Watoto Wengi Walio na Mkazo wa Akili
“RANDY!” Rita akapaaza sauti, akiogofywa na aliloona kutoka kwa mbali alipokuwa akiikaribia nyumba yake. Mtoto wake Randy, alikuwa ameangikwa nje ya dirisha la chumba cha kulala cha orofa ya juu, meta nane kutoka kwenye veranda yenye simiti. Akiwa ndani ya nyumba, Larry alisikia vilio visivyozuilika vya mke wake na akaamka mara moja. Akikimbia juu kwenye ngazi, aliruka ndani ya chumba cha kulala na kumshika Randy, akimvuta ndani kwa usalama. Wazazi wa Randy walitaka majibu ya upesi. “Kwa nini ulifanya hivyo? Kwa nini?” wakauliza kwa mshangao. “Ungeumia; ungeuwawa!”“Nilitaka kufa,” Randy akajibu bila kujali. Randy alikuwa na umri wa miaka mitano tu.
KWA sura yake ya nje, Randy alionekana kuwa kijana aliye timamu na mwenye afya. Hakuna aliyedhania kwamba alitaka kufa kisiri. Hata hivyo, uchunguzi wa baadaye ulionyesha kwamba Randy alikuwa mtoto aliye na mkazo mkali sana wa akili.
Kama vile Randy watoto wengi zaidi leo hupatwa na masumbuko makubwa. Wengine wao wanaposhindwa kupata njia zinazofaa za kukabiliana na mikazo yao, wanajaribu kukandamiza tu hangaiko lao. Lakini mkazo uliokandamizwa hatimaye hupata njia ya kujitokeza. Kwa wengine, hangaiko ambalo haliwezi kuzungumziwa litasababisha ugonjwa wa kimwili au tabia mbaya. Kwa wengine, mkazo wa akili utasababisha matendo ya kujiangamiza, kutia ndani kujiumiza mwenyewe, matatizo ya ulaji, kutumia vibaya vitu kama vileo na dawa za kulevya, na hata kujiua. Kitabu The Child in Crisis chasema: “Mengi ya matatizo hayo—hasa kujiua—yalionekana kuwa mambo ya watu wazima au vijana wakubwa. Sasa yanaonekana yakipenya polepole kwa wachanga zaidi.”
‘Hilo lawezekanaje?’ watu wazima wenye mshangao wanauliza. ‘Je! wakati wa utoto si wakati wa vibaramwezi na kucheza, wakati wa kucheka na kufurahi?’ Kwa watoto wengi jibu ni la. “Utoto kuwa wakati wa raha kabisa ni mawazo yasiyo ya kweli yanayofanyizwa na watu wazima,” adai Dakt. Julius Segal. Uhalisi huo wenye kuhuzunisha unahakikishwa na tabibu Joseph Lupo: “Nimekuwa nikishughulika na mambo ya kitiba kwa miaka ishirini na mitano. Siku hizi naona ongezeko la mara nne la watoto na vijana wanaougua mkazo wa akili.”
Ni nini linalosababisha mkazo wa akili wa aina hiyo usio na kifani kwa watoto? Kuna ishara zipi za maonyo? Watoto walio na mkazo wa akili wanaweza kusaidiwaje? Maswali haya yatashughulikiwa katika makala zifuatazo.