Upendo Wakati wa Mtazamo wa Kwanza na Hata Milele!
“UKIANGALIA watoto baada ya kuzaliwa kwao,” aeleza Dakt. Cecilia McCarton, wa Albert Einstein College of Medicine katika New York, “huwa macho na waangalifu sana kwa mazingira yao. Wanaitikia mama zao. Wanageuka kuelekea itokako sauti. Na wanakodolea macho mama yao kwenye uso.” Na mama huangalia machoni mwa mtoto wake. Ni upendo wakati wa mtazamo wa kwanza—kwa wote wawili!
Kipindi hiki cha kifungo kati ya mama na mtoto hutukia kiasili ikiwa kuzaliwa ni kwa asili, bila ya dawa zinazotuliza hisia za mama na za mtoto. Vilio vyake huchochea kutokezwa kwa maziwa ya mama. Mguso wa ngozi yake kwa mama hutoa homoni ambazo zapunguza kuvuja damu baada ya kuzaa kwake. Mtoto anazaliwa na orodha ya mambo ya ubongo yanayohakikisha shauku—kulia, kunyonya, kupayapaya na kuguguna, kutabasamu na kurusha mateke kwingi kwa kuvuta uangalifu wa mama. Shauku, kwa mama hasa, hufanya iwezekane kwa kitoto kukuza hisi ya upendo na kujali na tumaini. Baba upesi huwa wa maana akiwa umbo lenye shauku. Uhusiano wake hukosa ule ukaribu wa kama ule wa mama lakini zinaongezea sehemu ya maana: mdukuodukuo, kutekenywa, kelele nyororo sana ya kazi za nyumbani, ambazo mtoto anaitikia kwa kicheko chenye kusisimua na mishtukoshtuko.
Dakt. Richard Restak aripoti kwamba kwa wenye kuzaliwa karibuni, kushikwa na kupakatwa ni kama chakula. “Mguso,” asema, “ni wa lazima kwa ukuzi wa kawaida wa mtoto kama vile chakula na oksijeni. Mama anamfungulia mtoto mikono yake, anamlaza karibu sana naye, na mifanyiko mingi ya kisaikobayolojia inapatanishwa.” Chini ya kutenda huko hata ubongo wa kimwili hutokeza “sura tofauti ya vivimbe na mashimo.”
Jilinde Dhidi ya Kutokuwa na Shauku
Wengine wameonyesha kwamba ikiwa shauku hii kati ya mama na mtoto haitaonyeshwa wakati wa kuzaliwa, msiba upo mbele. Si hivyo. Pamoja na umama wenye upendo kuna mamia ya nyakati za ukaribu katika majuma yafuatayo yanayofanya kifungo kiwe salama. Mnyimo wa ukaribu kama huo kwa muda mrefu, hata hivyo, waweza kuongoza kwenye matokeo yenye msiba. “Ingawa sisi sote twahitajiana mmoja na mwenzake katika maisha yetu yote,” Dakt. Restak atuambia, “kuhitaji huko ni kwenye nguvu katika mwaka wa kwanza. Mnyime mtoto mwangaza, nafasi ya kutazama uso wa binadamu, raha ya kubebwa, kupakatwa, kuzungumziwa kwa sauti ya chini, kushughulikiwa, kuguswa—na kitoto hakivumilii kunyimwa huko.”
Watoto hulia kwa sababu nyingi. Kwa kawaida wanataka kuelekezewa fikira. Ikiwa vilio vyao haviitikiwi baada ya muda fulani, huenda wakaacha. Wanahisi kwamba mtunzi wao haitikii. Wanalia tena. Ikiwa bado hakuna itikio, wanahisi wameachwa, hawana usalama. Wanajaribu zaidi. Ikiwa hilo linaendelea kwa muda mrefu zaidi na ikiwa inarudiwa mara nyingi, mtoto anahisi kuwa ameachwa. Kwanza anakasirika, hata anaghadhabika, na mwishowe anaacha. Kutokuwa na shauku kwatokea. Akiwa hapokei upendo, hajifunzi kupenda. Dhamiri haikuzwi. Hatumaini yeyote, hajali yeyote. Anakuwa mtoto mwenye shida na, katika hali za kupita kadiri, mwenye utu wa jeuri bila uwezo wa kuhisi majuto kwa ajili ya matendo ya uhalifu.
Upendo wakati wa mtazamo wa kwanza sio mwisho wake. Ni lazima uendelee hata milele. Si kwa maneno tu bali kwa matendo pia. “Tusipende kwa neno, wala kwa ulimi, bali kwa tendo na kweli.” (1 Yohana 3:18) Kukumbatia kwingi na busu nyingi. Mapema, kabla haijawa kuchelewa mno, fundisha na kuagiza katika thamani za kweli za Neno la Mungu, Biblia. Halafu hali ya watoto wako itakuwa kama ilivyokuwa kwa Timotheo: “Tangu utoto umeyajua maandiko matakatifu, ambayo yaweza kukuhekimisha.” (2 Timotheo 3:15) Kila siku tumia wakati pamoja nao, kuanzia utoto na miaka ya utineja. “Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako; nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo.”—Kumbukumbu la Torati 6:6, 7.
‘Huenda Tukalia, lakini Inafaa Zaidi’
Nidhamu ni habari yenye kugusa hisia kwa wengi. Hata hivyo, inapotekelezwa vizuri, ni sehemu muhimu ya upendo wa mzazi. Msichana mdogo mmoja alitambua hili. Alimtengenezea mama yake kadi, iliyoandikwa “Kwa Mama, Kwa Bibi Mzuri.” Ilikuwa imepambwa kwa michoro yenye rangi ya jua la dhahabu, ndege wenye kuruka, na mauwa mekundu. Kadi hiyo ilisomeka hivi: “Hii ni yako kwa sababu sote tunakupenda. Tunataka kuonyesha uthamini wetu kwa kutengeneza kadi. Tunapokuwa na maksi za chini unatia sahihi karatasi yetu. Tunapokuwa wabaya unatuchapa. Huenda tukalia, lakini tunajua ni kwa ajili ya faida yetu. . . . Ninalotaka kusema ni kwamba nakupenda sana, sana. Asante kwa yale yote unayonifanyia. Upendo na busu nyingi. [Iliyotiwa sahihi] Michele.”
Michele anakubaliana na Mithali 13:24: “Yeye asiyetumia fimbo yake humchukia mwanawe; bali yeye ampendaye humrudi mapema.” Kutumia fimbo, inayowakilisha mamlaka, huenda ikahusisha kuchapa, lakini mara nyingi sivyo. Watoto tofauti, tabia tofauti, hutaka nidhamu tofauti. Karipio lenye kutolewa kwa fadhili huenda likatosha; utundu huenda ukahitaji jambo lenye nguvu zaidi: “Lawama hupenya moyoni mwa mwenye ufahamu, kuliko mapigo mia moyoni mwa mpumbavu.” (Mithali 17:10) Pia yenye kutumika ni: “Haitoshi mtumwa [au mtoto] kuonywa kwa maneno; maana ajapoyafahamu hataitika.”—Mithali 29:19.
Katika Biblia neno “nidhamu” humaanisha kufundisha, kuzoeza, kurudi—kutia ndani kuchapa ikiwa inahitajiwa ili kurekebisha tabia. Waebrania 12:11 inaonyesha kusudi layo: “Kila adhabu [nidhamu, NW] wakati wake haionekani kuwa kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini baadaye huwaletea wao waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani.” Wazazi hawapaswi kuwa wakali kupita kiasi wanapotoa nidhamu: “Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa.” (Wakolosai 3:21) Wala hawapaswi kuwa waendekevu kupita kiasi: “Fimbo na maonyo hutia hekima; bali mwana aliyeachiliwa humwaibisha mamaye.” (Mithali 29:15) Kuendekeza husema, ‘Fanya upendavyo; usinisumbue.’ Nidhamu husema, ‘Fanya linalofaa; Ninakujali.’
Gazeti U.S. News & World Report, la Agosti 7, 1989, lilisema kwa usahihi: “Wazazi wasiotoa adhabu kwa ukali, lakini huweka mipaka imara na kuishikilia, yaonekana sana kwamba watatokeza watoto wenye kufaulu sana na wenye kupatana vizuri na wengine.” Katika umalizio wayo makala hiyo ilitaarifu: “Labda kichwa kikuu chenye kushtua kinachozuka kutokana na habari yote ya kisayansi ni kwamba kuweka kiolezo cha upendo na tumaini na mipaka inayokubalika ndani ya kila familia ndilo jambo la muhimu, wala si mambo mengi ya kirasmi. Lengo hasa la nidhamu, neno lililo na chanzo kile kile cha Kilatini mwanafunzi, si kuadhibu watoto watundu bali kuwafundisha na kuwaongoza na kuwasaidia waingize udhibiti wa kindani.”
Wanasikia Unalosema, Wanaiga unalofanya
Makala juu ya nidhamu katika The Atlantic Monthly ilitangulizwa na taarifa hii: “Mtoto anaweza kutazamiwa ajiendeshe vizuri ikiwa tu wazazi wake wanaishi kulingana na thamani wanazofundisha.” Makala hiyo iliendelea kuonyesha thamani za udhibiti wa kindani: “Matineja waliojiendesha vizuri walielekea kuwa na wazazi ambao wenyewe walikuwa watu wenye kujali madaraka, wanyofu, na wenye kujinidhamu—ambao waliishi kulingana na viwango walivyotoa na waliwatia moyo watoto wao wafuate mfano huo. Matineja wazuri walipowekwa wazi, hiyo ikiwa sehemu ya uchunguzi huo, kwa matineja wenye taabu, tabia yao haikuathiriwa daima. Walikuwa wametunza sana viwango vya wazazi wao.” Ilithibitika kuwa kama Mithali isemavyo: “Mlee mtoto katika njia impasayo, naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee.”—Mithali 22:6.
Wazazi waliojaribu kuingiza viwango vya kweli ndani ya watoto wao, lakini ambavyo wao wenyewe hawakufuata, hawakuwa na mafanikio. Watoto wao “hawakuweza kutunza kindani thamani hizo.” Uchunguzi huo ulithibitisha kwamba “lililofanya hali iwe tofauti ni kadiri ambayo wazazi waliishi kulingana na viwango ambavyo walijaribu kuwafundisha watoto wao.”
Inathibitika kuwa kama mwandikaji James Baldwin alivyosema: “Watoto hawajawahi kuwa wazuri sana kwa kuwasikiliza wakubwa wao, lakini hawajawahi kukosa kuwaiga.” Ikiwa unapenda watoto wako na unataka kuwafundisha thamani za kweli, tumia njia iliyo bora zaidi ya zote: Uwe mfano wa mafundisho yako mwenyewe. Usiwe kama waandishi na Mafarisayo ambao Yesu alilaumu kuwa wanafiki: “Basi yo yote watakayowaambia, myashike na kuyatenda; lakini kwa mfano wa matendo yao, msitende; maana wao hunena lakini hawatendi.” (Mathayo 23:3) Au kama wale mtume ambao Paulo aliwauliza kwa kuwashtaki: “Basi wewe umfundishaye mwingine, je! hujifundishi mwenyewe? Wewe uhubiriye kwamba mtu asiibe, waiba mwenyewe?”—Warumi 2:21.
Leo wengi huiachia mbali Biblia eti ni ya kizamani na miongozo yake kuwa isiyotumika. Yesu akana nia hiyo kwa maneno haya: “Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa watoto wake wote.” (Luka 7:35) Masimulizi yanayofuata ya familia kutoka nchi mbalimbali yanathibitisha maneno yake kuwa kweli.
[Picha katika ukurasa wa 7]
Kifungo cha karibu pamoja na mama humsaidia mtoto akue kihisia-moyo
[Picha katika ukurasa wa 8]
Wakati wa baba pamoja na mtoto ni wa muhimu pia