita “mashine kubwa ya ngono,” na “watoto wa miaka 8 na 9 wanatazama mambo hayo.” Aliwalaumu wazazi pia kwa ajili ya upunguo wa hali ya familia ya Kiamerika: “Mama na baba wanashughulika sana na matatizo yao wenyewe na hawawezi kuchukua nafasi ya kuwaangalia watoto wao.”

Takataka Ndani, Takataka Nje

Sehemu mbalimbali katika jamii, hasa waeneza habari, watumbuizaji, na shughuli za vitumbuizo—sehemu zinazojipatia faida kwa kuendekeza ule ubaya zaidi katika ainabinadamu—zinamimina ngono na jeuri na ufisadi na hivyo wanachangia sana kushusha wachanga na familia. Kwa hiyo kanuni hii yaendelea: Panda lililooza, vuna lililooza. Takataka ndani, takataka nje. Matokeo hayo yataleta matatizo—nayo yatachukiza mno.

Je! jamii inakuza kizazi cha watoto wasio na dhamiri? Swali hilo lilitokezwa baada ya mchezo wa “kijeuri” wenye sifa mbaya katika Central Park ya New York ambapo mwanamke mwenye umri wa miaka 28 alipigwa na kulalwa kinguvu na genge la matineja wenye kuranda-randa wliomwacha wakidhani amekufa. Polisi walisema kwamba hao walikuwa “wenye kujikinai na wasiojuta” na walipokamatwa “walifanya mzaha, wakaongea na kuimba kwa umoja.” Walitoa sababu za kufanya hivyo: “Ilikuwa inafurahisha,” “Tulikuwa tumechoshwa,” “Lilikuwa ni jambo linalopasa kufanywa.” Gazeti Time liliwaita “wenye kung’olewa na moyo wa kibinadamu” ambao “walikuwa wamepoteza, labda kutositawisha kamwe, ule moyo wa kibinadamu tunaoita dhamiri.”

Gazeti U. S. News & World Report lilisihi: “Ni lazima taifa hili lichukue hatua ili kuzuia kizazi kingine cha watoto wasio na dhamiri.” Dakt. Ken Magid, msaikolojia mashuhuri, na Carole McKelvey wanakazia hatari hiyohiyo kwenye kitabu chao chenye kutoboa mambo High Risk: Children Without a Conscience. Rekodi za matukio yaliyopita na ushuhuda kutoka kwa wasaikolojia na matabibu wa ugonjwa wa akili huunga mkono mateto ya Magid: Kisababishi cha msingi ni ukosefu wa kifungo chenye nguvu kati ya mzazi na mtoto tangu kuzaliwa hadi kwenye miaka ya ukuzi unaofuata.

Kwa kweli, ni lazima familia zikaribiane katika miaka hiyo ya ukuzi inayofuata kabla haijawa kuchelewa mno!

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki